HOTUBA YA WAZIRI MKUU, MHESHIMIWA
MIZENGO
PETER PINDA (MB), KUHUSU MAPITIO NA MWELEKEO WA KAZI ZA SERIKALI NA
MAKADIRIO YA MATUMIZI YA FEDHA YA OFISI YA WAZIRI MKUU NA OFISI YA BUNGE
KWA MWAKA 2014/2015
UTANGULIZI
1. Mheshimiwa Spika, naomba
kutoa hoja kwamba, kutokana na Taarifa zilizowasilishwa katika Bunge
lako Tukufu na Wenyeviti wa Kamati za Katiba, Sheria na Utawala; Kamati
ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa; Kamati ya Uchumi, Viwanda na
Biashara na Kamati ya Masuala ya UKIMWI zilizochambua Bajeti ya Ofisi ya
Waziri Mkuu, Bunge lako sasa lipokee na kujadili Taarifa ya Mapitio ya
Utekelezaji wa Kazi za Serikali kwa mwaka 2013/2014 na Mwelekeo kwa
Mwaka 2014/2015. Aidha, naliomba Bunge lako Tukufu likubali kupitisha
Makadirio ya Matumizi ya Fedha ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Ofisi ya Waziri
Mkuu - Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Taasisi zilizo chini yake
pamoja na Ofisi ya Bunge kwa mwaka 2014/2015.
2. Mheshimiwa Spika, awali ya yote na kwa masikitiko makubwa
naomba nichukue fursa hii kutoa salamu za pole kwako na kwa Bunge
lako Tukufu kwa kuondokewa na wabunge wawili, Mheshimiwa William
Augustao Mgimwa, aliyekuwa Mbunge wa Kalenga, aliyefariki tarehe 01
Januari, 2014 na Mheshimiwa Saidi Ramadhani Bwanamdogo, aliyekuwa Mbunge
wa Chalinze, ambaye alifariki tarehe 22 Januari 2014. Aidha, niwape
pole Wananchi wa Mkoa wa Mara kwa kifo cha Mheshimiwa John Gabriel Tupa
aliyekuwa Mkuu wa Mkoa huo, kilichotokea tarehe 25 Machi 2014, na kwa
Wananchi wa Wilaya ya Urambo kwa kifo cha Mheshimiwa Anna Magowa
aliyekuwa Mkuu wa Wilaya hiyo, kilichotokea tarehe 24 Septemba 2013.
Vilevile, natoa pole kwa Wananchi wa Wilaya ya Kalambo kwa kifo cha
Mheshimiwa Moshi Mussa Chang’a aliyekuwa Mkuu wa Wilaya hiyo,
aliyefariki tarehe 21 Aprili 2014. Naomba pia niwape pole Waheshimiwa
Wabunge na Wananchi wote waliofiwa na ndugu na jamaa zao kutokana na
majanga na matukio mbalimbali tangu nilipowasilisha Bajeti yangu ya
mwaka 2013/2014.
Tunamwomba
Mwenyezi Mungu aziweke roho za marehemu wote mahali pema Peponi. Amina!
Nichukue fursa hii pia kuwapa pole Wahanga wote wa majanga mbalimbali
yakiwemo mafuriko na ajali za barabarani, na niwashukuru kwa dhati wote
waliotoa misaada ya hali na mali wakati wa ajali na maafa hayo.
3. Mheshimiwa Spika, katika
kipindi cha 2013/2014, Bunge lako Tukufu limepata Wabunge wapya watatu
ambao ni Mheshimiwa Yusuf Salim Hussein, Mbunge wa Chambani; Mheshimiwa
Godfrey William Mgimwa, Mbunge wa Kalenga; na Mheshimiwa Ridhiwan Jakaya
Kikwete, Mbunge wa Chalinze. Nawapongeza kwa kuchaguliwa kuwawakilisha
Wananchi katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Nawaomba
watumie fursa waliyoipata kwa manufaa ya Wananchi na Taifa kwa ujumla.
