Saturday, 4 January 2014

WAFUASI WA CHADEMA WAZITWANGA MAHAKAMANI

Filled under:



Vurugu za aina yake zimezuka katika Mahakama Kuu jijini Dar es Salaam, baada ya watu wanaodhaniwa kuwa wanachama wa Chadema  kumzomea aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa Chama hicho,  Zitto Kabwe.
 
Vurugu hizo zilihusisha wafuasi wa chama hicho wanaomuunga mkono Zitto na wale wanaompinga, ambao walikuwa wamebeba mabango ya kumsifia na wengine wakiwa wamebeba ya kumkashifu.
Katika vurugu hizo, baadhi ya wanachama hao waliamua kufanya doria isiyo rasmi ndani ya mahakama hiyo ya kuwasaka watu waliodai kuwa ni mamluki,  huku wakimkamata askari kanzu, kabla ya kumpiga ngumi na kumchania shati mtu mmoja wakidai kuwa alikuwa akiwarekodi kwa kutumia simu yake ya mkononi.
Tukio hilo la aina yake lilitokea jana asubuhi ambapo kundi la wanachama hao, huku baadhi wakiwa wamevaa nguo za kaki zinazotumiwa na chama hicho kufika katika mahakama hiyo kwa lengo la kusikiliza  kesi ya pingamizi iliyofunguliwa na Zitto. 
Mara baada ya kuwasili kwa Mbunge huyo wa Kigoma Kaskazini, huku akiwa ameongozana watu kadhaa wakiwamo wanasheria wake na mabaunsa, wanachama hao walianza kumzomea huku baadhi wakimwita fisadi.
Hali hiyo iliibua zogo katika eneo la mahakama hiyo, hali iliyowalazimu maofisa kadhaa wa polisi kuingilia kati kwa kuamua kumchukua Zitto na kumhifadhi kwenye chumba maalumu na kumtoa saa 6 mchana kesi yake ilipoanza kusikilizwa.  Baadhi ya mabango ya kumkashifu  yalisomeka; Zitto tulimpenda, CCM imempenda zaidi, Zitto rudisha fedha za CCM.
Yale yaliyomsifia yalisomeka; Zitto kama Mandela na Zitto ni Mkombozi.Baada ya kumalizika kusikilizwa kwa kesi hiyo, saa 12 jioni wanachama hao walianza kurushiana ngumi, hasa baada ya kuibuliwa kwa mabango yaliyosomeka ‘Zitto kwanza Chadema baadaye’.
Awali hali hiyo ilimfanya Zitto kutaharuki, huku mabaunsa wake wakijihami na kuanza kumlinda.
Baada ya Zitto kuhifadhiwa baadhi ya wanachama hao ambao waliingia kwa kuandikishwa majina yao getini, walianza kuwasaka watu waliowahisi  kuwa mamluki, ambapo walimnasa askari kanzu na kuanza kumzonga wakimuhoji anapeleleza nini katika eneo hilo.
“Hapa tunataka kujua wewe ni nani na unataka nini hapa, maana hatukuelewi kabisa kwa nini unakuja kusikiliza mazungumzo yetu, jitambulishe,” alisisika mmoja wa wanachama hao akimhoji askari huyo huku akiwa amemkandamiza ukutani,
“Tunajua wewe ni askari kwa nini hujavaa sare leo? Kisha unajichanganya kwenye kundi letu.”
Kesi hiyo ilimalizika saa 12 jioni ambapo Zitto alitolewa chini ya ulinzi mkali wa polisi kwa kupitia mlango wa nyuma wa mahakama hiyo na kuwaacha wafuasi hao wakionyeshana ubabe kwa mabango na kauli za kejeli.

