Saturday, 4 January 2014

APEWA TUZO NA BILAL KUTOKANA NA KUWA NA UTAMADUNI WA KUMSINDIKIZA MKEWE KLINIKI

Filled under:



Kwa desturi iliyojengeka nchini, wanaume wengi hawana utamaduni wa kuwasindikiza wake zao kwenda kliniki kupima ujauzito au kupeleka watoto.
Hali hii inatokana na mfumo dume uliojengeka au wanaume kuona aibu kufanya hivyo au kuhofia kuchekwa na wenzake.
Licha ya tatizo hilo kwa walio wengi, hali ni tofauti kwa Elia Mwumbui (26), yeye ni mmoja wa wanaume wanaofaa kuigwa kutokana na kuthamini akitekeleza kwa vitendo  uzazi wa mpango kwa kuhudhuria kliniki, akiambatana na mkewe.
Kwa kutekeleza hilo na kutambua mchango wake, Taasisi ya Madaktari Wahitimu wa Vyuo Vikuu vya Tanzania (TPHI), imemtunukia Mwumbui, Tuzo ya Heshima ya Kutambua Mchango wake, kwa kupunguza vifo vya wajawazito.
“Sikujua kama ni raha kumsindikiza mke wangu kliniki, nimejifunza mengi ambayo kila mwanaume anatakiwa kumfanyia mke wake,” anasema Mwumbui
Mwumbui ambaye ni mkazi wa Kijiji cha Matongo, Wilaya ya  Ikungi, mkoani Singida, aliwavutia watu wengi kutokana na mazingira anayoishi kijijini, kuamua kujitoa kwenda na mke wake kliniki, jambo ambalo ni nadra kuliona.
Dk Telesephory Kyaruzi, Mkurugenzi Mkuu wa THPI, anasema kuwa wameamua kutambua mchango wa Mwumbui katika kupunguza vifo vya wajawazito kutokana na wakati wote kuhudhuria kliniki pamoja na mke wake.
Dk Kyaruzi ambaye alimtunuku Mwumbui tuzo hiyo anasema  kuwa, ili mwanamke aweze kulea ujauzito na kujifungua salama, mwanaume ana mchango mkubwa, wenye kumhamasisha mwanamke hasa anapomwona  akimhudumia kwa vitendo kwani hujisikia vyema.
Tuzo hizo za heshima kwa kuwa mstari wa mbele kuboresha afya ya mama na mtoto nchini, zilizotlewa na THPI ziwatambua watu wanane.
Watu hao walitunukiwa tuzo hizo na Makamu wa Rais, Dk Mohamed Gharib Bilal mapema Novemba mwaka jana, lakini kivutio zaidi alikuwa Mwumbui.
Mara baada ya kuitwa kuchukua tuzo hiyo katika viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam, Mwumbui alishangiliwa na umati wa watu ulihudhuria, huku baadhi wakiimba “Shemeji, ...shemeji, ...shemeji,’ kitendo kilichomfurahisha kila aliyekuwapo eneo hilo.
Mwumbui anavyosimulia 

Anasema kuwa mke wake, Joyce Vanda (23), aliposhika ujauzito wa pili  mwaka jana, alikwenda kliniki katika zahanati ya kijiji hicho cha Matongo na alipofika aliambiwa aje kunichukua twende sote.
Anasema kuwa baada ya kurejea nyumbani na kumpa taarifa ya kuwa na mimi natakiwa kwenda naye kliniki nilisita, lakini baadaye niliamua kwenda.
“Siku iliyofuata niliongozana naye, tulipofika kule tulipewa semina iliyohusu masuala ya malezi ya ujauzito na niliambiwa mke wangu asifanye kazi ngumu, kutembea umbali mrefu na kuinama mara kwa mara,” Mwumbui anasema.
Anaeleza kuwa baadhi ya wanaume, hawawaonei huruma wake zao wanapokuwa wajawazito na kuwaachia wafanye kazi zote za nyumbani, jambo ambalo ni hatari.