MAANDALIZI YA BAJETI
4. Mheshimiwa Spika,
huu ni mwaka wa pili tangu tuanze utaratibu wa Mzunguko mpya wa Bajeti
ambao unatuwezesha kukamilisha Mjadala wa Bajeti ya Serikali ifikapo
tarehe 30 Juni ya kila mwaka. Taarifa za awali zinabaini kwamba
utaratibu huu umeanza kuonesha mafanikio ya haraka katika utekelezaji wa
kazizilizopangwa. Bajeti hii imeendelea kutayarishwa kwa
kuzingatia utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha
Mapinduzi ya mwaka 2010; Awamu ya Pili ya Mkakati wa Kukuza Uchumi
na Kuondoa Umaskini Tanzania (MKUKUTA II); Mpango wa Kwanza wa
Maendeleo wa Miaka Mitano wa Mwaka 2011/12 hadi 2015/16; Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025; Malengo ya Maendeleo ya Milenia 2015; na Mfumo wa Tekeleza Sasa kwa Matokeo Makubwa (Big Results Now – BRN).
Katika mwaka 2014/2015, Serikali itaendelea kutekeleza miradi ya
kipaumbele iliyoainishwa kwenye mipango hiyo ya Kitaifa ili kuleta
maendeleo endelevu na ya haraka yatakayowanufaisha Wananchi wa
Tanzania.
5. Mheshimiwa Spika,
nawashukuru Wajumbe wa Kamati zote za Kudumu za Bunge lako Tukufu kwa
mchango wao mkubwa wakati wa uchambuzi wa Makadirio ya Mapato na
Matumizi ya Wizara, Mikoa, Wakala, Idara za Serikali Zinazojitegemea na
Mamlaka za Serikali za Mitaa. Kazi waliyoifanya ni kubwa na ambayo
imetuwezesha kukamilisha maandalizi ya Bajeti ninayoiwasilisha leo.
Maoni na Ushauri wao utazingatiwa wakati wa kukamilisha mjadala wa
Bajeti ya Serikali na utekelezaji wake.
HALI YA SIASA
6. Mheshimiwa Spika, kwa
ujumla hali ya siasa Nchini ni tulivu na Vyama vya Siasa vinaendelea
kutekeleza majukumu yao. Nchi yetu inapitia kwenye kipindi cha mpito
ambapo tunaandika Katiba Mpya itakayoweka mustakabali wa mwelekeo wa
Taifa letu kwa miaka mingi ijayo. Nawasihi Wanasiasa na Wananchi wote
kwa ujumla kutoa ushirikiano mkubwa wakati wa maandalizi ya Katiba hiyo
ambayo baadaye wananchi wote wataipigia kura ya maoni. Nawaomba
tushindane kwa nguvu ya hoja na si hoja ya nguvu katika kuandaa Katiba
hii ambayo itatuongoza sasa na vizazi vijavyo.
7. Mheshimiwa Spika, katika
jitihada za kukuza na kuimarisha demokrasia ya vyama vingi Nchini,
Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa imeratibu shughuli za Vyama vya
Siasa kwa kuhakikisha kunakuwepo na fursa sawa katika shughuli za siasa
Nchini. Hadi Aprili 2014, idadi ya Vyama vya Siasa vyenye Usajili wa
kudumu imefikia 21 baada ya Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA) kupata
usajili wa kudumu mwezi Juni, 2013. Aidha, Chama cha Alliance for Change
and Transparency (ACT-TANZANIA), Chama cha Wananchi na Demokrasia
(CHAWADE) na Chama cha Maridhiano na Uwiano (CMU) vimepata usajili wa
muda. Nirejee wito wangu kwa Viongozi na Wanachama wa vyama vyote vya
siasa kuendeleza utamaduni wa kuvumiliana na kutohamasisha siasa za
chuki na vurugu ambazo zinaweza kutugawa na kuhatarisha amani, utulivu
na umoja wa Taifa letu tulioujenga kwa miaka mingi.