Kabla ya kuanza kwa kesi hiyo, Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu alimwomba Jaji John Utamwa kuendesha kesi hiyo kwa lugha ya Kiswahili kwa kuwa inagusa  sehemu ya masilahi ya umma, jambo ambalo liliibua shangwe kwa wafuasi wa chama hicho waliokuwa wamefurika katika mahakama hiyo.
Hata hivyo baada ya kesi kuanza kuendeshwa kwa lugha  ya Kiswahili,  Jaji Utamwa alilazimika kuikatiza, na kuwakemea wanachama wa Chadema baada ya sauti za kuguna kusikika wakati wakili wa Zitto,  Albert Msando alipokuwa akiwasilisha hoja kuhusu msingi wa kesi hiyo.
“ Nataka kuwakumbusha hapa mahakamani ni tofauti na sehemu nyingine sauti zinazosikika sizitaki, anayeona kwamba yanayozungumzwa hakubaliani nayo kama hawezi kunyamaza atoke nje vinginevyo hatua za kisheria zitachukuliwa,” alisema Jaji Utamwa.
 Kundi la Wanachadema hao huku wengine wakiwa wamevalia sare zao waliwasili mahakamani hapo ili kusikiliza kesi ya pingamizi iliyofunguliwa na Kabwe akiiomba Mahakama iwazuie Bodi ya Wadhamini wa Chadema, Katibu Mkuu pamoja na Kamati Kuu ya Chadema jana kumjadili, kumchukulia hatua, uamuzi wowote wala kuhusu uanachama wake.
Juzi Zitto aliomba  Mahakama hiyo kuzuia Kikao cha Kamati Kuu ya Chadema  kumjadili hadi rufaa yake aliyoikata kwenye Baraza Kuu  la Chadema  itakaposikilizwa na kuamuliwa na wazuiwe kumwingilia katika utekelezaji wa majukumu yake ya ubunge wa Kigoma Kaskazini .
Pia aliiomba Mahakama hiyo Kuu kumwamuru  Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Wilbroad Slaa  ampatie nakala ya mashtaka na maelezo ya uamuzi uliofikiwa na  Kamati Kuu  Novemba 22, 2013 na kusababisha avuliwe nyadhifa zake ili aweze kupeleka rufaa yake Baraza Kuu la Chadema kupinga uamuzi huo.

Posted By Unknown02:55

Friday, 3 January 2014

NAPE AFUNGUKA KWA WALE WANAOTANGAZA KUWANIA URAISI KABLA YA MUDA

Filled under:



Chama Cha Mapinduzi (CCM), kimesema mwanachama yeyote anayetangaza nia ya kuwania nafasi ya urais kabla ya muda mwafaka kutangazwa, anapoteza sifa ya kuwa mgombea.
 
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alisema Dar es Salaam jana kwamba chama hicho kinaamini katika umoja na mshikamano na kwamba wanaotangaza nia ya kugombea urais kabla ya muda wamepoteza sifa kwa kuwa ni kama wanakigawa.
Juzi, Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa alitangaza nia ‘kimtindo’ akisema anaanza rasmi safari aliyoiita ya matumani ya ndoto zake, ambayo pia itatimiza ndoto za Watanzania za kupata elimu bure, maji safi na maendeleo ya uhakika.
Lowassa ambaye amekuwa akitajwa kuwa mmoja wa wagombea wa nafasi ya urais kupitia CCM katika Uchaguzi Mkuu wa 2015, alitangaza hayo katika ibada ya shukrani ya kuupokea mwaka mpya, katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Usharika wa Monduli.
Nape alisema wanaotangaza nia ya kuwania urais hivi sasa wanafahamu kwamba hawana sifa za kuwa wagombea wa nafasi hizo kwa sababu mbalimbali.
Alisema wanafahamu wazi kwamba vikao vya chama havitawapitisha kutokana na kutuhumiwa kwa rekodi zao pia ni mbaya.
Suala hili liko wazi katika chama chetu, viongozi wenye sifa waliowahi kuongoza nchi hii hawakujitangaza mapema. Walisubiri na muda ulipofika wakatangaza nia ya kuwania,” alisema Nape.
Alisema kwa hao wanaojitangaza hivi sasa kabla muda, wanakigawa chama na kwamba vikao havitawapitisha labda wafanye hivyo kupitia vyama vingine.
Labda wagombee urais kupitia vyama vingine lakini si CCM, chama hiki kina misingi na taratibu zake, wanachama wanashikamana hadi muda utakapofika,” alisema.
Alisema viongozi bora hawapatikani kwa kujiandaa wao wenyewe kuchukua nafasi hizo, bali kwa kuombwa na wanachama wenzao katika hatua mbalimbali zinazokubalika.
Oktoba mwaka jana, Rais wa Zanzibar, Dk Mohamed Ali Shein alielezea kushangazwa na tabia ya baadhi ya wanachama wa CCM kutangaza nia ya kuwania nafasi za uongozi kwa uchaguzi wa 2015 ikiwamo nafasi ya urais wakati wahusika wa nyadhifa hizo bado hawajamaliza muda wao.

