Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(CHADEMA) Jimbo la Kigoma Kaskazini tunapenda kutoa taarifa kwa umma
kutokana na sintofahamu inayotaka kulazimishwa mbele ya jamii kuhusu
uimara wa chama chetu mkoani Kigoma.
Tangu jana na leo kumeenea
taarifa zinazowahusu watu watatu, Jaffari Kasisiko, Msafiri Wamarwa na
Mama Malunga Masoud, ambao vyombo mbalimbali vya habari vimeandika kuwa
wamehama chama chetu cha CHADEMA na kukimbilia wanakojua wao (maana CCM
inafanya kazi zake katika sura mbalimbali).
Katika hatua ya awali, sisi CHADEMA Jimbo la Kigoma Kaskazini tungependa kusema machache juu suala hilo la watu hao kuhama;
1.
Kwanza watu hao mbali ya kwamba walikuwa ni viongozi wa chama
ngazi ya mkoa, kwa uhakika kabisa walikuwa ni kikwazo kama si kizuizi
cha muda mrefu sana kwa chama chetu kustawi na kuwa imara zaidi katika
mkoa mzima wa Kigoma ili kiweze kukimbizana na wenzetu wa maeneo mengine
nchi nzima. Badala yake walikikumbatia na kukiatamia chama. Wakati
maeneo mengine wenzetu wakiongeza wabunge majimboni, Kigoma chini ya
uongozi wao ikauza majimbo.
2. Tunaweza kusema kuwa viongozi
hawa pamoja na wengine wachache ambao tunajua wako mbioni kuondoka kati
ya leo na kesho, walikuwa ni sawa na KOTI LILILOTUBANA. Kwa muda wao
wote wa uongozi hawakuwahi kufanya kazi yoyote ya kioganazesheni na
kukieneza chama mkoa mzima. Wao walikuwa watu wa mikutano ya hapa na
pale Kigoma mjini pekee au pale ambapo kunakuwa na uongozi wa kitaifa au
wabunge.
3. Kwa muda mrefu saa wamekuwa viongozi
‘waliotubana’ kwa sababu walifanya kazi kwa kuangalia zaidi maslahi yao.
Sasa kuondoka kwao, ni nafuu kwa chama. Pia ni fursa iliyokuja kwa
wakati mwafaka kwa wanachama makamanda waaminifu na watiifu waliofungiwa
milango kwa muda mrefu, kusonga mbele kukijenga chama chetu kwa imani
kubwa ya kuendelea kubeba matumaini ya Watanzania wanyonge.
4.
Upo ushahidi wa wazi katika hili. Kwa muda mrefu sasa viongozi hao
na wengine wenzao waliopangwa kuondoka kwa awamu nyingine, wamekuwa
wakilalamikiwa kufanya kazi ya chama kingine cha siasa kwa maslahi na
maelekezo ya CCM.
5. Katika madai yao ya kuhama chama watu
hao wamesema wamefikia hatua hiyo eti kutokana na chama chetu kuwa cha
kibabe eti kwa sababu tu Zitto Kabwe alivuliwa nafasi Naibu Katibu Mkuu
ndani ya chama!
6. Madai hayo yanashangaza kwa sababu mbali
ya chama kuwa na sababu nzito za kumvua Zitto (na wenzake akina Kitila
Mkumbo na Samson Mwigamba) cheo hicho kutokana na tuhuma za utovu wa
nidhamu, pia tunaamini hakuna mwanaCHADEMA amejiunga na chama hiki kwa
ajili ya cheo. Ndani ya chama chetu tunaamini katika kugawana majukumu
si vyeo.
7. Katika hali ya kushangaza zaidi wanasema eti
Zitto amezuiwa kugombea uenyekiti. Sasa tunajiuliza hiyo nia ya kugombea
ambayo hatujawahi kuisikia ikitangazwa kwa kufuata katiba, kanuni,
maadili, miongozo na itifaki za chama, waliambizana wao wenyewe na mtu
wao? Lakini kwa wanachama wa CHADEMA Mkoa wa Kigoma tunaelewa Jafari
Kasisiko analipa fadhila za misaada binafsi ikiwemo kupelekwa nje ya
nchi.
8. Ninaomba kutoa wito kwa viongozi wenzangu wa
wilaya na majimbo ya Kasulu Mashariki, Muhambwe, Buyungu, Kasulu
Magharibi, Manyovu, Kigoma Kaskazini, Kigoma Kusini na Kigoma Mjini,
tukutane kwa ajili ya kikao cha Baraza la Mashauriano la Mkoa ili sasa
tuchukue hatua zingine za muhimu na haraka za kuhakikisha tunasafisha
chama chetu kwa kuwaondoa vibaraka na wasaliti wote waliosalia.
9.
Pia tunaomba katika hali ya dharura Chama Makao Makuu pia
kiingilie kwa kutumia kifungu cha Katiba 6.1.3, ili kupata chombo cha
kuendelea kuwaunganisha wanachama wakati mkoa ukijiandaa kuchukua hatua
hiyo kupitia Baraza la Mashauriano.
10. Sisi wa CHADEMA Kigoma
Kaskazini tunawataka wale wengine waliosalia katika mkakati huo wa
kuhamisha watu wachache lakini kwa makundi ili eti kujenga taswira ya
CHADEMA kubomoka, wakiwemo viongozi kadhaa wa Kanda wasisubiri. Chama
chetu kitajengwa na watu wenye imani watakaoweka maslahi na matakwa ya
wananchi mbele kwa kuzingatia misingi yetu kama inavyoelezwa katika
Katiba ya Chama, kanuni, maadili na miongozo.
Kwa niaba ya
Wanachadema imara na makamanda watiifu na waaminifu kwa mabadiliko
yanayobeba matumaini na haki za Watanzania wanyonge, naomba kutoa
taarifa hii.
Ally Kisala
Mjumbe wa Baraza la Mashauriano la Mkoa wa Kigoma
0 comments:
Post a Comment