ULINZI NA USALAMA
8. Mheshimiwa Spika,
Nchi yetu imeendelea kudumisha amani na utulivu kama tunu ya Taifa
iliyojengwa na kuimarishwa tangu tulipopata uhuru. Katika mwaka
2013/2014, Jeshi la Polisi limeendelea kutekeleza Programu ya Maboresho
ya Jeshi na Mkakati wa Kupunguza Uhalifu ambavyo vimeongeza ushirikiano
na wananchi. Jeshi hilo limeongeza Vikundi 1,778 vya Ulinzi Shirikishi
na kufikia vikundi 6,798 kwa mwaka 2013 kwa Nchi nzima. Vikundi hivyo
vimechangia kupunguza vitendo vya uhalifu Nchini kutoka Asilimia 4.3
mwaka 2012 hadi Asilimia 2.8 mwaka 2013 na hivyo kuchangia kupungua kwa
makosa makubwa na madogo ya jinai kutoka makosa 566,702 mwaka 2012 hadi
makosa 560,451 mwaka 2013.
Mauaji ya Wanawake
9. Mheshimiwa Spika,
pamoja na juhudi zinazofanywa na Serikali kwa kushirikiana na Wananchi
katika kuimarisha ulinzi na usalama wa raia, hivi karibuni kumetokea
wimbi la mauaji ya kikatili dhidi ya wanawake. Katika kipindi cha
Januari hadi Aprili 2014, wanawake wanane (8) wameuawa kikatili katika
Kata za Mugango, Etaro, Nyakatende na Nyegina Wilayani Butiama.
Uchunguzi uliofanyika umebaini kwamba, mauaji hayo yamefanyika mchana na
kwa mtindo unaofanana wa kunyongwa na kanga au kamba na miili yao
kufukiwa kwenye mashimo mafupi au kufichwa vichakani. Mara zote walengwa
ni wanawake wanapokuwa kwenye shughuli zao za kilimo.
10. Mheshimiwa Spika, Serikali
inalaani vitendo hivyo visivyokubalika katika jamii na itawachukulia
hatua kali za kisheria wale wote watakaobainika kuhusika kwa namna
yoyote. Serikali imechukua hatua kadhaa za kudhibiti vitendo hivyo vya
mauaji ikiwa ni pamoja na kuwakamata watuhumiwa 26 na kati yao 13
wamefikishwa mahakamani. Vilevile, Jeshi la Polisi limeunda kikosi kazi
kwa ajili ya kudhibiti hali hiyo na kufanya mikutano ya kuhamasisha
jamii kuhusu kuanzisha na kuimarisha vikundi vya Polisi Jamii. Nitoe
wito kwa wananchi wema, wenye upendo na Nchi yetu kutoa taarifa za
uhalifu na wahalifu kwenye vyombo vya usalama ili Sheria ichukue mkondo
wake.
Ajali za Barabarani
11. Mheshimiwa Spika,
ajali za barabarani zimeendelea kuwa tishio kwa maisha ya watu na mali
zao. Takwimu za Jeshi la Polisi zinaonesha kuwa katika mwaka 2013,
kulitokea ajali za barabarani 24,480 zilizosababisha vifo vya watu 4,091
na majeruhi 21,536 ikilinganishwa na ajali 23,604 zilizosababisha vifo
vya watu 4,062 na majeruhi 20,037 mwaka 2012. Kwa
upande wa pikipiki pekee, mwaka 2012 zilitokea jumla ya ajali 5,763 na
kusababisha vifo 930 na majeruhi 5,532. Mwaka 2013, zilitokea ajali
6,831 na kusababisha vifo 1,098 na majeruhi 6,578. Aidha, katika kipindi
cha Januari hadi Machi, 2014 zimetokea ajali 1,449 na kusababisha vifo
218 na majeruhi 1,304. Ajali hizi ni nyingi na zinasababisha vifo
vingi na majeruhi ambao wengi wao ni nguvukazi ya Taifa. Ni vyema
ikumbukwe kwamba, Serikali iliruhusu matumizi ya pikipiki kwa nia njema
ya kupunguza matatizo ya usafiri hususan maeneo ya Vijijini. Hata hivyo,
fursa hiyo imeambatana na changamoto ya ajali nyingi barabarani. Hivyo
ni wajibu wa madereva wote kuzingatia sheria za barabarani na kukidhi
vigezo vyote vya kuwa na vibali halali vya kufanya biashara hizo pamoja
na leseni za udereva. SUMATRA, Jeshi la Polisi, Mamlaka za Serikali za
Mitaa, na Mamlaka nyingine zinazohusika zinatakiwa kukaa pamoja ili
kuweka mkakati wa kukabiliana na ajali hizo ikiwa ni pamoja na
kuhakikisha kwamba Kanuni za Leseni za Usafirishaji wa Pikipiki na
Bajaji za mwaka 2010zinatekelezwa ipasavyo.
