Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) umemuonya Mwenyekiti
wa CUF Taifa Profesa Ibrahimu Lipumba kuacha kuingilia maamuzi ya
kikatiba yanayofikiwa na CCM na kumtaka ashughulikie maendeleo ya chama
chake.
Hayo yalisemwa juzi na Naibu Katibu Mkuu wa UVCCM Zanzibar Shaka
Hamdu Shaka wakati akimnadi mgombea wa nafasi ya uwakilishi jimbo la
Kiembesamaki Mahmoud Thabit Kombo huko Buyu Kisiwani Unguja juzi.
Shaka alisema kuwa Profesa Lipumba hatakiwi kuingilia maamuzi yao
na kwamba kama ameshindwa kushughulikia maendeleo ya chama chake aache
siasa ama arudie kazi yake ya kushika chaki.
Shaka alikipuuza kitendo cha Profesa Lipumba kusema CCM kama kina
ubavu kiwafukuze wanachama wake watatu wanaotetea mfumo wa serikali tatu
akiwamo Waziri Mkuu mstaafu Dk. Salim Ahmded Salim, Joseph Warioba na
mwanasiasa mkongwe Joseph Butiku.
“Profesa Lipumba hana haki ya kukisemea CCM na badala yake inampasa
kuangalia kudorora kwa chama chake huku yeye na Katibu wake wakiendelea
kuwa viongozi wa kudumu wa chama hicho kinyume na misingi ya demokrasia
ya kweli,” alisema Shaka.
Shaka alisema Profesa Lipumba wakati akizindua kampeni ya chama
chake alikosa ajenda na neno la kuwaeleza wananchi wa Kiembesamaki
badala yake akaamua kuhoji mfumo wa utawala na uendeshaji wa kitaasisi
na kikatiba.
“Profesa Lipumba kama siasa imekushinda, pumzika, rudi ukashike
chaki na kufundisha wanafunzi, mambo ya ngoswe waachie ngoswe wenyewe,
usiipangie CCM la kufanya na kuamua, shughulikia udhaifu na mazonge
ndani ya CUF, CCM mfupa mgumu uliowashinda wengi”Alisema Shaka.
Alisema CCM ni taasisis inayoongozwa na kuheshimu katiba yake,
maadili , kanuni na nidhamu yake na kwamba haifukuzi wanachama au
mwanachama wake kiholela , kulazimishwa na mtu au shuruti ya kundi
lolote.
Akitoa mfano alisema hata mwaka 1988 CCM kwa kutambua dhamana
,kuelewa mantiki ya demokrasia na kuheshimu katiba yake, ilimfukuza
Maalim Seif Shari Hamad na wenzake sita ili kulinda heshima yake mbele
ya jamii na kimataifa bila ya kutetereka na kuyumba hadi leo.
“CUF mlimfukuza James Mapalala, Naila Jidawi, Salum Msabaha, Hamad
Rashid, Michael Nyaruba na wengine, CCM haikuingilia uhuru wa maamuzi
yenu, vipi Lipumba uweweseke unapoona CCM ikitimiza wajibu wake wa
kikatiba na kimaadili” alihoji Shaka.
0 comments:
Post a Comment