Akifungua Mkutano wa Makatibu wa CCM wa Mikoa, Dk Shein aliwataka watu hao kusubiri hadi chama kitakapotoa mwongozo.
Katika ziara ya Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana kwenye mikoa ya Kusini na Nyanda za Juu Kusini, mwishoni mwa mwaka jana, alisema wanaotangaza nia mapema, wanajitengenezea mazingira magumu ndani ya chama.
Mbali na Lowassa, wengine wanaotajwa kuwania nafasi hiyo ni pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Benard Membe, Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta, Mbunge wa Songea Mjini, Dk Emmanuel Nchimbi na Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Januari Makamba.

Posted By Unknown10:00

LISSU AWATOA HOFU WANANCHI KUHUSU SERIKALI TATU

Filled under:



Mnadhimu Mkuu wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Tundu Lissu, amewataka wananchi wanaohofia muundo wa serikali tatu kutokuwa na wasiwasi na muundo huo.

Akizungumza jana jijini Dar es salaam, Lissu alisema kuwa hofu inayojengwa ya ukubwa wa gharama za uendeshaji ni ya kufifisha jitihada za tume ya Katiba, ambayo haina msingi wala ushahidi.

Alisema kuwa rasimu ya pili ya Katiba imeeleza mambo saba ya msingi ambayo ni Katiba na mamlaka ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ulinzi na Usalama wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Uraia na Uhamiaji,  Sarafu na Benki Kuu, Mambo ya Nje,     Usajili wa Vyama vya Siasa,  Ushuru wa Bidhaa na Mapato yasiyo ya kodi yatokanayo na mambo ya Muungano.

Lissu alisema anaamini Serikali ya Muungano haitakuwa na gharama kubwa katika uendeshaji wake kwani haitazidi mawaziri saba.

Alisema kabla ya kuanza kuhoji muundo wa serikali tatu uliopendekezwa katika rasimu hiyo ni vema wakahoji serikali ya sasa inatumia gharama kiasi gani.

“Nani anajua gharama ya kuendesha serikali kwa sasa, watu waache kutishwa na maneno yasiyo ya msingi, kwa hili mimi naona ni jema,” alisema.

Pia alisema rasimu hiyo kama itakuwa katiba, kitendo cha kutumika kwa miaka minne ikiwa katika kipindi cha mpito ni jambo jema na litafungua milango ya kutungwa sheria ndogo ndogo kwa wakati huo.

Posted By Unknown08:40

CHADEMA YATOA UFAFANUZI KUHUSU PINGAMIZI ALILOWEKA ZITO KABWE MAHAKAMANI

Filled under:

 
Mmoja wa wanachama watatu wa CHADEMA waliovuliwa nafasi zao za uongozi ndani ya chama, Zitto Kabwe kupitia kwa Wakili wake, Alberto Msando, leo ameanza kufanya ‘FORUM SHOPPING’ kwa kupeleka maombi Mahakama Kuu ya Tanzania, akiomba Kamati Kuu isijadili na kuamua jambo lolote kuhusu uanachama wake, kwenye kikao maalum kinachofanyika kesho.

Awali muombaji kwa namna ambayo inaweza kuitwa kuwa ni kuvizia, alitaka Mahakama Kuu hiyo itoe amri kutokana na ombi lake hilo, bila upande wa chama kuwepo mahakamani, lakini kwa bahati nzuri mawakili wa chama, Mwanasheria Mkuu wa chama, Tundu Lissu na Mkurugenzi wa Sheria na Haki za Binadamu, Peter Kibatala; wakafanikiwa kuwepo kortini, hivyo wakawa-served maombi hayo kisha mahakama ikalazimika kusikiliza Preliminary Objections (PO) kutoka kwa mawakili wa CHADEMA dhidi ya waleta maombi.

