Siku moja kabla ya Bunge la Katiba kujadili rasimu ya kanuni za
kuendesha bunge hilo, mbunge wa Ubungo (Chadema), John Mnyika,
ameainisha udhaifu uliomo kwenye taratibu hizo, akionya kuwa unaweza
kuwapa mafisadi mwanya wa kuhujumu katiba mpya.
Mnyika amesema kanuni zinampa Mwenyekiti wa bunge hilo mamlaka
makubwa na kumfanya aonekane kama 'mungu mtu', jambo linaloweza kutoa
mwanya kwa mafisadi kuchakachua rasimu na kukiuka maoni ya wananchi.
Mbunge huyo alishauri kamati ya muda ya kanuni kuzifanyia
marekebisho, lakini pia akiahidi kuwa atawasilisha hoja za kanuni
zinazotakiwa kurekebishwa.
Akizungumza jana mjini hapa , Mnyika ambaye ni mjumbe wa bunge hilo
alitaja kanuni ya 20, fasili ya pili ya rasimu hiyo kuwa inampa
mwenyekiti mamlaka na madaraka ya kutafsiri kanuni na uamuzi anaotoa
kuhusu utaratibu kuwa ni wa mwisho.
Kadhalika kanuni ya 44 fasili ya tisa inatoa mamlaka ya kutoa
muongozo na uamuzi wake ni wa mwisho, alitaja pia kanuni ya 80 fasili ya
pili kuwa inampa mwenyekiti huyo mamlaka makubwa hata ya kuamua
pendekezo lolote la kamati au mjumbe bungeni linakubalika au la na
uamuzi wake ni wa mwisho.
“Kanuni hizo zikipita na kukawa na mwenyekiti aliyepokea misimamo
ya chama chake na maelekezo kutoka kwa mafisadi wenye malengo ya
kuchakachua rasimu ya katiba kinyume cha maoni ya wananchi, basi njama
zao zitafanikiwa,” alionya Mnyika.
Aliongeza: “Natarajia kamati ya muda ya kanuni itavirekebisha
vifungu hivyo. Iwapo havitaondolewa, najiandaa kuwasilisha hoja za
kufanya mabadiliko ya kanuni zitakapojadiliwa bungeni. Nitaendelea
kuchambua kanuni zote 113 fasili kwa fasili.”
Rasimu ya kanuni za bunge hilo iligawanywa kwa wajumbe Jumatano
wiki hii ili wakaisome na kuanza kuijadili kesho kabla ya kupitishwa.
Mwenyekiti wa muda wa bunge hilo , Pandu Ameir Kificho, aliunda
kamati ya wajumbe 20 waliopewa jukumu la kumshauri na kuandika nukuu
mbalimbali za majadiliano ya wajumbe na kutoa ufafanuzi wa vifungu
mbalimbali.
Baadhi ya wajumbe hao ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali Jaji
Frederick Werema, Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Angella Kairuki,
Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu, Waziri wa Katiba na
Sheria Zanzibar Abubakari Khamis Bakari, Othman Masoud Othman, Mgeni
Hassani Juma, Ussi Jecha Simae, Ismail Jussa Ladhu na Dk. Tulia Akison.
0 comments:
Post a Comment