Mnamo tarehe 11/03/2014
TAKUKURU Wilaya ya Mvomero iliwafikisha mahakamani Washitakiwa wawili
kwa makosa ya Matumizi Mabaya ya Mamlaka chini ya kifungu na. 31 cha
Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Na. 11 ya mwaka 2007 na
kuisababishia Serikali hasara chini ya Sheria ya Uhujumu Uchumi ya mwaka
1984 (RE: 2002).
Washitakiwa hao ni Bibi. SARAH PHILBERT LINUMA (61) ambaye alikuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya Mvomero na kustaafu mwaka 2013 pamoja na Bibi ANNA ANDULILE MWAKALYELYE
(53) ambaye ni Afisa Utumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero
ambaye pia alikuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Zabuni ya Halmashauri hiyo
katika kipindi cha mwaka 2007-2010.
Ilielezwa
mahakamani kwamba Washitakiwa hao wakiwa waajiriwa wa Halmashauri ya
Wilaya ya Mvomero, kwa nafasi zao kama Mkurugenzi Mtendaji na Mwenyekiti
wa Bodi ya zabuni katika kipindi cha kati ya tarehe 5 mwezi Mei na 28 mwezi Septemba mwaka 2009 walitumia mamlaka yao vibaya kwa kukiuka Sheria ya Manunuzi ya Umma ya mwaka 2004.
Washitakiwa walitenda kosa hilo kwa kumpatia LUCAS CONSTRUCTION COMPANY LIMITED zabuni
ya ujenzi wa jengo la ofisi za Halmashauri ya wilaya ya Mvomero awamu
ya tatu kwa kufanya kazi moja tu ya uwekaji wa paa kwa gharama ya kazi
zote zilizopaswa kufanyika katika zabuni iliyotangazwa ambazo ni; kuweka
paa, kazi za bomba, plasta na umeme ambapo kwa kufanya hivyo
waliisaidia kampuni ya LUCAS CONSTRUCTION COMPANY LIMITED kupata manufaa isiyostahili ya mkataba wa Tsh 365,059,674/= .
Washitakiwa
wote kwa pamoja kwa kitendo chao cha kutumia mamlaka yao vibaya kwa
kukiuka sheria ya manunuzi ya umma kwa kumpatia zabuni LUCAS CONSTRUCTION COMPANY LIMITED
kufanya kazi moja ya kuweka paa pekee kwa gharama ya kazi zote
zilizopaswa kufanywa katika zabuni iliyotangazwa wameisababishia
Serikali hasara ya TZS 83,455,474/= ikiwa ni gharama ya kazi ambazo
hazikufanywa chini ya Sheria ya Uhujumu Uchumi ya mwaka 1984 (CAP 200) (RE: 2002).kifungu cha 10(i) Jedwali la kwanza.
Washitakiwa hao wamefunguliwa Kesi ya Uhujumu Uchumi Namba ECC 4/2014
katika Mahakama ya mkoa wa Morogoro na Kesi hii itakuja tena mahakamani
tarehe 25/3/2014 kwa ajili ya maelezo ya awali (Preliminary Hearing).
Imetolewa na Eufrasia Kayombo,
Mkuu wa TAKUKURU Wilaya ya Mvomero
Machi 11,2014
0 comments:
Post a Comment