Chama kipya cha siasa cha Alliance for Change and Transparency
(ACT-Tanzania) kimeanzishwa na kupewa usajili wa muda huku kikitamba
kuwa mbadala wa vyama vyote vilivyopo sasa kwa maelezo kuwa vimekosa
demokrasia ya kweli.
Miongoni mwa viongozi wa muda wa chama hicho ni
Samson Mwigamba aliyetimuliwa uanachama wa Chadema kutokana na
kuhusishwa na waraka uliotaka kumwandaa Zitto Kabwe kuwania uenyekiti wa
chama hicho.
Mwigamba aliyekuwa ,Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Arusha, alitimuliwa pamoja na aliyekuwa Mjumbe wa Kamati Kuu, Dk Kitila Mkumbo, huku uanachama wa Zitto aliyevuliwa nyadhifa zake zote zikiwamo za Naibu Katibu Mkuu na Naibu Kiongozi wa Upinzani Bungeni, ukisubiri kesi aliyofungua mahakamani.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mwigamba
alisema mchakato wa kuandikisha wanachama mikoani kwa ajili ya kuomba
usajili wa kudumu kwa mujibu wa sheria umeshakamilika.
Alisema kimepata wanachama katika mikoa yote ya
Tanzania Bara na Zanzibar. Hata hivyo, alisema kimechagua mikoa 10
ambayo Msajili wa Vyama vya Siasa atakwenda kuhakiki kama sheria
inavyoeleza kabla ya kupewa usajili wa kudumu.
“Kama tutafanikiwa kupata usajili wa kudumu
mapema, tunatarajia kushiriki kwa nguvu zote katika chaguzi zote ndogo
zitakazojitokeza, uchaguzi wa Serikali za Mitaa na Uchaguzi Mkuu
mwakani,” alisema Mwigamba.
Alisema bendera ya chama hicho itakuwa na rangi ya
zambarau inayoashiria haki, heshima na uadilifu na rangi nyeupe
inayonyesha uwazi na usafi.
“Katikati ya bendera inayozungukwa na rangi
zambarau kuna nyota mfano wa chama kinachojitokeza katikati ya vyama
vingi inayokuja kutatua matatizo ya wanyonge yaliyowakabili kwa kipindi
kirefu,” alisema Mwigamba na kuongeza:
“Pembeni mwa bendera hiyo kuna misitari ya rangi
ya dhahabu inayoonyesha rasilimali zetu, rangi nyeusi zinazoashiria sisi
ni Waafirika.”
Alisema hivi sasa hakuna kiingilio katika kujiunga
na chama hicho na kwamba mara baada ya kupatikana kwa katiba, ndipo
suala hilo litakaposhughulikiwa sambamba na kiingilio.
Mwenyekiti wa chama hicho, Kadawi Limbu alisema
ACT - Tanzania kinaamini katika demokrasia jamii na kina shabaha kuu ya
kupigania na kusimamia mabadiliko na uwazi ambayo ni lazima jamii
inufaike nayo.
Alisema ACT-Tanzania kinaongozwa na msingi mitano ambayo ni:
uzalendo, usawa, uadilifu, demokrasia ya kweli, uwazi na uwajibikaji
vitu ambavyo vyama vyote vya siasa nchini vimeshindwa kuvisimamia kwa
vitendo.
“Hakuna chama hata kimoja chenye demokrasia ya
kweli na hii inatokana na vyama kuanzishwa na watu kwa malengo yao.
ACT-Tanzania inakuja kuwafuta machozi wanyonge wote kwani vyama 21
vilivyopo vimeshindwa,” alisema Limbu aliyewahi kuwa Katibu Mkuu wa
Chama cha Alliance For Democratic Change (ADC) na kuongeza:
“Watu wameipora demokrasia, wanyonge wanahangaika
kutafuta usawa katika huduma za jamii kama elimu, afya na nyinginezo.
Sisi hatutakubali, tutahimiza usawa kwa kila kitu.”
Msajili wa Vyama vya Siasa, Francis Mutungi
alithibitisha chama hicho kupata usajili wa muda na kusema kipo katika
hatua za kusaka usajili wa kudumu.
0 comments:
Post a Comment