NAIBU Waziri wa zamani wa Maji, Anthony Diallo, amesema dhana
inayojengwa kwamba Mradi wa Maji wa Ziwa Victoria ulifanikishwa kwa
nguvu ya aliyekuwa Waziri, Edward Lowassa, ni potofu na afadhali
angetajwa yeye.
Katika mazungumzo na Raia Mwema yaliyofanyika mjini Mwanza wiki hii na
ambayo yatachapishwa katika gazeti dada la hili la Raia Tanzania kesho,
Diallo ambaye sasa ni Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa
Mwanza, ameweka wazi kwa kila hatua kuhusu mradi huo.
Kimsingi, Diallo ameeleza kwamba mradi huo wa maji ulitokana na ahadi
iliyotolewa na Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa, kwa wananchi wa
Kanda ya Ziwa mwaka 2000 na kama ingekuwa sifa ni bora zingeenda kwake.
“Kwanza kuna vitu viwili. Cha kwanza miradi yote inayolipiwa na kodi za
wananchi ni jukumu la serikali iliyoko madarakani, sidhani anaweza
kutokea mtu mmoja kudai kwamba nilifanikisha hiki.
Ukienda kwa staili
hiyo ndiyo watu wanasema ile dhana ya wabunge kuwa mawaziri inaleta
haya matatizo kwamba mtu anavutia kwake akiwa na nia fulani, sasa hao
wanaodai kwamba walifanya hivi definitely lazima ujue kwamba wana nia fulani, wanataka kuwavutia wapiga kura kwamba wao wanawajali sana.
Sitakueleza
mambo ambayo ni siri ya Baraza la Mawaziri, siwezi kuitoa, lakini moja
ni kwamba mradi huo ulikuwa ahadi ya Rais Mkapa, mwaka 2000 wakati
anaomba kura kipindi cha pili, alipopita Shinyanga na Kahama alisema
lazima tufanye chini juu tutajenga mradi wa maji kuelekea huko kutoka
Ziwa Victoria.
Sasa ngoma ilikuwa ni pesa zitapatikana wapi,
mwaka 2002 tukaanza mazungumzo makali sana na nchi hizi zilizo kwenye
Bonde la Nile, na bahati nzuri mimi ndiye nilihudhuria vikao vyote,
mpaka tukafika mahali tukauvunja ule mkataba wa Misri na Uingereza, kwa
sababu walikuwa wanatuzuia tusitumie maji ya Ziwa Victoria na hiyo
mikutano yote nimehudhuria mimi, Addis Ababa. Na nimshukuru sana waziri
mwingine aliyenisaidia, maana nilikuwa vocal sana, Martha Karua wa
Kenya, aliyekuwa Waziri wa Maji wakati huo,”
alisema Diallo.
Kauli hii ya Diallo ni ya kwanza kutamkwa hadharani kuhusiana na mradi huo ambao mara nyingi
umekuwa ukitajwa na wapambe wa Lowassa kuwa kati ya
kete zake muhimu ndani ya chama chake kuelekea kwenye Uchaguzi Mkuu wa
mwakani.
Wapambe hao wamekuwa wakisema ni Lowassa aliyeusukuma na kuusimamia
tangia kwenye mchakato wa kuondoa tatizo la maji kwa wananchi wa Kanda
ya Ziwa, hasa Shinyanga na Kahama.
Katika mazungumzo hayo, Diallo alieleza ya kuwa akiwa Naibu Waziri chini
ya Lowassa, namna alivyoshiriki katika kila hatua kabla ya kuhamishwa
wizara.
“Baada ya hapo ikaja ngoma kwamba huu mradi utapate pesa kutoka wapi.
Mimi nikafanya utafiti mdogo nikagundua kwamba tusingeweza kupata hela
za wahisani kokote kwa sababu World Bank (Benki ya Dunia) jamaa wa
Misri wamejaa hata IMF (Shirika la Fedha Duniani) kote kule wamejaa.
Lakini
pia tukakumbuka miaka ya 1960 tulipokazana kuchukua haya maji kwenye
mradi ule wa Wendele, nchi za Scandinavia zikazuia kwamba tusichukue
maji Ziwa Victoria badala yake wakasema tuchimbe malambo, yakaja
matrekta mengi na kwa sababu tulikuwa hatuna ufundi matrekta hayo mengi
yamekuja kukusanywa kwenye vyuma chakavu, kama unakumbuka kulikuwa na
katapila karibu kila kijiji mengi yamekuja kukusanywa kama vyuma
chakavu. Kwa hiyo ilikuwa ni tabu sana pesa mtapata wapi.
