MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA),
Freeman Mbowe, amemvaa Rais Jakaya Kikwete, akimtaka kuacha kutafuta huruma ya
Watanzania juu ya suala la Katiba na badala yake atumie nafasi hiyo kuwataka
wabunge wake kuheshimu maoni ya wananchi. Mbowe ambaye pia ni Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni,
alisema kuwa hotuba ya Rais Kikwete juzi kwamba Katiba haiwezi kupatikana kwa
ngumi imejaa upotoshaji kwa wananchi. Katika hotuba yake ya maadhimisho ya miaka 37 ya kuzaliwa kwa
CCM, yaliyofanyika mkoani Mbeya, Rais Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM,
alimshangaa Mbowe kwa kauli yake kwamba mfumo wa serikali tatu ukikataliwa
katika Bunge hilo nchi haitatawalika.
“Huku ni kuwadanganya wananchi, pale hakuna ngumi wala vurugu
yoyote, kila ibara iliyopo katika rasimu itajadiliwa ili upatikane mwafaka.
Huku ni kukosa ukomavu wa kisiasa,” alisema. Akizungumza na Tanzania Daima jana, Mbowe alisema ni vema Rais
Kikwete akaacha kuhangaika na wapinzani, badala yake awe tayari kuheshimu
mawazo ya wananchi waliyotoa wakati wa kutoa maoni ya Katiba. Mbowe alisema kuwa Rais Kikwete ni mwanasiasa na mtu anayejaribu
kupotosha hoja, kwani CHADEMA waliposema watapambana, hawakumaanisha kupigana
ngumi kama alivyosema kiongozi huyo. Alisema kuwa viongozi wa CCM wamekuwa wakilazimisha ajenda ya
Katiba mpya kuonekana kama sera yao, jambo ambalo CHADEMA haiwezi kuafiki.
“Katiba ni ya wananchi, si ya chama chochote cha siasa, ndiyo
maana hatukubali kuona mawazo ya wananchi yakishindwa kuheshimiwa,” alisema. Mwenyekiti huyo alisema Tume ya Mabadiliko ya Katiba
inayoongozwa na Jaji Joseph Warioba imefanya kazi nzuri ambapo Rais Kikwete na
wabunge wake wanapaswa kuheshimu mchango huo. Alisema kuwa CHADEMA itahakikisha inashindana kwa hoja katika
Bunge la Katiba litakaloketi hivi karibuni na iwapo hilo litashindikana
watarudi kwa wananchi ambao ndio wenye uamuzi wa mwisho juu ya suala hilo. “Wajumbe watakaoshiriki Bunge la Katiba ni 640 ambao hao si
waamuzi wa mwisho na kama tutaona kuna suala lolote linaloenda kinyume, sisi
tutakachokifanya ni kurudi kwa wananchi kuwaeleza juu ya kilichotokea na hao
ndio wenye maamuzi ya mwisho katika kura ya maoni,” alisema.
Mbowe alisema kuwa hata katika kushindana kwa hoja CCM wanapaswa
wasiweke hila, maana wataweza kuchangia mchakato huo kushindwa kufanikiwa. Alisema kuwa nia ya CHADEMA ni kuhakikisha Katiba nzuri, bora na
iliyo ya wananchi inapatikana na si kusababisha vurugu kama ambavyo Rais
Kikwete amejaribu kupotosha. “Hila hiyo imeonekana wazi maana kuna hali ya kutaka kupuuza
mawazo ya wananchi na CCM kulazimisha mawazo yao, hilo hatutalikubali na
tutapambana…hiyo si mara ya kwanza kupambana katika suala hilo,” alisema. Mbowe alisema kuwa kuhusu serikali tatu ni muhimu Rais Kikwete
akaheshimu mawazo hayo na CHADEMA itashindana kwa hoja juu ya suala hilo ili
kuhakikisha mawazo hayo yaliyowasilishwa na Jaji Warioba yanaheshimiwa.
Katika ziara ya mikutano ya hadhara ya CHADEMA iliyopewa jina la
Operesheni M4C Pamoja Daima, Mbowe na viongozi wengine waliionya Serikali ya
CCM kutochakachua mchakato wa Katiba, kwani Watanzania hawako tayari kurudi
kwenye Katiba ya sasa ambayo alidai imekosa uhalali wa kuongoza nchi. Alisema CCM kwa kutumia wabunge wake wakiamua kuhujumu mchakato
huo bungeni, yeye na viongozi wenzake watapita nchi nzima kuwataka wananchi
wasishiriki kura za maoni na yuko tayari kufunguliwa kesi kwa kudai Katiba
mpya.
0 comments:
Post a Comment