Saturday, 8 February 2014

SUMAYE ASIFU UPINZANI

Filled under:



Waziri Mkuu mstaafu katika serikali ya awamu ya tatu, Frederick Sumaye, amesema vyama vya upinzani vimefanya kazi kubwa katika kuchagiza kasi ya maendeleo nchini, hivyo havipaswi kupuuzwa.
Sumaye alikuwa akizungumza katika mahojiano yaliyofanywa jana mchana kupitia kituo cha redio Ukweli cha Kanisa Katoliki, Jimbo la Morogoro.

Alisema vyama hivyo (upinzani) vipo kwa mujibu wa sheria inayokidhi demokrasia ya vyama vingi, lengo lake likiwa ni jema.

 “Unapokuwa na chama kimoja chenye sera fulani, lazima uwe na wengine wenye mawazo na msimamo tofauti ili tuwe na kasi zaidi katika maendeleo, hivyo kwa maana ya siasa ya vyama vingi, upinzani ni mzuri,” alisema.

 Sumaye alisema anaamini kwamba upinzani umechangia vizuri katika `uhai’ wa takribani miaka 22 tangu kuanzishwa kwake.

 “Kwa sababu ukiwa na upinzani, chama tawala kinakuwa hakipumui, hakipati muda wa kusinzia na ndivyo tunavyotaka. Upinzani wetu umeshakua na ni lazima nisema kwamba siyo tena wa kupuuzwa,” alisema.

Kwa mujibu wa Sumaye ambaye pia alizungumzia masuala mengine ya kisiasa na kijamii, upinzani umefahamika na kwa maeneo mengine, umefanikiwa kujenga ngome imara.

Hata hivyo, Sumaye alisema zipo dalili na kauli zinazotoka upinzani, vikiwa na mlengo wa kukikomoa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambacho yeye ni mwanachama wake na kusema hali hiyo si sahihi.

 “Kama tunasambaratika ama vipi, nadhani ni uchanga tu wa kisiasa na kama wapinzani baadhi wanasema nchi haitawaliki ama kufanya fujo kama unakomoa chama tawala.. hiyo siyo sahihi,” alisema.

Alisema kama Tanzania ikiingia katika orodha ya mataifa yenye kutawaliwa na vurugu, hakuna raia wake atakayepona, hivyo akasisitiza umuhimu wa amani ya kweli na utulivu wa kweli kuwa moja ya misingi ya vyama vya siasa.

“Wote tuwe wastahamilivu, lengo liwe kumsaidia mwananchi, tushindane kwenye majukwaa lakini tusimharibie mwananchi maisha yake,” aliasa.

UKUAJI WA RUSHWA
Sumaye aliirejea kauli yake ya mara kwa mara kwamba kiwango cha rushwa nchini hivi kimekuwa kwa kasi inayotishia uhai wa  nchi.

 “Kulikuwa na rushwa wakati wa uchaguzi lakini si sana, hata wakati wa Mwalimu Julius Nyerere, wakati wa vikao alituasa …najua wako aliwabeza kuwa hawafai, akasema kunyweni vichai vyao lakini msiwachague,” alisema.

Akisema kutokana na onyo hilo, watu waliomsikiliza hawakuwachagua `waliozodolewa’ na Mwalimu Nyerere.

“Lakini sasa watu wanazungumza waziwazi kiwango cha rushwa wanayopokea na watu wanawachagua. Mwenye kutoa fedha nyingi anaonekana anafaa, lakini ukweli hafai kabisa,” alisema.
 
AMKUMBUKA MKAPA
Sumaye alielezea kumkumbuka aliyekuwa bosi wake, Rais mstaafu wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa, kwa namna alivyofanikiwa kulinda misingi ya CCM ikiwamo kuwafuta matajiri waliotaka kuwania uongozi na uwakilishi kupitia chama hicho.

 “Mkapa alipokuwa Mwenyekiti wa CCM,  wakati wa uchaguzi wa ndani ya chama aliwaacha matajiri wengi sana, tena wengine walipata asilimia tisini na kura zote, akawaambiwa wewe endelea na biashara zako katika chama tuache,” alisema na kumnukuu.

Alisema hatua kama alizochukua Mkapa, zilichangia kupunguza na kudhibiti hongo wakati wa uchaguzi kutokana na, pamoja na mambo mengine, kuhofiwa majina yao kukatwa.
Sumaye alisema hali inapoachwa kutawaliwa na rushwa wakati wa uchaguzi, wahusika wasiokuwa na mapenzi mema kwa CCM wataendelea kutafuta fedha zikiwamo za haramu, ili waweze kuhonga na kuchaguliwa.

0 comments:

Post a Comment