Wakati vita ya kupambana na biashara ya dawa za kulevya
ikiendelea nchini, wasafirishaji wa dawa hizo wameanza kutumia fukwe
ndogondogo za bahari nchini kuziingiza kutoka Mashariki ya mbali, gazeti
hili limebaini.
Januari 10, mwaka huu saa 6:30 usiku, mwandishi
wetu alishuhudia mzigo unaoaminika kuwa ni dawa za kulevya, ukishushwa
kutoka kwenye boti, eneo la Salender Bridge, nyuma ya Kituo cha Polisi
kilichopo eneo hilo.
Baada ya boti hiyo kutia nanga, walishuka watu
zaidi ya 10; Wazungu wawili, Waafrika kadhaa na mmoja mwenye asili ya
Asia na kuungana na wengine wanne ambao tayari walikuwa katika eneo hilo
wakiwa ndani ya magari mawili.
Mara moja walianza kupakua mizigo iliyokuwa
imefungwa kwenye maboksi na kupakia kwenye magari ambayo yalikuwa
yameegeshwa mbali kidogo na ufukwe huo. Kazi hiyo ilichukua muda
usiozidi nusu saa na baada ya mizigo kupakiwa, magari hayo moja likiwa
ni Land Cruiser liliondoka na kuelekea upande wa Morroco na jingine aina
ya Nissan liliondoka kwenda uelekeo wa Posta Mpya.
Wakati magari hayo yakiondoka kwa mwendokasi, boti
iliyokuwa na mzigo huo nayo iling’oa nanga na kuelekea katikati ya
Bahari ya Hindi.
Chanzo chetu kilisema mzigo ulioshushwa ni dawa za kulevya na kwamba boti hizo ndogo hufika eneo hilo hata mara mbili kwa wiki.
Uchunguzi zaidi ulibaini kuwa dawa hizo huingizwa
nchini kwa meli kubwa za mizigo, hasa zile zinazotoka Iran, Pakistan na
Afganistan.
Ukamataji polisi
Mwandishi wetu aliwasiliana na polisi kuhusu njia hiyo ya kuingiza dawa za kulevya nchini na jeshi hilo kuahidi kutoa majibu baada ya kufanya ufuatiliaji. Kabla ya kutoa majibu juu ya ufuatiliaji huo, polisi ilikamata meli kutoka Iran ikiwa na kilo 201 za heroini katikati ya Bahari ya Hindi.
Msemaji wa Polisi, Advera Senso alisema kama
taarifa hizo zingeripotiwa katika vyombo vya habari, ingekuwa vigumu kwa
jeshi hilo kufanikisha kukamatwa kwa wahusika.
Katika wiki moja iliyopita, kilo 846 za dawa za
kulevya zenye thamani ya Sh38 bilioni zimekamatwa kwenye mipaka ya
Tanzania iliyoko katika eneo la Bahari Kuu, kiwango ambacho ni kikubwa
katika rekodi ya kukamatwa kwa dawa za hizo.
Dawa hizo zilikamatwa kati ya Februari 2 na 5
mwaka huu. Kilo 350 za heroini zilikamatwa Februari 5 na wadhibiti wa
dawa za kulevya wa Australia na kilo 265 za heroini zilikamatwa na
wadhibiti wa kimataifa wa Canada, zote zikiwa zinaelekea Tanzania.
Fukwe nyingine
Dawa nyingine ni kilo 201 za heroini zilizokamatwa ndani ya
mpaka wa Tanzania na Kikosi cha Polisi cha Wanamaji na kilo 30
zilizokamatwa Zanzibar.
Kamishna Msaidizi wa Tume ya Kuratibu Dawa za
Kulevya, Aida Tesha alisema, kiasi hicho kikubwa kilikamatwa na
wadhibiti wa bahari wa kimataifa walioshirikiana na wadhibiti wa
Tanzania.
“Huu msimu ni wa wasafirishaji wa dawa za kulevya
kwa njia ya maji. Ni wakati ambao wasafirishaji huleta dawa kwa wingi
kwa sababu ya hali ya hewa. Ieleweke kuwa zinazokamatwa ni asilimia 10,
tu. Wapo wengi ambao wanapita bila kubainika,” alisema Tesha.
Tesha alisema wadhibiti wa kimataifa wanapokamata
dawa huziharibu majini ili kuwapa hasara wauzaji hao kwani wanapowaacha
au kuzikabidhi kwa nchi zilizo mipakani, zinaweza kuwafikia watumiaji.
