Mara baada ya kuundwa kwa Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya CCM
Taifa inayoongozwa na Katibu Mkuu Ndg. Abdulrahman Kinana mwanzoni mwaka
mwaka jana, Sekretarieti hiyo imejiwekea utaratibu wa kufanya ziara
mikoani kukutana na wananchi kusikiliza kero zao, kukagua utekelezaji wa
Ilani ya Uchaguzi ya CCM na kuimarisha Chama mikoani.
Utaratibu huu ni agizo la mkutano mkuu wa Taifa wa nane wa CCM uliofanyika Novemba 2012 mjini Dodoma. Nanukuu azimio hilo;
“Chama Cha Mapinduzi lazima kiwe karibu na wananchi, kisikilize changamoto zao na kiwasemee wananchi na hasa wanyonge” Moja ya maazimio ya Mkutano Mkuu wa nane wa CCM 2012.
Kwa hiyo msingi wa kwanza wa ziara hizo ni maagizo ya Mkutano Mkuu wa
CCM Taifa ambacho ndicho kikao cha juu kabisa cha Chama. Msingi wa pili
ni ukweli kuwa CCM ndio iliyopewa dhamana na kuingia mkataba na
wananchi kupitia ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2010/2015, hivyo
inayowajibu wa kukagua utekelezaji wa ilani hiyo.
Na bila shaka wote tumeshuhudia jinsi ziara hizo zilivyoinua uhai wa
Chama nchi nzima na kuongeza kasi ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi na
kutatua kero mbalimbali za wananchi kwenye maeneo yao, kiasi cha
kuongeza imani ya wananchi kwa CCM.
Tumeshuhudia makundi mbalimbali ndani ya jamii yakija kueleza
changamoto zao ndani ya Chama. Makundi hayo ni pamoja na makundi ya
wakulima, wafugaji, wafanyabiashara, wanafunzi na wafanyakazi hasa
walimu. Huu ni uthibitisho wa kuongezeka kwa imani yao kwa CCM.
Katika mwendelezo wa ziara hizo mwishoni mwa mwaka jana Katibu Mkuu
wa CCM na baadhi ya wajumbe wa Sekretarieti walifanya ziara ya siku 26
katika mikoa ya Ruvuma, Mbeya na Njombe. Pamoja na mambo mengine
wananchi walilalamikia baadhi ya watendaji wa serikali hasa baadhi ya
mawaziri wakiamini kuwa yapo mapungufu kadhaa yanayotokea kwenye wizara
zao.
CCM kama lilivyo agizo la Mkutano mkuu la kuwasemea wananchi
tulisikiliza kilio chao na kwa kufuata utaratibu, baadhi ya mawaziri hao
waliitwa na kuhojiwa kwenye Kamati Kuu ya CCM mwezi Disemba 2013.
Utaratibu wa watendaji wa serikali kutoa taarifa za utekelezaji wa
Ilani ya Uchaguzi ya CCM kwenye vikao vya Chama sio mgeni na wala
haujaanza jana. Wakuu wa wilaya hutoa kwenye wilaya, wakuu wa mikoa
hutoa mikoani kwao, hivyo sio utaratibu mpya.
Baada ya mahojiano hayo Kamati Kuu ya CCM ilitoa ushauri kwa serikali
wa namna ya kurekebisha mapungufu yaliyoelezwa na wananchi. Kwakuwa kwa
mujibu wa Katiba ya Nchi mwenye mamlaka na mawaziri ni Rais mwenyewe,
CCM ililiacha suala hili kwake aangalie njia ipi bora ya kuondoa
mapungufu tuliyoyaeleza.
Na kwenye taarifa yetu kwa vyombo vya habari baada ya kikao hicho
tulisisitiza kuwa sio lazima awafukuze mawaziri husika isipokuwa
wanaweza kufanya mabadiliko katika mfumo,sheria nk ili mradi kuwepo na
mabadiliko katika kushughulikia mambo yaliyolalamikiwa na wananchi.
Hivi karibuni Rais amefanya mabadiliko kidogo kwenye baraza lake la
mawaziri na kuwarudisha baadhi ya mawaziri waliolalamikiwa na wananchi
na wabunge, ambao malalamiko hayo yaliungwa mkono na CCM. Ni kupitia
malalamiko hayo ndipo lilipozaliwa jina la mawaziri mizigo. Baada ya
uteuzi huo kukaibuka mjadala mkubwa nchini wakihoji kulikoni Rais kaamua
kutowatimua mawaziri hao.
Kwanza haikuwa hoja ya CCM kuwafukuza mawaziri hao bali kuchukua
hatua za kurekebisha mapungufu husika. Kufukuza inaweza kuwa ni njia ya
kutatua tatizo lakini sio njia pekee. Hivyo basi CCM tunaamini kuwa
kurudishwa kwao wamepewa fursa ya kurekebisha mapungufu tuliyoyasema kwa
niaba ya wananchi. Tunaamini mawaziri wote hawatabweteka bali
watatimiza wajibu wao na kuhakikisha wanawatumikia wananchi ambao ndio
waajiri wa serikali.
Ifahamike kuwa Chama Cha Mapinduzi hakitasita kuchukua hatua kali
dhidi ya mawaziri na watendaji wengine watakaoshindwa kurekebisha
mapungufu na watakaoshindwa kutimiza wajibu wao vizuri. Wakumbuke
kushindwa kwao kutimiza majukumu yao ni hujuma kwa Ilani ya uchaguzi ya
CCM, CCM haitavumilia usaliti huo. Kukaa kimya kwa CCM itakua ni
kujinyonga yenyewe jambo ambalo hatutaruhusu kabisa.
Tunajua wapo baadhi ya watendaji wa serikali wasiopenda kuhojiwa
utendaji wao, tunawasihi kwa moyo safi wasiotaka kuulizwa juu ya
utendaji wao waondoke serikalini wenyewe kwani CCM tutakuwa wakali sana
kwenye mapungufu,kwani tukikaa kimya tutakua tunajihujumu wenyewe.
Tutatumia vizuri wingi wa wabunge wetu bungeni na wingi wa madiwani
wetu kwenye halmashauri kuisimamia vizuri serikali. Hivyo kuanzia sasa
kasi ya CCM kuisimamia serikali, kuisifu itakapofanya vizuri na kukosoa
itakapofanya vibaya itaongezeka mara dufu kwa kila ngazi.
Tunawaomba watanzania kwa ujumla tuwape muda wateule hawa wa Rais
watimize wajibu wao, lakini tusisite kusema pale tutakapoona mambo
hayaendi kama tunavyotarajia. Uwajibikaji wa kweli ndio msingi wa
mafanikio na maendeleo yetu.
CCM inawatakia kila lakheri kwenye kutimiza wajibu wao. Tuna
matumaini makubwa kuwa wote kwa pamoja hawataisaliti ilani ya Uchaguzi
ya CCM na kwamba hawatayaangusha matumaini ya wananchi kwa serikali yao.
KIDUMU CHAMA CHA MAPINDUZI!
KIDUMU CHAMA CHA MAPINDUZI!
Imetolewa na;
Nape Moses Nnauye
Katibu wa NEC Itikadi na Uenezi
23/01/2014
Nape Moses Nnauye
Katibu wa NEC Itikadi na Uenezi
23/01/2014
0 comments:
Post a Comment