Nikaja
na wazo kwamba kwanini tusiombe pesa kwa Rais, tutumie pesa zetu
wenyewe, wakati huo pesa za makusanyo ya kodi zilianza kupanda sana.
Basi tukamwandikia barua Rais, tukamwambia uwezekano wa kupata funding
ni mdogo sana, kwa hiyo akakubali tutumie pesa zetu wenyewe.
Wakati
ule huo mradi ulikadiriwa kumalizika kwa bilioni 27. Mimi nikaja na
wazo pale wizarani, nikawaambia kwa pesa hiyo huu mradi hauwezi kuisha ,
kwanini tusilishawishi Baraza la Mawaziri tufanye kwa awamu, tukaandika
mradi wetu na matarajio yote tukakubaliwa.
Ili tujenge kwanza
pampu na lile tenki la Ihelele (kijiji kando ya ziwa unakoanzia mradi
huo) hiyo ilikuwa awamu ya kwanza bilioni 27 zingeishia hapo. Nikawa
nawatania wizarani kwamba tukishafikisha maji pale (Ihelele) hakuna
Wizara itakayopinga tusichukue hela kuyapeleka maji mbele.
Awamu
ya pili ilikuwa umeme tutaupata wapi, kwa sababu pale (kwenye chanzo cha
maji) ni porini tu, mara ya kwanza tukakubaliana kwamba tujenge sub
station (kituo kidogo) lakini Tanesco hawakuwa waangalifu sana ule mradi
tukaliwa, kwa sababu waliweka nguzo na nyaya ambazo ni sub standard
(chini ya kiwango) zisingeweza kuendesha yale mapampu.
Tukaja na
wazo la kuchukua umeme Kahama Mining, ikadibi tufanye hivyo, zile nguzo
za awali zikatelekezwa. Hapo serikali tulikula hasara, ingawa si mbaya
kwa sababu tulikuwa tunafanya kitu kinaitwa learning curve na watalamu
wetu hawakuwa wazuri kiasi hicho.
Idea ya pili niliyoitoa mimi,
nilikuwa mtu wa kwanza kuleta ule utaratibu wa design and build,
nikawaambia hapa tukitaka tuweke feasibility study (upembuzi yakinifu),
tutazeekea hapo mradi hautakamilika.
Kwa hiyo mkandarasi
tutakayempa atakuwa ana design, tunaipitia design (michoro) yake na
consultant (mtaalam mshauri) tutakuwa tumeshamuweka tunakubaliana
anajenga ili mradi tunajua bei haiwezi kuvuka hapo.
Hata
mkimuuliza Waziri Lowassa (Edward Lowassa Waziri wa Maji wakati huo)
anakumbuka. Ule mradi ulikuwa mikononi mwangu, yeye alikuwa
anashughulikia DAWASA. Tulikubaliana kugawana mimi nisimamie mradi wa
Shinyanga yeye asimamie DAWASA, nilikuwa na maamuzi yote.
Huo
mradi ndiyo ulikuwa hivyo, lakini ku- single out (huwezi kusema) kwamba
nani aliukubali au aliukataa, ninajua waliokuwa wanaupinga lakini siwezi
kusema ni nani kwa sababu ilikuwa ni siri, uamuzi wa Baraza la Mawaziri
ni siri,”
alisema Diallo.
Septemba mwaka jana, Lowassa alinukuliwa katika vyombo vya habari
akieleza kwamba wakati alipopendekeza mradi huo wa maji kwenye Baraza la
Mawaziri wakati wa enzi ya Mkapa, ni mawaziri wawili tu ndiyo
waliomuunga mkono.
Akizungumza katika Kanisa la AICT mjini Kahama, Shinyanga, Lowassa
alinukuliwa akiwataja mawaziri waliomuunga mkono kuwa ni Jakaya Kikwete
ambaye alikuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wakati
huo na Muhammed Seif Khatib aliyekuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais
(Muungano).
|
Katibu mwenezi mkoa wa Shinyanga ndugu Emmanuel Mlimandago |