USHINDANI wa kisiasa kati ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) umefikia hatua mpya baada ya CCM
kuibuka na mkakati wa kumtumia Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe,
kupambana na CHADEMA waziwazi.
Katika mkakati huo CCM imepanga kukodisha helikopta ya kumpeleka
Zitto katika mikoa minne kwa gharama ya sh milioni 50 mara tu baada ya
CHADEMA kuhitimisha Operesheni yao ya M4C Pamoja Daima.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka vyanzo vilivyo karibu na Zitto na CCM,
yeye na chama hicho sasa wana adui mmoja – CHADEMA; na wameamua kujibu
mapigo baada ya kuridhika kwamba kwa vyovyote Zitto amekwisha kupoteza
uanachama wake katika CHADEMA.
Nia yao ni kumtumia Zitto kuleta mpasuko katika CHADEMA, na kufunika
mjadala wa mgogoro wa CCM, kero za wananchi na mchakato wa Katiba mpya.
Zitto ambaye alivuliwa nyadhifa zake zote ndani ya CHADEMA – Naibu
Katibu Mkuu Bara, Mjumbe wa Kamati Kuu, Mjumbe wa Baraza Kuu na Naibu
Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni – anatarajia kutumia
helikopta yenye uwezo wa kubeba watu wanne, ambayo inadaiwa kukodishwa
na wapinzani wa CHADEMA.
Kwa mujibu wa habari hizo, lengo la ziara ya Zitto ni kujibu mapigo
ya CHADEMA, hasa katika maeneo ambayo baadhi ya makada na viongozi wa
chama hicho wamepita na kuzungumzia hatima yake kisiasa, hasa walipojibu
maswali ya wananchi kuhusu sakata lake kuvuliwa uongozi kwa tuhuma za
usaliti, na hatimaye Zitto kwenda mahakamani kuzuia chama kujadili
uanachama wake.
Katika kesi ya msingi, Zitto aliyewahi kuwa maarufu akiwa kiongozi wa
CHADEMA, anaomba arudishiwe nyadhifa zake zote, na apatiwe nakala za
uamuzi wa Kamati Kuu (CC) ili aweze kukata rufaa Baraza Kuu.
Taarifa zinasema tayari chama kimempatia nyaraka hizo, lakini kwa
mujibu wa Katiba ya CHADEMA, Zitto amekwisha kujiondoa kwenye chama
hicho kwa kupeleka shauri mahakamani.
Taarifa za Zitto kuanza ziara mikoani zilianza kusikika mwishoni mwa wiki iliyopita.
Mikoa iliyotajwa ni Kilimanjaro, Arusha, Tanga, Morogoro na Dar es
Salaam, ingawa maandalizi yanaendelea na kuna uwezekano wa kubadili
baadhi ya mikoa kulingana na mkakati wao.
Kwa hadhi yake ya sasa, CHADEMA imeshasema haitahusika na mikutano
yake, na wanachama wake hawatajihusisha nayo. Uratibu wa mikutano yake
unafanywa na viongozi waandamizi wa CCM.
Baadhi yao walizungumza na gazeti hili kwa kujitapa kwamba hii ndiyo
njia ya kuimaliza CHADEMA, lakini hawakutaka kutajwa majina gazetini.
Iwapo Zitto atakubali ufadhili huo wa CCM na kuendelea na mikutano
yake, ni wazi atakuwa amekamilisha ushahidi wa kinachodaiwa na chama
chake kwamba amekuwa akikisaliti kwa masilahi ya CCM.
Hata hivyo, baadhi ya viongozi wa CCM walipoombwa maelezo juu ya
urafiki wao na Zitto kiasi cha kumkosanisha na chama kilichomlea
kisiasa, CHADEMA, walisema kwamba urafiki uliopo si wa Zitto na CCM,
bali Zitto na Rais Jakaya Kikwete.
Gazeti hili linafahamu kwamba wakati fulani mwaka juzi Zitto
alipobanwa na wabunge wenzake kuhusu tabia zake za kuwasaliti kwa Rais
Kikwete, alisisitiza kuwa Rais Kikwete ni rafiki yake binafsi, kwa hiyo
wamwelewe.
Vilevile, wapo wanaohoji nia ya ziara hii wakati kwa muda mrefu
amekuwa akikwepa kuambatana na viongozi wenzake katika ziara na
operesheni nyingi za kichama.
Wanasema kwa kuwa operesheni ya sasa ya CHADEMA imepewa jina la M4C
Pamoja Daima, kitendo cha CCM kuandaa ziara ya Zitto na kumkodishia
helikopta, ni uthibitisho kuwa Zitto hayuko pamoja na CHADEMA tena.
Wameongeza pia kuwa kama hilo litafanyika, litakuwa limemwingiza
Zitto katika orodha ya makada kadhaa wa upinzani waliotumikia CCM baada
ya kufukuzwa au kunyimwa fursa za uongozi katika CHADEMA, kama Tambwe
Hiza, Dk. Aman Walid Kabourou na Dk. Masumbuko Lamwai.
Alipotafutwa athibitishe kuhusu ziara hii na kama ni kweli inafadhiliwa na CCM, Zitto hakuweza kupatikana.