Hali ya Mipaka ya Nchi
12. Mheshimiwa Spika,
Serikali imeendelea kuliwezesha Jeshi la Wananchi wa Tanzania kutimiza
majukumu yake ya kulinda mipaka ya nchi yetu na raia wake. Katika mwaka
2013/2014, Serikali imewezesha Wanajeshi wetu kupata mafunzo mbalimbali
katika vyuo vya ndani na nje ya Nchi pamoja na kushiriki katika mazoezi
ya ushirikiano kikanda. Aidha, Jeshi limeshiriki katika operesheni
mbalimbali za kulinda amani zinazoongozwa na Umoja wa Mataifa huko
Darfur (Sudan), Lebanon, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Sudan
Kusini. Nafurahi kulieleza Bunge lako Tukufu kuwa Jeshi limefanya kazi
kubwa, nzuri na kwa weledi mkubwa, nidhamu na kujituma hivyo kuendelea
kuipatia heshima kubwa Nchi yetu. Katika jitihada za kuwapatia Askari
mazingira mazuri ya kuishi, Serikali imeanza kutekeleza Awamu ya Kwanza
ya mradi wa ujenzi wa nyumba za Askari ambapo ujenzi wa majengo 191 kati
ya 6,064 unaendelea katika vikosi mbalimbali vya Jeshi Nchini.
Mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa
13. Mheshimiwa Spika,
mwaka 2013/2014 ni wa tatu tangu Serikali iliporejesha utaratibu wa
kuwachukua Vijana wanaohitimu kidato cha sita kujiunga na mafunzo ya
Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kwa Mujibu wa Sheria. Hadi kufikia mwezi
Desemba 2013, jumla ya Vijana 15,167 wamehitimu mafunzo ya JKT wakiwemo
baadhi ya Waheshimiwa Wabunge wa Bunge hili Tukufu. Mafunzo hayo
yamewapatia vijana hao fursa ya kujifunza juu ya Ulinzi, Usalama na
Ukakamavu, Uzalishaji mali, Uzalendo na Umoja wa Kitaifa. Katika mwaka
2014/2015, Serikali itachukua vijana zaidi kujiunga na JKT kwa Mujibu wa
Sheria.
SHUGHULI ZA UCHAGUZI, BUNGE, MUUNGANO, MABADILIKO YA KATIBA NA VITAMBULISHO VYA TAIFA
Tume ya Taifa ya Uchaguzi
14. Mheshimiwa Spika,
katika mwaka 2013/2014, Tume ya Taifa ya Uchaguzi ilisimamia na
kuendesha chaguzi ndogo za Wabunge katika Majimbo matatu na Udiwani
katika Kata 53 nchini. Chaguzi hizo zimefanyika kutokana na sababu
mbalimbali zikiwemo vifo na baadhi ya Waheshimiwa Madiwani kukosa sifa
za kuendelea na nyadhifa hizo. Katika Uchaguzi wa Ubunge uliofanyika
katika Jimbo la Chambani - Zanzibar, CUF ilishinda kwa kupata Asilimia
84 ya kura zote. CCM ilipata kura Asilimia 12.4, ADC ilipata kura
Asilimia 3.5 na CHADEMA ilipata Asilimia 0.4 ya kura zote. Katika Jimbo
la Kalenga – Iringa, CCM ilishinda kwa kupata Asilimia 79.3 ya kura,
CHADEMA ilipata kura Asilimia 20.2 na CHAUSTA ilipata kura Asilimia 0.5.
