WABUNGE na Wawakilishi kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM) wamepongeza hatua ya kiongozi wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo kueleza kuwa kanisa halikutoa msimamo wake juu ya muundo wa serikali unaotakiwa. Pia wameelezea hofu zao kuhusu uwepo wa dalili za baadhi ya vyama vya upinzani, kutaka kuvuruga mchakato wa kupatikana kwa katiba mpya.
Pengo katika mkutano na waandishi wa habari juzi Dar es Salaam, alipinga waraka unaodaiwa kutolewa na Tume ya Haki na Amani ya Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC) kuhusu muundo wa serikali tatu na kusema sio wa Kanisa Katoliki nchini.
Wakizungumza na waandishi wa habari mjini hapa jana, wajumbe hao wakiongozwa na Mbunge wa Ilala, Mussa Azzan Zungu (CCM), walidai kuwa wamefanikiwa kunasa mipango mbalimbali inayoratibiwa na baadhi ya watu ambao hawana nia njema na mchakato wa kupatikana kwa Katiba.
Alisema pamoja na kuandaa mikakati hiyo ambayo tayari mingine imeshaanza kukataliwa, ikiwemo waraka huo unaodaiwa kutolewa na Kanisa Katoliki wa kulazimisha uwepo wa serikali tatu.
“Katiba ni ajenda ya kitaifa lakini hivi sasa kumekuwa na maneno ya kila aina, hata wananchi kuaminishwa mambo yasiyo sahihi.
“Jana (juzi) mmesikia Kadinali Pengo ameukana ule waraka unaodaiwa kutolewa na Kanisa, nasi kama wajumbe kupitia CCM tunapongeza hatua hii, na sasa tumejua kila aina ya mbinu chafu za kukwamisha kupatikana kwa Katiba.
“Tunajua wazi katika kipindi hiki kuna hata baadhi ya nyaraka na vipeperushi, ikiwemo hata ujumbe kupitia baadhi ya mitandao ya jamii, ikiwa na lengo la kuaminisha jamii kuwa CCM ndiyo haitaki Katiba mpya, tunasema si kweli na Watanzania ni lazima wakatae kuburutwa na mawazo ya wanasiasa waliofilisika,” alisema.
Zungu, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Bunge la Jamhuri la Muungano, alisema CCM haitasaliti uamuzi ulioamuliwa na wananchi isipokuwa haitakuwa tayari kuona Muungano ukivunjwa kwa tamaa ya madaraka.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Idara Maalumu katika Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Haji Omar Kheir ambaye ni Mbunge wa Tumbatu, alikemea mipango inayoratibiwa na baadhi ya wanasiasa, ikiwemo kupandikiza chuki ili Muungano uvunjike.
“Tunajua wapo wanasiasa ambao wamekaa kuona bora Muungano uvunjike kwa tamaa ya kutaka madaraka, ili watawale, sisi wawakilishi tutasimama imara kupinga aina yoyote ya udhalimu huu.
“Nampongeza Pengo, kwani kwa imani yangu tutakwenda pamoja katika mchakato huu …zile taarifa za awali zilizodaiwa kuwa za Kanisa, nilikuwa najiuliza ni kweli taasisi kama hii ambayo inaheshimika na mamilioni ya waumini duniani inaweza kutoa tamko kama hili,” alisema Kheir.
Naye Mjumbe wa Bunge hilo ambaye pia ni Mwakilishi wa Chwaka, Issa Haji Ussi, alisema CCM ni chama kinachoongozwa na misingi imara yenye kutetea matakwa ya wananchi.
“Kama mtu anataka kuvuruga amani, kwanza atambue kuwa atashughulikiwa yeye na Katiba mpya itapatikana ambayo italinda na kuimarisha Muungano wetu zaidi kwa miaka 50 ijayo,” alisema Ussi.
Katika tamko la Tume ya Haki na Amani ya Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC) inayoongozwa na Askofu Mkuu wa Tabora, Paulo Ruzoka, iliwekwa bayana kuwa muundo wa serikali mbili haukutatua matatizo ya msingi na badala yake ulilimbikiza kero zilizosababisha Zanzibar kujiundia Katiba yake mwaka 2010 bila kushauriana na Tanzania Bara.
0 comments:
Post a Comment