Wednesday, 29 January 2014

USHAWISHI WA LOWASA NDANI YA CCM,YATESA UVCCM

Filled under:



Ushawishi wa Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), umeipasua Jumuiya ya Vijana ya chama hicho (UVCCM).

Mmoja wa viongozi  wake ametoa taarifa iliyojaa maneno makali akimshambulia Lowassa na baadhi ya viongozi wa dini akiwahusisha na kampeni za uchaguzi wa urais mwakani.

Bila kutaja jina la kiongozi yeyote wa dini, ila tu kurejea kwa ujumla wao kama maaskofu na masheikh, Katibu wa Uhamasishaji na Chipukizi wa UVCCM, Paul Makonda, aliwataka kwenda kwa Lowassa kama wanataka fedha za haraka. Hakusema ni fedha za nini.

Akizungumza katika mkutano wa waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Makonda alisema  hawawezi kukaa kimya wakati viongozi wa CCM wakishambuliwa na watu aliosema hawana mapenzi mema na chama chao.

Alisema wapo watu aliodai wanafadhiliwa na Lowassa ili kuwashambuliwa viongozi wa sekretariati ya CCM, Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana na Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, kwa kuwa anautaka urais mwakani.

Aliwataja makada wa CCM aliodai wanaosukumwa na Lowassa kuwa ni Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Singida, Mgana Msindai na Mwenyekiti mstaafu wa CCM Dar es Salaam, John Guninita.

Makonda aliwatuhumu makada hao kuwa ni wahaini, waongo na wazandiki, na kueleza kuwa kama nia yao ni kusaka urais kwa ajili ya Lowassa, basi wajue kuwa amekosa sifa za kuteuliwa na chama hicho kuwania wadhifa huo katika uchaguzi mkuu wa mwakani.

Hata hivyo, muda mfupi tu baada ya kauli ya Makonda, Makamu  Mwenyekiti wa UVCCM, Mboni Mhita, alisema kauli hiyo siyo msimamo wa UVCCM.

Msindai alikaririwa hivi karibuni akielezea msimamo wa kumuunga mkono Lowassa katika masuala ya maendeleo, wakati Guninita alimkosoa Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, kutokana na kauli zake za kuwaita baadhi ya mawazi ‘mizigo’ kwa kuwa wameshindwa kutekeleza ilani ya CCM ya mwaka 2010-2015.

Pia alimlaumu Nape kwa kukosoa uteuzi mpya wa baraza la mawaziri uliofanywa na Rais Jakaya Kikwete Januari 19, mwaka huu.

Guninita alimkosoa Nape akisema kuhoji uteuzi huo ni sawa na kuingilia mamlaka ya Rais katika kutimiza wajibu wake kwa kikatiba.

Katika mkutano na waandishi wa habari jana Makonda alisema: “Tutaendelea kuwajibu akina Msindai (Mgana) ama Guninita (John), lakini kuna mtu anayewatuma kutoa kauli hizo, na huyu ni Edward Lowassa.”

NIPASHE iliwasiliana na Lowassa kwa njia ya simu jana, lakini ikapokewa na mtu aliyeagiza suala hilo aulizwe mmoja wa wasaidizi wake wa masuala ya vyombo vya habari.

Msaidizi huyo ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini, alisema Lowassa hawezi kuzungumzia madai ya Makonda.

Makonda alisema UVCCM imemuandikia barua Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Philip Mangula, kuhusu vitendo vya Lowassa kuwatumia viongozi na makada wa chama hicho kutoa kauli zenye mwelekeo wa kumchonganisha Rais Kikwete na sekretarieti ya chama hicho.

Alisema barua hiyo (hakuionyesha) ililenga kumuomba Mangula, asaidie ili kanuni za chama hicho zitumike kumdhibiti Lowassa. 

NIPASHE ilimtafuta Mwenyekiti wa UVCCM,  Sadifa Hamisi Juma, kuzungumzia kauli ya Makonda kama ndiyo msimamo wa jumuiya hiyo, lakini simu yake haikujibiwa wala ujumbe mfupi wa maneno (sms) hadi tunakwenda mitamboni jana

Akifafanua kauli hiyo Mhita alisema ni ya Makonda kama mkuu wa kitengo cha uhamasishaji.

“Kama utafika wakati ikahitajika kuzungumzia jambo lolote la kitaifa, basi mzungumzaji mkuu ni Mwenyekiti wa UVCCM au Makamu Mwenyekiti,” alisema Mhita pasipo kufafanua zaidi.

NIPASHE ilipowasiliana na Msindai na Mangula, simu zao ziliita bila kupokelewa wakati ile ya Guninita haikupatikana.

Awali, Makonda alisema ziara ya Kinana na Nape (iliyowaibua mawaziri mizigo) ilikuwa sehemu ya utekelezaji wa kanuni, misingi na katiba ya CCM, vinavyotoa jukumu kwa chama hicho kuwa kiungo kati ya serikali na wananchi.

Alisema CCM ni chama kinachoiunganisha serikali na wananchi, na kwamba ziara ya Kinana iliyokuwa na wajumbe kadhaa akiwamo Nape, ilifanikisha kuibua kero kadhaa zilizopo kwenye jamii.

Makonda alisema kupitia ziara hiyo, ujumbe wa Kinana ulibaini kuwapo kero zilizowasilishwa serikalini kwa nia ya kupatiwa ufumbuzi, hivyo inashangaza kuibuka kwa baadhi ya wana-CCM wanaoikejeli.

Kwa mujibu wa Makonda, ziara kama iliyofanywa na Kinana, haijawahi kufanywa na kiongozi yeyote wa ngazi hiyo kwa miaka ya karibuni, na kusema wanaoipinga hawana nia njema na wananchi wanaokabiliwa na kero mbalimbali za kijamii.

“Chama hiki ni cha wanyonge, maskini wa taifa hili, haiwezekani matajiri watake kukihodhi na waratibu mikakati ya kukihujumu kwa fedha, hali sisi vijana tukitazama, tunasema tutakilinda na tutawalinda viongozi wetu waadilifu,” alisema.

 Makonda alisema viongozi wanaobezwa (Kinana na Nape) wamechangia kurudisha imani ya wananchi kwa CCM, akitoa mfano wa kukutana na `kuzichukua’ kero za wafugaji, walimu, wakulima wa pamba, korosho na wananchi wa kawaida.

UVCCM RORYA YAMVAA MAKONDA
Katika hatua nyingine, Mwenyekiti wa UVCCM Wilaya ya Rorya, Sango Kasera, amemtaka Katibu Mkuu wa Umoja huo, Sixtus Mapunda, kueleza kama tamko lililtolewa na Makonda ni la kamati ya utekelezaji au ni lake binafsi.

 Pamoja na kumtaka Mapunda kueleza hilo, pia amemtaka Makonda kufanya kazi za kufufua chipukizi na kueleza kazi walizofanya kama UVCCM hadi sasa, kwani tangu ateuliwe amekuwa akiishia tu kutoa matamko, ambayo hayana tija kwa vijana wa Kitanzania.
 

0 comments:

Post a Comment