WATU watatu, akiwemo mtumishi wa Benki ya NMB, wamepandishwa kizimbani
katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kujibu mashitaka 13, yakiwemo ya
kuiibia benki hiyo zaidi ya sh. bilioni moja na kutakatisha fedha
haramu.
Mtumishi wa benki hiyo, Mtoro Suleiman, Daudi Kindamba na John
Kikopa, walisomewa mashitaka hayo jana na Wakili wa Serikali Pius Hilla,
mbele ya Hakimu Mkazi Hellen Riwa.
Hilla aliwasomea washitakiwa hao mashitaka ya kula njama, kuiibia
benki hiyo sh. 1,029,454,383, kufanya udanganyifu, kutakatisha fedha na
kuisababishia benki hiyo hasara ya kiasi hicho.
Washitakiwa hao wanadaiwa kutenda makosa hayo, tarehe tofauti kati ya Januari Mosi, 2007 na Julai 30, 2009 katika makao makuu ya benki hiyo, mkoani Dar es Salaam.
Alidai katika kipindi hicho, mkoani Dar es Salaam, washitakiwa kwa udanganyifu na bila haki, waliiba kiasi hicho cha fedha.
Mtoro anadaiwa katika kipindi hicho, makao makuu ya NMB, yaliyoko
wilayani Ilala, Dar es Salaam, akiwa mtumishi wa benki hiyo, aliingiza
maingizo yasiyo sahihi katika akaunti maalumu na kuhamisha sh. milioni
579.8 kwenda akaunti binafsi ya Kindamba.
Pia, Mtoro anadaiwa kuhamisha sh. milioni 389 kutoka akaunti ya NMB kweda akaunti ya Cariton Trading Co. Industrial na alihamisha tena sh. milioni 60.5 kwenda akaunti ya Jacques Investment.
Mtoro anadaiwa katika kipindi hicho, alitakatisha fedha kwa kuhamisha sh. 1,029,454,383, kutoka akaunti maalumu ya NMB kwenda akaunti za Kindamba, Cariton na Jacques huku akijua ni kosa.
Katika shitaka lingine, Mtoro anadaiwa kutakatisha fedha haramu kwa kubadilisha fedha kwa kununua nyumba maeneo ya Mbezi.
Mshitakiwa Kindamba anadaiwa kutakatisha fedha sh. milioni 579,887,395, ambazo zilikuwa zimehamishwa kutoka akaunti ya NMB kwa udanganyifu na Mtoro, na kwamba sehemu ya fedha hizo alinunulia nyumba maeneo ya Mabibo.
Kikopa anadaiwa kutakatisha sh. milioni 389 zilizohamishwa kutoka akaunti ya NMB na Mtoro kwenda akaunti ya Cariton, ambayo yeye alikuwa mtiaji saini pekee na alitakatisha tena sh. milioni 60 na sehemu ya fedha hizo ambazo ni sh. 449,566,988 alinunulia nyumba maeneo ya Mbezi Mshikamano.
Washitakiwa wote wanadaiwa katika kipindi hicho waliisababishia NMB hasara ya sh. 1,029,454,383.
Washitakiwa walikana mashitaka ambapo Hilla alidai upelelezi umekamilika na kuomba tarehe ya usikilizwaji wa awali.
Hakimu Hellen aliahirisha shauri hilo hadi Agosti Mosi mwaka huu kwa usikilizwaji wa awali na washitakiwa walirudishwa rumande.
0 comments:
Post a Comment