Maombi hayo ya wakili Msando kwa niaba ya Zitto yamefunguliwa mahakamani dhidi ya Baraza la Wadhamini CHADEMA na Katibu Mkuu wa Chama.

Hoja za mawakili wa CHADEMA katika PO zilikuwa ni katika maeneo matatu ambayo ni vifungu vya kisheria ambavyo waombaji walikosea;

1. Vifungu vya sheria walivyotumia waombaji kuomba court injunction, haviipatii Mahakama Kuu mamlaka ya kufanya maamuzi hayo wanayoomba ifanye. Kwa sababu kwa ujumla ukikosea vifungu hasa vinavyohusu msingi wa kesi, ni sawa na kwamba hakuna kesi.

2. Hati ya kiapo ya waleta maombi haikuwa na facts kama inavyotakiwa badala yake ilikuwa imejaa maneno ya ubishi ubishi.

3. Mahakama haiwezi ku-entertain kusikiliza migogoro ya ndani katika vyama vya hiari mf; vyama vya siasa, dini na michezo (ambavyo uanachama wake ni wa hiari), kwa sababu mojawapo ya principle ni kwamba ili mtu awe mwanachama anakuwa amekubaliana na katiba, kanuni, taratibu na makatazo ya chama husika.

Aidha katika maombi yake kuna vitu vingine ‘muhimu’ ambavyo mleta maombi amejikuta akivionesha kuwa anakubaliana na taratibu za chama lakini wakati huo huo tena anataka mahakama imsikilize;

· Amekiri kuwa amevuliwa nafasi za uongozi na amekata rufaa

· Amekiri kuwa ameandikiwa mashtaka kwa maandishi na yeye amejibu

· Amekiri kuwa ameandikiwa kuitwa mbele ya kikao cha Kamati Kuu ili asikilizwe utetezi wake kwa mdomo.

Kwa maneno yake hayo ni kwamba anakubaliana na na process ya chama na kwamba anajua atasikilizwa lakini tena wakati huo huo anataka mahakama imsikilize. Huo ndiyo msingi wa Mwanasheria Mkuu wa CHADEMA kusema kuwa kuhangaika huko ni sawa na kufanya ‘FORUM SHOPPING’.

Mleta maombi angeweza kuwa na hoja katika maombi yake iwapo angeona kuna breach of natural justice kwenye suala lake. Kitu ambacho hakijatokea na hata yeye kwenye maelezo yake anakiri hivyo.

Uamuzi wa Mahakama Kuu

Katika uamuzi wake, Jaji Utamwa amesema chama kitaendelea na shughuli zake kama kawaida.

Hivyo kikao maalum cha Kamati Kuu kilichopangwa kufanyika kesho Januari 3, 2014, kitafanyika na kitajadili agenda zote (kama zilivyotolewa awali) na masuala yote yanayohusu uendeshaji wa chama, isipokuwa hakitajadili na kuamua kuhusu uanachama wa Zitto pekee, hadi Mahakama Kuu itakaposikiliza ombi lake kesho saa 3 asubuhi.

Posted By Unknown08:25

WAWILI WASHIKIRIWA NA POLISI CHANZO KUKAMATWA NA MENO 81 YA TEMBO

Filled under:



Watu wawili wanashikiliwa na polisi nchini Tanzania baada ya kukamatwa na shehena ya meno ya tembo katika bandari ya Dar es Salaam, waliyokuwa wakisafirisha kiharamu maafisa wa nchi hiyo wamesema.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Msemaji wa Wizara ya Maliasili na Utalii wa Tanzania, Chikambi Rumisha amesema meno hayo yapatayo 81 yana uzito wa kilo 303.

Kwa mujibu wa maafisa wa Wizara meno hayo ya tembo ni mapya ikiwa na maana yametokana na tembo 41 waliouawa ndani ya mwezi mmoja uliopita.

Naibu Waziri wa Maliasiali na Utalii wa Tanzania Lazaro Nyalandu amesema mauaji ya tembo yameongezeka nchini Tanzania baada ya operesheni ya kupambana na majangili iliyopewa jina la "Operesheni 

Tokomeza" kusimamishwa kutokana na baadhi ya watendaji kukiuka haki za binadamu.
Mapema wiki hii Naibu Waziri huyo amesema tembo wapatao 60 wameuawa kati ya mwezi Novemba na Decemba ikilingalishwa na tembo wawili waliouawa mwezi Octoba.