Mkuu wa Interpol, Tawi la Tanzania, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP),
Gustav Babile alisema hana taarifa za kina za kukamatwa kwa kiasi hicho
cha dawa za kulevya isipokuwa wenzake wamemtumia taarifa hizo akiwa
Algeria.
Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI),
Isaya Mngulu alisema: “Nina taarifa za Kilo 201 za heroini, ambazo
watuhumiwa wake 12 Raia wa Iran na Pakistan tayari wameshafikishwa
mahakamani na kusomewa mashtaka yao”.
DCI Mngulu alisema polisi wanaendelea na doria
kwenye maeneo ya bahari kwa kutumia mbinu zote ili kuhakikisha tatizo
hilo linapungua.
Kwa upande wake, Kamishna wa Kikosi cha Polisi cha
Kupambana na Dawa za Kulevya, Godfrey Nzowa alisema: “Ni kweli hicho ni
kiasi kikubwa kukamatwa kwenye mipaka ya Tanzania na kinaonyesha kuwa
watu hawa wanadharau mipaka yetu, pia kunaonyesha kuwa tunafanya misako
mikali.”
Fukwe nyingine
Uchunguzi ulibaini kuwa fukwe nyingine ndogo za
Dar es Salaam zinatumika kushusha dawa za kulevya bila kugundulika kwa
urahisi na kukwepa nguvu nyingi za udhibiti ambazo zilikuwa zimewekwa
katika viwanja vya ndege na mipaka ya barabara.
Miongoni mwa fukwe hizo ni Mbezi Jogoo, Dar es
Salaam na eneo maarufu la Loliondo ya Kigamboni ambako pia kunadaiwa
kuwa na vitendo vya kutisha vya ukahaba, biashara ya pombe haramu ya
gongo na bangi.
Uchunguzi umebaini pia kuwa katika eneo la
Loliondo, wavuvi hutumika kubeba dawa hizo kwa kutumia boti kutoka
kwenye meli kubwa na kufikisha mizigo husika nchi kavu ambako hupokewa
na watu maalumu na kuanza usambazaji.
Katika Pwani ya Bagamoyo, kiasi kikubwa cha dawa
za kulevya hupitishwa na mara nyingi huwa zimefungashwa kama makopo ya
samaki waliosindikwa.
Mkoani Mtwara, wasafirishaji hutumia fukwe ndogondogo kama za
Mikindani kuingiza dawa hizo ambazo baadaye husafirishwa kupelekwa
Msumbiji.
Katika Mkoa wa Lindi, maeneo ya Songo Mnara, Kilwa
nayo yanatajwa kwamba yanatumika kuingiza dawa za kulevya kutoka Dar es
Salaam na Zanzibar.
Uchunguzi wetu umebaini baadhi ya mbinu za
kusambaza dawa hizo mitaani. Mizigo hufungwa kwenye khanga au matenga
ili isitiliwe shaka na kisha kupelekwa mitaani kwa miguu na watu kati
(middlemen) ambao hulipwa ujira kwa kazi hiyo.
Katika siku ambazo kuna wasiwasi au hofu ya kukamatwa, mizigo hufukiwa ardhini hadi hali inapotulia.
Kamanda wa Kikosi cha Wanamaji, ACP Mboje Kanga
alisema kwa Tanzania ni kazi ngumu kusimamia fukwe na uharamia
unaofanyika, kwani ina fukwe zenye urefu wa kilometa 1,424.
Ripoti ya 2013 ya Kitengo cha Uhalifu na Dawa za
Kulevya cha Umoja wa Mataifa (UNODC), inataja Bahari Kuu kuwa njia kuu
zinazotumika kusafirisha dawa za kulevya hadi Tanzania hasa Tanga na
Zanzibar, kisha kusafirishwa kwa boti ndogo kwenda Dar es Salaam na
baadaye nchi za Kusini mwa Afrika.
Kadhalika, taarifa ya 2011 ya kitengo cha dawa za
kulevya iliyochapishwa katika Ripoti ya Kitengo cha Dawa za Kulevya cha
Marekani inaeleza kuwa, heroini huingia Tanzania kupitia Bahari ya Hindi
ikitokea Afghanistan, Iran na Pakistan kupitia Dubai.
0 comments:
Post a Comment