Thursday, 27 February 2014

SLAA:KUMPITISHA CHENGE NI MAJANGA

Filled under:



Wakati  Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge, akitajwa kuwa miongoni mwa wajumbe wa Bunge la Katiba watakaowania uenyekiti wa bunge hilo, Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Willibrod Slaa, amesema mbunge huyo hafai kwa kuwa uadilifu wake una walakini.

Dk. Slaa amewapa angalizo wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba wakiwamo wa kutoka chama chake kwamba watajuta kwa miaka mingi iwapo watamchagua Chenge kuwa Mwenyekiti wa bunge hilo.

Alisema uadilifu wa Chenge unatia shaka kwa kuwa anakabiliwa na tuhuma za kuhusika katika kashfa ya ununuzi wa rada ya kijeshi ambayo serikali iliinunua kwa fedha nyingi kuliko thamani yake kutoka Uingereza wakati akiwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali mapema miaka ya 2000.

“Katiba hii, sisi (Chadema) ndiyo waasisi wake katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 na baada ya hapo ndipo wenzetu (CCM) walipoidandia na kutangaza nia ya kusaka katiba mpya. Yote sawa, lakini nitashangaa sana na wala sitegemei itokee Andrew Chenge akachaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Bunge hilo...Na wabunge wangu

wanafahamu machungu yatakayojitokeza iwapo watamuunga mkono Chenge,” alisema Dk. Slaa wakati akimnadi mgombea ubunge wa Chadema katika Jimbo la Kalenga, Grace Tendega, katika mkutano wa hadhara wa kampeni.

Dk. Slaa alisema licha ya kukabiliwa na tuhuma hizo, Chenge hadi sasa hajasafishwa.

Akizungumza katika mkutano huo uliofanyika katika kijiji cha Igula kata ya Luhota, Dk. Slaa alisisitiza kuwa wajumbe wa Bunge la Katiba hawapaswi kufanya makosa katika uchaguzi huo kama kweli wana nia ya dhati ya kupata katiba mpya itakayokuwa imebeba mawazo ya Watanzania wote na si ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Wakati Dk. Slaa akitoa angalizo hilo, Mjumbe wa Bunge hilo na Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, ametaja sifa za mgombea wa nafasi ya mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba anayepaswa kuungwa mkono kuwa ni yule atakayelinda heshima ya mawazo ya wananchi kuhusu katiba mpya pamoja na hadhi na heshima ya Bunge hilo.

 Profesa Lipumba aliliambia NIPASHE jana kuwa sifa hiyo ya mgombea wa nafasi hiyo ndiyo hasa msimamo wa Umoja wa Katiba ya Wananchi, ambao yeye na chama chake ni wajumbe wake.

 Profesa Lipumba alisema baada ya umoja huo kuundwa, wanachokisubiri hivi sasa ni wajumbe wa Bunge hilo kupitisha Rasimu ya Kanuni za Bunge hilo.
“Sisi tutamuunga mkono (mgombea) yule mwenye uwezo wa kutoa heshima kwa mawazo ya wananchi na hadhi ya Bunge bila kujali anatoka chama gani,” alisema Profesa Lipumba.

MWENYEKITI KUCHAGULIWA JUMAPILI
Katika hatua nyingine, Mwenyekiti wa kudumu wa Bunge Maalum la Katiba, anatarajiwa kupatikana Jumapili wiki hii.

Habari zilizopatikana mjini hapa jana zilieleza kuwa, zoezi la uchukuaji wa fomu za kuomba kuwania nafasi hiyo litafanyika Jumamosi.

Kwa mujibu wa habari hizo leo ambayo awali ilipangwa kwa ajili ya kuwapa wajumbe wa bunge hilo semina kuhusu rasimu ya kanuni za bunge maalum pekee, sasa itatumika pia kwa wajumbe hao sambamba na kujadili rasimu hiyo ya kanuni.

Habari hizo zinasema kuwa semina hiyo itaendelea hadi kesho na kwamba Ijumaa bunge litapitisha azimio la kuipitisha rasimu ya kanuni hizo.

Habari hizo zinasema kuwa baada ya uchaguzi wa Mwenyekiti, litafuatia zoezi la Rais kumuapisha Katibu wa Bunge la Katiba na Naibu Katibu wa Bunge hilo wiki ijayo.Katibu wa Bunge atamwapisha Mwenyekiti, ambaye naye atawaapisha wajumbe.

Hata hivyo, Katibu wa Bunge Maalum la katiba, Dk. Thomas kashillilah, hakupatikana kutoa ufafanuzi.

Katika hatua nyingine, wajumbe wa CCM jana walikuwa na kikao kilichotarajiwa kuanza saa 1:00 jioni pamoja na mambo mengine, kuweka msimamo kuhusiana na mgombea wake wa uenyekiti.

Hadi sasa wanaotajwa kugombea nafasi hiyo mbali na Chenge ni Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta.

0 comments:

Post a Comment