Posted By Unknown07:47

HEKAHEKA ZAWAKUMBA WAKAZI WA DAR KUHOFIA BOMU

Filled under:



Wakazi na wapita njia katika makutano ya barabara ya Morogoro na Shekilango,  jana walikumbwa na hofu kufuatia kuzagaa kwa taarifa ya kuonekana kwa kitu kinachodhaniwa kuwa  ni bomu la kutupa kwa mkono ambalo lilikuwa ardhini eneo hilo, jirani na maghorofa ya Shirika la Nyumba la Taifa (NHC).

Shughuli hiyo ilizuka kunako saa tano na robo za asubuhi na kudumu kwa zaidi ya saa moja, kulitokana na mkazi mmoja wa jijini, Alfani Zidadu kuona kitu kilichokuwa ardhini ambacho kilishabihiana na bomu hali ambayo ilimfanya awasiliane na mama yake ambaye alikuwa na miadi ya kukutana nae eneo hilo.

Zidadu alisema kuwa mama yake, Asha Zidadu alikuwa anakaribia eneo la tukio na alipofika eneo hilo alimuonyesha kitu hicho na muda mfupi baadae aliwasiliana na polisi Urafiki ambao walifika na baada ya kukiona kitu hicho walizungushia uzio eneo hilo.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Camillius Wambura alikiri kuwepo kwa tukio hilo lakini alikataa kuingia kwa undani kuhusiana na kitu hicho iwapo ni bomu au la kwa madai kuwa polisi wanakifanyia uchunguzi ili kujua ni kitu gani hasa.

“Kwa sasa siwezi kusema kuwa ni bomu au la isipokuwa tunasubiri uchunguzi kujua kilikuwa ni kitu gani hasa” alisema Kamanda Wambura na kubainisha kuwa kwa sasa anaweza kusema kuwa ni mabaki ya vipande vya mabati.

Wananchi wakitawanywa na kutakiwa kuwepo mita 100 kutoka eneo la tukio kwa maelezo kuwa iwapo litalipuka linaweza kusababisha wakapoteza maisha.

“Ondokeni hapa, simameni huko” alisema askari aliyekuwa ameshika bunduki ya kufyatulia mabomu ya machozi na kuongeza kuwa wateguaji wangefika eneo hilo wakati wowote na iwapo makosa yatafanyika wakati wa kulitegua wananchi walio jirani na eneo hilo wangeweza kupoteza maisha.

Askari wa kikosi maalum cha kutegua mabomu ilifika eneo hilo na kuanza kazi ya kuchimba na kuweka tahadhari zote za kuzuia lisilipuke na msimamizi wa operesheni hiyo ambaye alikataa kutaja jina lake aliwataka askari wanaotegua kuhakikisha pini ya bomu hilo imekaza na ipo katika sehemu yake.

“Hakikisheni pini imekaza na hata kama imelegea irudishieni” alisema msimamizi huyo na baada ya kufukuliwa kwa kitu hicho kinachodhaniwa kuwa ni bomu, kiliwekwa katika mfuko wa karatasi na kufungiwa katika sanduku maalum ambalo walifika nalo eneo hilo la tukio.

Baadhi ya watu waliozungumza  walionyeha mshangao kuhusiana na kitu hicho na kuhoji kuwa iwapo ni bomu ambalo limetegwa lilikuwa limemlenga nani kwani wengi wa watu wanaoshinda eneo hilo ni wale wa bodaboda na abiria wanaosubiria mabasi ya kwenda Mwenge kupitia Sinza.

Sijui mlengwa alikuwa nani lakini ni bomu kabisa kama yale ambayo huwa tunayaona katika luninga
alisema muosha magari katika eneo hio aliyejitambulisha kwa jina la Ibrahim Momba na kuongeza kuwa huenda kuna harufu ya ugaidi katika tukio hilo.