Aizungumzia tuzo
Anasema alichokuwa anakifanya, hakujua kama ipo siku angeweza kujulikana na kwamba kwani hakuwahi kufikiria kupata zawadi kama hiyo maishani.
Mwumbui anasema kuwa tuzo hiyo inatakiwa kuwa chachu kwa wanaume wengine kuiga mfano wa kuwapeleka wake zao kliniki na siyo kwamba wafanye hivyo wakisubili kupata chochote.
“Nimefurahi sana, sikuamini nilivyoambiwa nimeshinda tuzo ya heshima, kwanza tuzo yenyewe sikuwa naijua, ila namshukuru Mungu kwa kutambulika kitaifa. Wanaume wengine waige mfano wangu, kwani mimi sikujali maneno ya kejeli,  niliziba masikio na kufanya kile nilichokiamini mimi,” anasema Mwumbui.
Maneno ya kejeli
Akizungumzia ugumu aliokuwa akiupata kwa siku za mwanzoni, Mwumbu anasema kuwa alikuwa akiambiwa maneno ya kejeli na kashfa mbalimbali kutoka kwa vijana wenzake hivyo kumnyima raha.
“Si uanjua tena maneno ya vijana, walikuwa wakiniita mume bwege na maneno mengine kama hayo, lakini wao hawakuwa wakijua kuwa ni jambo la muhimu kumsindikiza mama kliniki,” anasema Mwumbui na kyuongeza:
“Maneno hayo hayakunikatisha tamaa, kadiri siku zilivyozidi kwenda, mimba imekuwa kubwa sasa, mimi ndiye ninayefanya kazi kama kufua, kupika na yeye anafanya zile kazi za kawaida tu.”

Wito kwa wanaume
Mwumbui anasema kuwa ili kufanikisha malengo ya utekelezaji wa kuwapo kwa uzazi wa mpango ni lazima kila mmoja akatekeleza wajibu wake katika familia.
Semina zinatolewa kila siku ya kliniki huwa ni nzuri na endapo mwanaume anakuwa jukumu hilo na kuliacha kwa mwanamke, hawawezi kufanikisha kuwa na uzazi wa mpango.
“Wanaume wasindikizeni wake zenu kliniki, kwani kuna mafunzo bora na yenye kujenga. Tubadilike, kwani maisha ya sasa ni kusaidiana tofauti na zamani ambapo mfumo dume ulivyokuwa ukiwakandamiza wanawake.
Serikali nayo inatakiwa kuweka mkazo kwa hospitali na zahanati zetu nchini kwa kutowahudumia wajawazito wanaofika kliniki bila kuwa na waume zao, hii itasaidia  kuhakikisha wanaume wanawasindikisha wake zao kliniki,” anasema Mwumbui.

Waliopata tuzo
Waliotunukiwa tuzo hizo za heshima na Dk Bilal ni pamoja na Rais, Jakaya Kikwete aliyechangia kupunguza vifo vya mama na mtoto tangu alipoingia madarakani  mwaka 2005, Rais Mstaafu, Ali 

Hassan Mwinyi kwa kupigana vita dhidi ya maambukizi ya Virusi vya Ukimwi enzi za utawala wake na jitihada zake za mara kwa mara za matembezi ya hisani ya kuchangisha fedha za kuwatibu watoto wenye matatizo ya moyo na saratani.

Wengine ni Rais Mstaafu, Benjamin Mkapa ambaye kupitia taasisi yake ya Mkapa Foundation kwa kujali afya ya mama na mtoto na kuboresha miundombinu ya utoaji wa huduma za afya nchini akiwamo pia Mama Salma Kikwete kupitia Taasisi ya Wanawake na Manedeleo (WAMA).

Mkurugenzi wa Kampuni za IPP, Dk Reginald Mengi pia alipata tuzo kwa kuisaidia jamii kupitia vyombo vyake vya habari, Dk Faraja Nipwapwacha kwa juhudi zake kwa pindi cha miaka miwili mfululizo ambapo kituo chake hakikuwa na kifo cha mjamzito kuanzia  mwaka 2010 hadi 2013.
Tuzo hizo hazikuishia hapo kwani muuguzi na mkunga wa Hospitali ya Mpanda mkoani Katavi, alitunukiwa tuzo kwa kujitolea damu na kumwongezea mwanamke mwenzake aliyetokwa na damu nyingi wakati wa kujifungua, huku wa mwisho akiwa Elia Mwumbui.

0 comments:

Post a Comment