Saturday, 11 January 2014

JK ASEMA KATIBA MPYA NI LAZIMA MWAKA HUU

Filled under:



Rais  Jakaya Kikwete amesema Rasimu ya  mwisho ya Katiba Mpya itakamilika mwezi  Mei mwaka huu na kuwasilishwa kwa  wananchi kwa ajili ya kutoa maoni.
Aliyasema hayo jana katika hafla ya kuukaribisha mwaka mpya aliyowaandalia mabalozi wa nchi za nje  wanaoziwakilisha nchi zao nchini, Ikulu jijini Dar es Salaam.

Alisema kama mipango itakwenda kama ilivyopangwa Tanzania itakuwa na katiba yake mpya kabla ya mwisho wa mwaka huu.

“Nina furaha kwa kuwa rasimu ya pili ya Katiba mpya nimeshakabidhiwa  na inatarajiwa kujadiliwa kwenye Bunge maalumu la Katiba, Februari mwaka huu,” alisema.

Aliwaambia mabalozi hao kuwa  bunge hilo litajadili rasimu hiyo kwa siku zisizopungua 70 au zisizozidi 90.
Alisema baada ya kujadiliwa rasimu hiyo itapelekwa kwa wananchi kwa ajili ya kutoa maoni na kabla ya mwisho wa mwaka huu katiba mpya itapatikana.

Rais Kikwete alisema mwaka 2014 utakuwa mwaka wa kihistoria kwa kuwa Watanzania watakuwa wamepata katiba mpya.

“Tutakuwa tunasheherekea  miaka 50 ya Mapinduzi  ya Zanzibar na miaka 50 ya Muungano wa Zanzibar na Tanganyika  ambao uliunda Jamhuri ya Muungano wa  Tanzania,” alisema.

Aliwaomba mabalozi hao kuiombea Tanzania na watu wake kutimiza ndoto yao ya kufikia sherehe hizo.

Akizungumzia uchumi wa nchi, Rais Kikwete alisema umekuwa kwa asilimia 7.1 ukilinganisha na asilimia 6.9  mwaka 2012.

“Tunatarajia kuwa kiwango hicho kitaongezeka kufikia 7.3 kwa mwaka huu,” alisema.

Kuhusu tatizo la maji nchini, Rais Kikwete alisema tatizo la kupatikana kwa maji safi na salama kwa Watanzania ni changamoto kubwa inayoikabili serikali.

Alisema mpaka sasa kiwango kinachowafikia wananchi ni asilimia 57 tu katika maeneo ya vijijini  na asilimia 81 kwa maeneo ya mijini.

Alisema sekta hii imepewa kipaumbele kwa mwaka huu na miaka miwili ijayo na kwamba katika bajeti ya mwaka huu itazingatiwa kwa kupewa umuhimu wa kwanza.
 

0 comments:

Post a Comment