Posted By Unknown07:35

SERIKALI ITAWEKA HADHARANI SABABU ZA KIFO CHA MH.MGIMWA

Filled under:


Serikali imesema itaweka wazi kilichomuua Dk William Mgimwa Jumapili, huku Katibu wa aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Kalenga mkoani Iringa, Martini Simangwa akisema marehemu Mgimwa atazikwa Jumatatu katika Kijiji cha Magunga kilichopo Kata ya Maboga mkoani Iringa.

Mwili wa Dk Mgimwa aliyekuwa Waziri wa Fedha, unatarajiwa kuletwa nchini kesho ukitokea Pretoria, Afrika Kusini. Mgimwa alifariki dunia katika Hospitali ya Kloof Medi-Clinic iliyoko Pretoria alikokwenda kwa matibabu.

Wakati hayo yakielezwa, Serikali imeahidi kuweka wazi kilichomuua Dk Mgimwa wakati wa kumuaga marehemu Jumapili kwenye Viwanja vya Karimjee, Dar es Salaam.

Mwenyekiti wa Kamati ya Mazishi na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu na Bunge,William Lukuvi, alisema kuwa kwa sasa ni mapema kueleza kilichomuua Dk Mgimwa.

Akizungumza nyumbani kwa marehemu, Msemaji wa familia, Charles Nyato alisema mwili utawasili saa 7.00 mchana kwa ndege ya Shirika la Ndege la Afrika Kusini (SAA) na kupelekwa nyumbani kwake Mikocheni B, Mtaa wa Ruvu.

“Baada ya shughuli ya kuaga, siku hiyohiyo, mwili utasafirishwa kwa ndege kwenda kijijini, Magunga ukipitia Iringa mjini kutoa nafasi kwa wananchi kutoa heshima za mwisho kisha kwenda kijijini ambako mwili utalala kabla ya mazishi Jumatatu,” alisema Nyato.
Rais wa zanzibar atuma salamu
Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein amemtumia salamu za rambirambi Rais Jakaya Kikwete kutokana na kifo cha Waziri wa Fedha, Dk William Mgimwa.

Katika salamu hizo, Dk Shein amemwelezea marehemu kwamba atakumbukwa kutokana na utumishi wake uliotukuka kwa Serikali na wananchi wa Tanzania.

“Tanzania imempoteza kiongozi shupavu, mpenda kazi, mzalendo na mtu mwenye busara na upendo kwa wenzake,” alisema.
Naye mtoto wa marehemu, Godfrey Mgimwa akizungumzia kifo cha baba yake alisema: “Kifo cha mzee ni pigo kubwa sana kwetu, inauma ila ndiyo mipango ya Mungu.

“Mzee alikuwa ni mtu anayependa haki na mpenda maendeleo, kiongozi bora na alikuwa akifanya kazi vizuri serikalini. Tumempoteza mtu muhimu sana,” alisema Godfrey kwa upole.

“Mzee alikuwa na kawaida ya kwenda kuangalia hali ya afya yake na alikwenda Afrika Kusini kutokana na mazingira yake ya kazi, lakini kilichosababisha kifo bado hatukijui,” alisema Godfrey.

Mbunge wa Namtumbo Mkoa wa Ruvuma (CCM), Vita Kawawa alisema kifo cha Dk Mgimwa ni pigo kubwa serikalini, jamii na jimboni kwa jumla.

Naibu Katibu Mkuu wa CCM, Mwigulu Nchemba alisema: “Chama na Taifa kimempoteza mtu makini na muhimu kutokana na kuwajibika ipasavyo, alifufua vyanzo vya mapato vilivyokuwa vimejificha.

“Ameondoka wakati tunamuhitaji...mara ya mwisho nakumbuka alisema ana matatizo ya figo sasa sijui ndio kilichosababisha kifo chake au la lakini tusubiri ripoti ya madaktari.”

Naye Naibu Waziri wa Fedha, Saada Mkuya Salum alisema: “Tangu nianze kufanya kazi sijawahi kukutana na kiongozi kama Dk Mgimwa. Alikuwa kiongozi na msikilizaji wa mawazo yanayotolewa na wengine, ametufundisha jinsi ya kuwa kiongozi.”
Aliongeza “Tumempoteza mtu muhimu kutokana na weledi wake katika kazi. Taifa, wapigakura wake na wananchi kwa ujumla tutamkumbuka kwa uongozi wake madhubuti.”

Posted By Unknown07:18