Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi DAVID MISIME - SACP amesema tarehe 25/09/2014 alfajiri vimeokotwa vipeperushi maeneo mbalimbali mjini Dodoma vyenye ujumbe ufuatao: ONYO – DODOMA SI MAHALI PA KUFUGA WEZI WA FEDHA ZA UMMA. UTAKAYEINGIA BUNGENI KUANZIA KESHO, YATAKAYOKUPATA UTAJUTA.
Kamanda MISIME amesema tumeendelea kupokea taarifa za watu wanaodaiwa kuandaa vipeperushi hivyo na tunafanyia kazi ili tuweze kuwakamata ili washtakiwe kulingana na kosa walilolitenda hasa la kutoa vitisho na kuhamasisha uvunjifu wa amani.
Aidha Kamanda MISIME ameongeza ametoa wito kwa wananchi na wageni wanaofika Dodoma watii sheria bila shuruti. Kila mmoja ajiepushe kujiingiza kwenye kuhamasisha uvunjifu wa amani, kujiingiza katika mikusanyiko isiyo halali na maandamano ambayo yameshapigwa marufuku na Jeshi la Polisi.
Atakayekiuka na kujiingiza katika vitendo hivyo vya kiuhalifu atashurutishwa kwa nguvu zote kwa mujibu wa sheria za Nchi na kwa mamlaka iliyopewa Jeshi la Polisi.
Kamanda MISIME ameongeza kuwa wananchi na wageni wapenda amani waendelee na shughuli zao kama kawaida kwani Jeshi la Polisi limejiimarisha ipasavyo kukabiliana na yeyote yule atakayekiuka sheria na maelekezo yaliyotolewa.
- Taarifa ya Sylvester Onesmo wa Jeshi la Polisi, Dodoma.
0 comments:
Post a Comment