Saturday, 30 November 2013

MTUHUMIWA WA WIZI M-PESA ATOROKA NA KUWAACHIA KASHFA POLISI

Filled under:



Jeshi la Polisi limeingia kwenye kashfa ya kumuachia mtuhumiwa wa wizi wa fedha zaidi ya sh milioni 1.2 kwa kutumia njia ya utapeli kwenye huduma ya kutoa na kuweka fedha kwa njia ya simu ya Kampuni ya Vodacom (M-pesa).

Tukio la utatanishi la kuachiwa kwa kijana huyo aliyefahamika kwa jina la Ahmed Ahmad, limethibitishwa na askari aliyekuwa ameshikilia faili lake, Venance Ngeze ambaye alidai kuwa mtuhumiwa huyo alitoroka jana asubuhi alipokuwa kwenye chumba cha mahojiano.

Ilielezwa kuwa kabla ya kutoroka, mtuhumiwa huyo alilala selo siku moja baada ya walalamikaji ambao ni mawakala wa M-pesa, Melina Marki, Rose Marki na Teresia Wilhad kukataa kushawishiwa kufuta kesi hiyo kwa makubaliano ya kurudishiwa fedha zao wanazodai kuibiwa na Ahmad.

Katika tukio hilo, Melina alidai aliibiwa sh 300,000, Rose sh 684,000 na Teresia sh 229,000. Wote wameibiwa katika ofisi zao zilizopo maeneo tofauti katikati ya Jiji la Dar es Salaam.
Melina alieleza kuwa mtuhumiwa huyo amekuwa akifika katika shughuli zao akiwa na kadi za Vodacom zaidi ya 150 alizokuwa akihitaji kusajiliwa ambapo baadaye iligundulika kuwa huzitumia kwa utapeli.

“Alifika kwangu akiwa na kadi za simu 150 na kuhitaji huduma ya kuzisajili, lakini alikuja hana vielelezo ndipo akasema kuwa anaomba tuendelee kumsajilia yeye anaenda kutoa photocopy ya kitambulisho, huku akiwa ameacha simu yake ya mkononi na kiasi kidogo cha fedha, kuonyesha kwamba anarudi, lakini aliporudi aliniambia amekosa photocopy, ila anahitaji kutoa fedha kwenye simu yake.

“Nikamtajia namba yangu ya uwakala, akatoa na ujumbe ukaja ukionyesha anatoa kiasi cha sh 300,000 baada ya kuondoka nilishangaa kadi yangu ya simu ilikuwa imefungwa, nilipokwenda Vodacom kujua sababu ya kufungiwa, nilielezwa kwamba hawatanifungulia kwa sababu bado wanamtafuta mtu anayefanya mchezo huo,” alisema Melina.

Naye Teresia akielezea tukio hilo, alisema mtuhumiwa huyo ambaye hutumia kadi za simu ambazo zimekuwa zikisajiliwa bila ya kuwa na picha za kitambulisho kwa nia ya kuondoa ushahidi pindi linapotokea tatizo la kufungiwa, alifika na kumtaka atoe kiasi cha sh 229,000 huku akiomba asajiliwe kadi zaidi ya 150, lakini baada ya kumshughulikia naye alijikuta simu kadi yake ikifungwa pasipo kujua sababu hadi pale alipokwenda Vodacom.

“Baada ya kufika Vodacom, waliniambia kwamba hawataweza kuifungua kwa sababu wanamtafuta mtuhumiwa anayefanya mchezo huo wa kuiba fedha, kwani kumekuwa na malalamiko mengi yaliyoripotiwa katika ofisi hizo,” alisema Teresia.
Akielezea kushangazwa kwake na kutoroka kwa mtuhumiwa huyo, 
 Melina anayefanya shughuli zake Mtaa wa Samora, alisema kuwa 
baada ya kufika katika kituo hicho jana, walielezwa na askari Venance aliyemkamata mtuhumiwa huyo juzi kuwa ametoroka katika mazingira ya kutatanisha huku akiwa ameacha  sh 300,000 na vifaa vyake vingine.

Anasema kuwa Venance aliwaeleza kuwa baada ya mtuhumiwa huyo kutoroka, alichukua uamuzi wa kuwakamata ndugu zake wawili waliokuwa wamefika kwa ajili ya kumdhamini ili aweze kumpata kirahisi mtuhumiwa huyo, huku akiwaomba walalamikaji kukubali kulimaliza suala hilo kinyemela.
Taarifa ilizozipata Tanzania Daima zinasema kuwa mtuhumiwa huyo hakutoroka kama ilivyoelezwa, ila aliachiwa na kuwaacha ndugu zake na vifaa vyake ikiwa kama dhamana ili akatafute fedha za kuwalipa walalamikaji wa tukio hilo.

Akizungumzia tukio hilo, Kamanda wa Kipolisi wa Mkoa wa Ilala, Marietha Minangi, alisema kutokana na mazingira ya kutoroka kwa mtuhumiwa huyo, Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi na endapo litabaini kuwa askari huyo alimuachia kwa uzembe litamchukulia hatua kwa kosa la kinidhamu.
Kamanda Minangi alisema jukumu la kumtafuta mtuhumiwa huyo amekabidhiwa polisi aliyedaiwa kumuachia mtuhumiwa, na walalamikaji wakatakiwa kurudi leo saa nne asubuhi.


0 comments:

Post a Comment