Mbowe kuwania tena uenyekiti
Katika hatua nyingine, Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na
Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe, amesema kuwa kamwe hatakiacha chama
hicho katika uchanga wa harakati za kulikomboa taifa kama kiongozi wake
wa juu.
Akihutubia katika mikutano ya Operesheni M4C Pamoja Daima katika
sehemu mbalimbali mkoani Morogoro jana, mwenyekiti huyo alisisitiza
kuwa, bado atagombea nafasi ya uenyekiti kwa lengo la kuendeleza
harakati za ukombozi wa pili wa taifa hili.
Bila kutaja jina, Mbowe alionya kuwa wenye fikra za kuachiwa chama
hicho kikiwa katikati ya ukombozi huo hawatapata nafasi, kwa sababu
hawana nia thabiti ya kukiendeleza, bali wana nia ya kukibomoa kwa
kutumiwa na wapinzani wa CHADEMA.
“Makamanda, kumbukeni kuwa chama hiki na sisi viongozi wake tumepita
katika majaribu makubwa na hata kukoswakoswa kuuawa. Mimi nimekoswakoswa
kuuawa kwa bomu huko Arusha, lakini pia kuna watu wamepoteza maisha,
wamefungwa jela, wengine wamekuwa vilema, halafu watu wengine
wanatusaliti kwa kupewa visenti ili wakivuruge chama na wanataka tuwape
chama. Huu ni uendawazimu,” alisema.
Mwenyekiti huyo alisema CCM imekuwa ikifanya jitihada za kuihujumu
CHADEMA kwa mbinu mbalimbali, zikiwemo za kupandikiza migogoro, jambo
ambalo limeshindwa kufanikiwa kwani Mungu ameweka mkono wake ili
kisisambaratike.
“Harakati hizi tunazofanya za kuwakomboa Watanzania mjue
tunahatarisha maisha yetu, tumejaribiwa kushawishiwa ndani na nje ya
Bunge ili tuwe kondoo, tumekataa. CCM wamekuja na mbinu za kupandikiza
migogoro wameshindwa na sasa wanaomba nife wakifikiri nikifa na CHADEMA
itakufa. Nawaambia CHADEMA haifi kwa kuwa tumezalisha makamanda wengi,
watakiendeleza,” aliongeza Mbowe.
Akielezea kwa mara ya kwanza kwa undani zaidi kuhusu mauaji ya
Arusha, mwenyekiti huyo alisema wana ushahidi wa kutosha kwamba polisi
walihusika na mauaji hayo na kuongeza kuwa waliohusika ni polisi wa
kutoka mkoani Morogoro.
“Kwa mara ya kwanza niliseme hili, mauaji ya Arusha yaliyofanyika kwa
kurusha bomu katika mkutano wa kampeni za CHADEMA, yalifanywa na polisi
ambao walitoka mkoani Morogoro. Ndiyo maana tunaendelea kumwambia Rais
Jakaya Kikwete aunde tume ya kimahakama ili kupata ukweli wa jambo
hili,” alisema.
Kuhusu Katiba
Akizungumzia msimamo wa CHADEMA kuhusu muungano, Mbowe alisema chama
hicho kinaunga mkono maoni yaliyokusanywa na Tume ya Mabadiliko ya
Katiba inayoongozwa na Jaji Joseph Warioba, ya serikali tatu.
Alisema hata tafiti mbalimbali zilizofanyika, zikiwemo za wanasheria
na wachumi zinaonyesha kuwa Muungano utaimalika zaidi chini ya muundo wa
serikali tatu.
“Nawaonya Wana CCM wasijaribu kuingilia mjadala wa Bunge la Katiba na
kama wanataka nchi ichimbike, basi walazimishe serikali mbili,” alisema
Mbowe.
“Zipo tetesi za CCM kutaka kupitisha hoja zao kwa nguvu kutokana na
idadi yao ndani ya wabunge zaidi ya 600, wakiwemo 356 wa Bunge la
Tanzania Bara, 84 kutoka Zanzibar na 201 kutoka makundi mbalimbali
watakaokwenda kwenye bunge hilo. Wasidanganyike kwamba wanaweza kutumia
wingi wao kubadilisha maoni ya Watanzania kuhusu serikali tatu,”
alisisitiza Mbowe.
Halima Mdee anguruma
Naye Mbunge wa Kawe, Halima Mdee, ambaye yuko katika msafara wa
mwenyekiti huyo, alisema vijana wengi wanaochipukia katika siasa kupitia
chama hicho, wamelelewa na Mbowe, ambao leo wamekuwa chachu ya
mabadiliko nchini.
“Ukweli ni kwamba kamanda huyu wa anga (Mbowe), ndiye ametulea vijana
wengi nikiwemo mimi, tena wengine hatukuwa na ujasiri tulionao sasa,
asiwadanganye mtu, hasa sisi vijana kwamba tuliingia CHADEMA na
umaarufu, hawapo hao, tumelelewa na huyo kamanda,” alisisitiza huku
akipigiwa makofi.
0 comments:
Post a Comment