Kesi ya aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na
Maendeleo (Chadema), Zitto Kabwe dhidi ya chama chake hicho inatarajiwa
kuanza kutajwa leo katika Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam.
Zitto ambaye pia ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini
alifungua kesi hiyo dhidi ya Bodi ya Wadhamini wa Chadema na Katibu Mkuu
wa Chadema, akiiomba mahakama hiyo ikizuie chama kujadili uanachama
wake, hadi rufaa anayokusudia kuikata Baraza Kuu la chama kupinga
kuvuliwa nyadhifa, itakaposikilizwa.
Katika kesi hiyo namba 1 ya 2014, Zitto pia
aliiomba mahakama hiyo imwamuru Katibu Mkuu wa Chadema ampatie mwenendo
na taarifa za Kikao cha Kamati Kuu ya Chadema kilichomvua nyadhifa zote
alizokuwa nazo ndani ya chama na iwazuie walalamikiwa kumwingilia katika
utekelezaji wa majukumu yake kama Mbunge wa Kigoma Kaskazini.
Kesi hiyo ambayo inasikilizwa na Jaji John Utamwa
imepangwa kuanza kutajwa leo kabla ya kupangiwa tarehe ya kuanza
kusikilizwa rasmi.
Tayari mahakama imeshatoa amri ya zuio la muda kwa Chadema kumjadili na au kuchukua uamuzi wowote kuhusu uanachama wake.
Uamuzi huo ulitolewa Januari 7 na Jaji Utamwa, kutokana na maombi ya Zitto, kupitia kwa Wakili wake Albert Msando.
Awali mawakili wa Chadema, Mwanasheria Mkuu wa
chama hicho, Tundu Lissu na Mkurugenzi wake wa Katiba, Sheria na Haki za
Binadamu, Peter Kibatala walipinga maombi hayo wakidai kuwa hayajakidhi
matakwa ya kupewa zuio la muda.
Katika uamuzi wake, Jaji Utamwa alikubaliana na
hoja za Wakili Msando kuwa maombi hayo yametimiza matakwa yote ya kupewa
zuio hilo.
0 comments:
Post a Comment