Waziri wa Afya wa Ghana Sherry Ayittey ametoa siku 14
kwa hospitali moja katika mji wa Kumasi kuonyesha miili ya watoto
watano wanaodaiwa kufa baada ya kuzaliwa.
Watu saba wameshitakiwa kwa kuiba na kula njama ya kuiba mtoto kutoka hospitali ya chuo cha Komfo Anokye, mapema mwezi Februari.
Suwaiba Mumuni, ambaye mtoto wake ni
miongoni mwa watoto watano waliopotea, ameiambia BBC kuwa anaamini
mtoto wake yu angali hai.
Hospitali hiyo ya pili kwa ukubwa nchini Ghana, imekana tuhuma hizo.
Bi Mumuni amesema baada ya kujifungua tarehe 5
Februari, aliambiwa kuwa mtoto wake alikuwa amekufa na hivyo
amechukuliwa na wahudumu kupelekwa chumba cha kuhifadhi maiti.
Amesema, ndugu zake walipofika hospitalini hapo kuchukua mwili wa mtoto, hawakuweza kuupata.
Miili ya watoto wengine wanne waliosemekana kuwa wamekufa siku hiyo, nayo pia haijapatikana.
Kutokana na matukio hayo, waziri wa Afya Sherry Ayittey amesema lazima ukweli ujulikane kuhusu tukio hilo.
Bi Ayittey amesema hospitali hiyo ameipa siku 14 za kazi kupata miili ya watoto hao, ili ikazikwe na familia zao.
0 comments:
Post a Comment