Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimesema kuwa
Mahakama Kuu haikuzuia kikao cha Kamati Kuu yake kujadili mambo mengine
yanayomhusu aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wake, Zitto Kabwe bali uanachama
wake pekee.
Juzi mahakama hiyo iliweka zuio, ikitaka chama
hicho kupitia kikao hicho kutojadili ajenda zozote zinazomhusu Zitto,
ambaye ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini.
Uamuzi huo ulitolewa na Jaji John Utamwa, baada ya
kupokea maombi ya Zitto kupitia wakili wake, Albert Msando kukata rufaa
yake iliyowasilishwa Baraza Kuu la Chadema kusikilizwa kwanza, kabla ya
kufanyika uamuzi mwingine.
Akizungumza na waandishi wa habari muda mfupi
kabla ya kuanza kwa kikao hicho cha Kamati Kuu jijini Dar es Salaam
jana, Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uenezi wa Chadema, John Mnyika
alisema: “Kuna watu walipotosha amri iliyotolewa na mahakama… Ilitoa
zuio la kujadili uanachama wa Zitto, lakini haikuzuia mambo mengine
kujadiliwa.”
Mnyika alifafanua: “Baada ya wao kufungua kesi ya
msingi kusema Kamati Kuu isijadili masuala ya uanachama wake mpaka pale
rufaa yake ambayo bado hajaikata itakapojadiliwa, ameeleza tu kusudio la
kutaka kuikata itakapojadiliwa na Baraza Kuu.”
Aliongeza kuwa jambo hilo liliwekewa pingamizi la
awali na mawakili wa chama hicho juzi na kwamba jana, walikuwa wakiandaa
majibu ya maswali yaliyofikishwa mahakamani na mpeleka madai (Zitto).
“Suala la hatima ya uanachama wake ndiyo
halitajadiliwa, lakini jambo jingine lolote likijitokeza, Kamati Kuu ya
chama ina haki ya kumjadili mtu yeyote yule,” aliongeza Mnyika.
Alisema kuwa mkutano huo utatangaza majina ya watu
waliopelekwa kwa Rais Jakaya Kikwete kwa ajili ya kuteuliwa kuwa
wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba.
Aliongeza kuwa Bunge la Katiba linapaswa kuchukua
maoni ya wananchi, huku akiwalaumu baadhi ya viongozi wa CCM kwa kuanza
kupinga pendekezo la Serikali tatu.
“Tayari CCM imekwishatoa msimamo ambao baadhi yao
wanauendeleza wa Serikali mbili, wakati wananchi wameshasema Serikali
tatu,” alisema.
Mnyika alibainisha kuwa mkutano huo pia utajadili
namna ambavyo Tume ya Taifa ya Uchaguzi(Nec), ambayo inalalamikiwa na
chama hicho kupewa kazi ya kusimamia uchaguzi na kwamba chama hicho
kinawasiwasi kuwa mchakato wa kura ya maoni utakuwa shakani.
“Bungeni tulitaka Daftari la Kudumu la Mpigakura
lingeboreshwa, lakini baadaye tulipomaliza Bunge, tume ikasema
halitaboreshwa,” alisema Mnyika.
Kabla ya kuanza kwa mkutano huo, wajumbe walionekana wakiwa na furaha huku wakizungumza katika makundi makundi nje ya ukumbi.
Wajumbe hao walipoingia ndani waliwataka waandishi
wa habari kuingia kupiga picha, kisha kutoka nje kwa kuwa
hawakuruhusiwa kusikiliza.
Saa 7:27 mchana, aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema,
Samson Mwigamba na aliyekuwa Mjumbe wa Halmashauri kuu, Dk Kitila Mkumbo
waliwasili katika eneo la mkutano, huku wakipokelewa na Mwenyekiti wa
Bazara la Vijana Chadema (Bavicha), John Heche na Mkurugenzi wa Ulinzi
na Usalama wa chama hicho, Willfred Lwakatare na kuwaelekeza sehemu ya
kukaa wakati wakisubiri kuitwa ndani kwenda kujitetea.
Zitto, Mwigamba na Dk Kitila walivuliwa nyadhifa
zao zote walizokuwa nazo ndani ya chama hicho baada ya kubainika kuwa
walikuwa wakiandaa waraka wa siri kwa ajili ya kukihujumu chama hicho,
ikiwamo kumng’oa mwenyekiti wake kinyume na kanuni, sheria na Katiba ya
Chadema.
0 comments:
Post a Comment