Friday, 3 January 2014

LISSU AWATOA HOFU WANANCHI KUHUSU SERIKALI TATU

Filled under:



Mnadhimu Mkuu wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Tundu Lissu, amewataka wananchi wanaohofia muundo wa serikali tatu kutokuwa na wasiwasi na muundo huo.

Akizungumza jana jijini Dar es salaam, Lissu alisema kuwa hofu inayojengwa ya ukubwa wa gharama za uendeshaji ni ya kufifisha jitihada za tume ya Katiba, ambayo haina msingi wala ushahidi.

Alisema kuwa rasimu ya pili ya Katiba imeeleza mambo saba ya msingi ambayo ni Katiba na mamlaka ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ulinzi na Usalama wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Uraia na Uhamiaji,  Sarafu na Benki Kuu, Mambo ya Nje,     Usajili wa Vyama vya Siasa,  Ushuru wa Bidhaa na Mapato yasiyo ya kodi yatokanayo na mambo ya Muungano.

Lissu alisema anaamini Serikali ya Muungano haitakuwa na gharama kubwa katika uendeshaji wake kwani haitazidi mawaziri saba.

Alisema kabla ya kuanza kuhoji muundo wa serikali tatu uliopendekezwa katika rasimu hiyo ni vema wakahoji serikali ya sasa inatumia gharama kiasi gani.

“Nani anajua gharama ya kuendesha serikali kwa sasa, watu waache kutishwa na maneno yasiyo ya msingi, kwa hili mimi naona ni jema,” alisema.

Pia alisema rasimu hiyo kama itakuwa katiba, kitendo cha kutumika kwa miaka minne ikiwa katika kipindi cha mpito ni jambo jema na litafungua milango ya kutungwa sheria ndogo ndogo kwa wakati huo.

1 comments:

  1. That right changes soja,we keep up together forever.

    ReplyDelete