Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Uhusiano na Uratibu, Stephen
Wassira akiwakilisha CCM, Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu na
Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba, jana walitoana jasho katika
mdahalo wa Katiba ulioandaliwa na East African Business and Media
Institute.
Mdahalo huo uliohudhuriwa na watazamaji wapatao
500, ulikuwa na mada inayosema: ‘Nani anakwamisha Upatikanaji wa Katiba
Mpya.’ Kila upande ulitumia fursa hiyo kutupa shutuma kwa mwingine huku
jazba na kelele vikitawala miongoni mwa waliohudhuria.
Hata hivyo, suala la muundano wa serikali ndiyo
uliochukua nafasi kubwa katika mdahalo huo huku Umoja wa Katiba ya
Wananchi (Ukawa) ukiishutumu Serikali ya CCM kuwa ndiyo kikwazo cha
upatikanaji wa Katiba Mpya nayo ikitupa mpira huo kwa Ukawa kwa kitendo
chake cha kutoka katika Bunge Maalumu la Katiba.
Profesa Lipumba alisema wahafidhina wa CCM ndiyo
waliomshauri Rais Jakaya Kikwete abadilike kimsimamo kuhusu upatikanaji
wa Katiba Mpya.
“Rais Kikwete alikuwa na nia njema kabisa kuhusu
Katiba Mpya lakini wahafidhina wa CCM wanaopenda madaraka walipoona
muundo wa serikali tatu wakambana naye akabadilisha msimamo, tunamwomba
abadilike, nchi hii ni yetu sote ili tupate katiba ya wananchi,”
alisema.
Lissu aliongeza kwa kusema kuwa anayekwamisha
upatikanaji wa Katiba Mpya ni CCM ambao wanaweka maoni yao badala ya
kujadili rasimu iliyotolewa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba ambayo ndiyo
maoni ya wananchi.
“Hatuwezi kurudi kwenye Bunge Maalumu la Katiba
kwenda kujadili rasimu ya CCM kwa sababu wanaonyesha hawana nia ya
Katiba Mpya, bali wanataka kuwadanganya Watanzania, watawadanganya
wananchi kwa kuleta Katiba ileile ila ikiwa na rangi tofauti,” alisema
huku akishangiliwa.
Alisema Ukawa hawawezi kushiriki katika
udanganyifu wa aina hiyo na kwamba wameamua kuwaachia CCM ili wananchi
waweze kuwahukumu kwa uovu watakaoufanya.
Alisema kati ya wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba
katika Kundi la 201, wajumbe 166 ni wana CCM walioteuliwa ili kuongeza
idadi ya watu.
“Humo kuna viongozi wa dini mashehe na maaskofu na
waganga wa kienyeji ambao ni wana CCM ili wapitishe Katiba yenye
masilahi yao binafsi,” alisema.
Hata hivyo, Wassira alisema hoja za Ukawa hazina
mashiko na kumtaka Lissu kuwaomba radhi masheikh na maaskofu kwa kuwa
hawakuteuliwa na Rais kutokana na kuwa wanachama wa CCM, bali ni
mapendekezo ya taasisi wanazozitumikia.
“Namwomba Tundu Lissu akawaombe radhi masheikh na
maaskofu kwa sababu kundi hili liliteuliwa kutokana na mapendekezo ya
wahusika wenyewe pasipo shinikizo la Rais. Hapakuwa na uwezekano wa Rais
kuwatambua wana CCM ili awateue wanaofaa. Kama ana ugomvi na Kingunge
Ngombale Mwilu aseme.”
Alisema wanaokwamisha upatikanaji wa Katiba Mpya ni Ukawa...
“Katiba Mpya haiwezi kupatikana mitaani, bali kwa majadiliano na
maridhiano kwenye Bunge Maalumu la Katiba, nawashauri warudi bungeni ili
tuweze kupata Katiba Mpya.”
Alisema Bunge Maalumu la Katiba lina mamlaka ya
kubadilisha vifungu kwenye rasimu ya Katiba na kwamba halipo kwa ajili
ya kupitisha tu vifungu vilivyowekwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Kauli hiyo ya Wassira ilifanya kila aliposimama
kuzomewa na wananchi waliohudhuria mdahalo huo huku wafuasi wa Chadema
na CCM wakitishiana kupigana hali iliyosababisha mabaunsa kuwatoa nje ya
ukumbi baadhi yao walioshindwa kustahimiliana.
Wajumbe wawili waliokuwa katika Tume ya Mabadiliko
ya Katiba, Humphrey Polepole na Awadh Said, katika michango yao
walitaka kuheshimiwa kwa maoni ya wananchi ili kupata katiba
itakayowafaa kwa muda uliokusudiwa.
Polepole alisema tatizo la wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba ni masilahi binafsi na ya makundi katika utafutaji wa Katiba Mpya.
“Wananchi wasimamie masilahi ya taifa na
wasiwaachie mchakato mzima wanasiasa ambao wana masilahi binafsi pamoja
na yale ya kikundi yenye shinikizo la masilahi binafsi,” alisema
Polepole.
Awadh alisema maoni yalikusanywa kutoka katika
mabaraza ya katiba 170 na 600 ya taasisi na vyama vya siasa kutoka
katika wilaya zote 43 za Zanzibar.
“Kwa nini juhudi zote hii zibadilishwe na wajumbe
629 peke yao kwenye Bunge Maalumu la Katiba? Tufuate maoni ya wananchi
kupitia tume ndipo tutakuwa tunawatendea haki Watanzania,” alisema.
Alielezea kusikitishwa na kitendo cha Serikali
kufunga tovuti ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba akisema kimewanyima
wananchi haki ya kupata taarifa mbalimbali za tume hiyo.
0 comments:
Post a Comment