Katika Jimbo la Chalinze – Pwani, CCM ilishinda kwa kupata Asilimia
86.61, CHADEMA ilipata kura Asilimia 10.58, CUF ilipata kura Asilimia
1.98, AFP ilipata kura Asilimia 0.59 na NRA ilipata Asilimia 0.25 ya
kura zote. Aidha, katika Chaguzi za Madiwani zilizofanyika katika Kata
53, CCM ilishinda viti 40, CHADEMA viti 12 na NCCR – Mageuzi kiti kimoja
(1).
15. Mheshimiwa Spika,
Tume ya Taifa ya Uchaguzi inaendelea na maandalizi ya kupata vifaa vya
kisasa kwa ajili ya zoezi la kuboresha Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.
Katika awamu hii ya uboreshaji wa Daftari, Mfumo wa Biometric Voter
Registration utatumika tofauti na Mfumo wa awali wa Optical Mark
Recognition ambao ulikabiliwa na changamoto nyingi za utendaji. Mfumo
huu wa kisasa unawezesha uandikishaji na uchukuaji wa alama za vidole
kwa haraka zaidi na hatimaye mwananchi kupatiwa kitambulisho cha kupiga
kura kwa muda mfupi. Hii itasaidia sana kuokoa muda na kupata takwimu
sahihi za wapiga kura watakaoshiriki kwenye chaguzi.
16. Mheshimiwa Spika,
nitumie fursa hii kuwaomba Viongozi wa Vyama vya Siasa kuhamasisha
Wanachama na Watanzania wote wenye sifa kujiandikisha kwenye Daftari
hilo na kupata kitambulisho halali cha mpiga kura pale zoezi hilo
litakapoanza rasmi. Aidha, ninatoa wito kwa Wananchi wote wenye sifa
kujitokeza kujiandikisha. Ni imani yangu kwamba tukitumia fursa hii
kikamilifu tutaondoa malalamiko ya majina ya baadhi ya wapiga kura
kutokuwepo kwenye orodha wakati wa chaguzi. Ni muhimu tukumbuke kwamba
ni wananchi wenye sifa tu ndiyo watakaoandikishwa. Katika mwaka
2014/2015, Tume itakamilisha zoezi la kuboresha Daftari la Kudumu la
Wapiga Kura, kusimamia Kura ya maoni kwa ajili ya Katiba Mpya, na
kuendelea kutoa elimu ya Mpiga Kura kwa Wananchi.
Bunge
17. Mheshimiwa Spika, kuanzia
mwezi Julai, 2013 hadi Aprili 2014, Ofisi ya Bunge imeendesha Mikutano
Mitatu ya Bunge na Mikutano mitatu ya Kamati za Bunge. Maswali ya Msingi
410 pamoja na maswali 73 ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu yaliulizwa na
Waheshimiwa Wabunge na kujibiwa. Aidha, Miswada minane (8) ya Sheria
ilipitishwa na Bunge. Pia, Bunge limekamilisha ukarabati wa Ukumbi wa
Bunge na Miundombinu yake kuwezesha Mkutano wa Bunge la Katiba kufanyika
na ujenzi wa Ofisi za Wabunge Majimboni umeendelea kufanyika. Vilevile,
Ofisi ya Bunge imewajengea uwezo Wabunge na Watumishi wake kupitia
semina mbalimbali katika masuala ya Utawala Bora. Katika mwaka
2014/2015, Ofisi ya Bunge itaendelea kuratibu Mikutano ya Bunge, Vikao
vya Kamati za Kudumu za Bunge pamoja na kuimarisha miundombinu na
majengo ya Bunge.
Muungano
18. Mheshimiwa Spika,
tarehe 26 Aprili 2014, tumeadhimisha Miaka 50 ya Muungano wa Tanganyika
na Zanzibar. Miaka 50 kwa lugha yoyote ile siyo kipindi kifupi.
