MBUNGE wa Moshi Mjini, Philemon Ndesamburo (CHADEMA), amesema
matatizo yanayokikumba chama hicho kwa sasa yanatokana na kundi la watu
wachache wenye uchu wa madaraka, ambao pia wanatumiwa na Chama Cha
Mapinduzi (CCM).
Ndesamburo alisema kuwa wanaosababisha hali hiyo ni vijana ambao
hawana uchungu na CHADEMA, na hivyo kushauri uongozi uchukue hatua
stahiki ya kinidhamu kwa watu hao.
Mbunge huyo ambaye pia ni Mwenyekiti wa CHADEMA Mkoa wa Kilimanjaro,
alikuwa akijibu maswali ya wananchi kwenye mikutano yake ambapo walitaka
kujua nini hatima ya mzozo unaoendelea kwenye chama hicho.
Alisema kuwa kiongozi yeyote wa CHADEMA ambaye anakubali kuhongwa na
kusaliti chama ni msaliti mkubwa na anahujumu maisha ya Watanzania
milioni 45 ambao wanakitegemea chama.
Ndesamburo alisisitiza kuwa uongozi wa chama lazime ufanye uamuzi
mgumu kwa wanachama na viongozi wengine ambao hawatakuwa na nidhamu
ndani ya chama, kwamba bila kufanya hivyo watajiamulia watakalo.
“CHADEMA lazima iwe tofauti na vyama vingine, kwanza kwa
kuwawajibisha wale wote ambao hawatakuwa na nidhamu ndani ya chama ili
kuwepo tofauti, na kwa sasabu ni chama cha upinzani, hatuwezi kuwa kama
CCM ambao wanakumbatia mafisadi,” alisema.
Ndesamburo aliongeza kuwa CHADEMA kwa sasa ni sawa na mti wenye
matunda, hivyo CCM haiwezi kuacha kuupiga mawe ila akaonya kuwa wao
wataendelea kupigana na kuhakikisha chama kinafanya vizuri.
Kuhusu uchaguzi wa serikali za mitaa, alisema chama hicho kimejipanga
kuimarisha msingi wake kuanzia ngazi ya mabalozi, matawi mikoa hadi
taifa.
0 comments:
Post a Comment