MKURUGENZI wa Kampuni ya uwakala wa ajira ya Erolink Tanzania Limited ametoroka nchini baada ya serikali kubaini kuwa ameikosesha kodi ya zaidi ya sh bilioni tatu kwa miaka mitatu.
Imedokezwa kuwa mkurugenzi huyo ajulikanaye kwa jina
la Elvis Rogers Kamanyile, aliondoka nchini na familia yake kuhofia
hatua za kisheria ambazo zinaweza kuchukuliwa kwa kosa la kukwepa kodi.
Aidha, chanzo chetu kilidokeza kuwa mkurugenzi huyo aliondoka
nchini kwa madai ya kwenda kutibiwa ingawa madai hayo yanasemekana
kutokuwa na ukweli ndani yake. Habari zilizopatikana zilidokeza kuwa
hivi sasa kampuni hiyo ya Erolink ipo katika mchakato wa kubadili jina
ili kuepuka kesi ya madai ya kukwepa kodi inayokuja mbele yake, huku
baadhi ya viongozi serikalini (majina yanahifadhiwa) wakiwa mstari wa
mbele kufanikisha zoezi hilo.
“Hivi sasa Erolink ipo katika mchakato wa kubadili jina ili
kupoteza ushahidi lakini pia kama hiyo haitoshi zoezi hilo
linasimamiwa na baadhi ya viongozi wazito serikalini, kutokana na baba
wa mkurugenzi huyo aliwahi kuwa mkurugenzi wa moja ya benki kubwa hapa
nchini ili kuhakikisha sakata hilo linazimika kwa sheria kutofuata
mkondo wake,” kilisisitiza chanzo hicho.
Hofu ya mkurugenzi huyo inakuja baada ya agizo la Waziri wa Kazi na
Ajira, Gaudensia Kabaka, alilolitoa wiki mbili zlizopita la kupiga
marufuku utaratibu wa mawakala kuajiri wafanyakazi wanaowatafutia.
Badala yake aliwataka mawakala husika wakiwamo Erolink kuwahamisha
wafanyakazi waliokodishwa kutoka kwao na mawakala wengine kwenda
kampuni husika moja kwa moja na kuwa waajiri halali katika kipindi cha
mwezi mmoja.
Kwa mujibu wa Waziri Kabaka, kuhusiana na uchunguzi uliofanywa kwa
kampuni 13 ulibaini kuwepo kwa ujanja unaotumiwa na mawakala wanane
kutofuata na kuzingatia sheria na taratibu ambapo mwisho wake hukwepa
kodi na kujipatia faida kwa kutotoa haki za msingi kwa wafanyakazi
kama inavyofanywa na Erolink.
Mbali ya hayo, uchunguzi pia ulibaini kutokuwapo kwa tahadhari kwa
wafanyakazi wanaoajiriwa kwa utaratibu huo ikiwemo kukosa haki za
kijamii kama likizo ya uzazi, matibabu na sheria za mifuko ya hifadhi
ya jamii.
Waziri Kabaka alibainisha kuwa uwepo wa kampuni za mawakala
wanaoajiri watu unaleta mfumo wa kibaguzi katika mishahara kwa kazi za
aina moja, kukosa fursa ya kujiendeleza kielimu na mafunzo,
kukosekana kwa uasalama na uhakika wa ajira huku wafanyakazi wakilipwa
mishahara ya kima cha chini kinyume cha sekta wanayofanya kazi.
Hata hivyo kampuni nyingi za uwakala hapa nchini ikiwamo Erolink
zinakiuka sheria ya ajira na uhusiano kazini namba 6/2004 inayomtaka
mwajiri kuchukua hatua stahiki kwa kuhakikisha wafanyakazi bila
kujali jinsia zao wanalipwa mshahara linganifu kwa kazi zenye uzito
na thamani sawa.
Pamoja na katazo hilo limebaini kuwapo kwa wafanyakazi
wa kigeni wanaohusishwa katika utaratibu wa kukodishwa ambao Waziri
Kabaka aliwataka kuhakikisha wanaomba vibali huku akisisitiza kwamba
waajiriwe na kampuni zinazowakodisha.
0 comments:
Post a Comment