Tumeweza kufika hapa tulipo kutokana na misingi imara ya Muungano
iliyowekwa na Waasisi wetu na kuendelezwa na Viongozi walioongoza Taifa
letu katika awamu zilizofuatia. Tunajivunia kwamba Muungano wa Tanzania
umejengeka kwenye historia ya muda mrefu ya ushirikiano wa watu wa pande
hizi mbili. Jamii hizi zina uhusiano wa damu, kifikra na mapambano ya
pamoja dhidi ya wakoloni waliotawala kwa vipindi tofauti. Walichofanya
waasisi wetu mwaka 1964 ni kurasimisha ushirikiano wetu wa muda mrefu.
Nichukue fursa hii kuwashukuru na kuwapongeza Watanzania wote kwa
kuadhimisha Miaka 50 ya Muungano. Aidha, ninawashukuru kwa dhati
Viongozi wote walioongoza Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Zanzibar
tangu kuasisiwa kwa Muungano. Kwa namna ya pekee namshukuru Mheshimiwa
Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na
Mheshimiwa Dkt. Ali Mohammed Shein, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa
Baraza la Mapinduzi kwa Uongozi wao ambao umezifanya pande mbili za
Muungano kuwa karibu zaidi.
19. Mheshimiwa Spika,
tumeadhimisha Miaka 50 ya Muungano tukiwa na takwimu za Sensa ya Watu
na Makazi ya Mwaka 2012. Takwimu hizo zinaweka jambo moja wazi kwa
Muungano wetu; kwamba zaidi ya asilimia 90 ya Watanzania wote
wamezaliwa baada ya Muungano. Hivyo, tuliozaliwa kabla ya Muungano ni
chini ya asilimia kumi. Kwa mujibu wa takwimu hizo, Tanzania nzima ina
watu 44,926,923. Kati yao, watu 40,640,425, sawa na Asilimia 90.6 ni wa
umri wa siku moja hadi miaka 50. Kwa upande wa Tanzania Bara, idadi
ya watu ilikuwa 43,625,354, kati ya hao, watu 39,456,065 sawa na
asilimia 90.5 wamezaliwa baada ya Muungano. Kwa upande wa Zanzibar
kulikuwa na watu 1,303,569, ambapo watu 1,184,360 sawa na asilimia 90.9
wamezaliwa baada ya Muungano. Takwimu hizo zina maana kwamba, asilimia
90.6 ya watu wote wamezaliwa ndani ya Muungano na nchi wanayoifahamu ni
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Sote tunawajibika kuwatendea haki watu
hawa kwa kuulinda, kuuimarisha na kuudumisha Muungano wetu.
20. Mheshimiwa Spika, tuna
kila sababu ya kuadhimisha Miaka hii 50 ya Muungano kwa furaha. Katika
maadhimisho ya mwaka huu, tuliandaa maonesho maalum, makongamano na
shughuli nyingine ambazo zilisaidia wananchi kuelimishwa kuhusu masuala
ya Muungano. Aidha, kimeandaliwa kitabu maalum kinachoelezea historia,
utekelezaji wa mambo ya Muungano, mafanikio, changamoto, fursa na
matarajio ya Muungano kwa miaka ijayo. Kitabu hicho kitatumika kama
rejea kwa kizazi chetu na vizazi vijavyo.
21. Mheshimiwa Spika, tutaendelea
kuulinda Muungano wetu kwa nguvu zote tukiwa na uelewa kwamba, katika
kipindi cha miaka 50 iliyopita Watanzania wameishi kwa amani na kufanya
kazi zao za kujiletea maendeleo wakiwa upande wowote wa Muungano.
Tunatambua changamoto zilizopo na tumeweka utaratibu mzuri wa vikao ili
kuzitafutia ufumbuzi changamoto hizo. Vikao hivyo vitaendelea kufanyika
katika ngazi ya wataalam, Watendaji Wakuu na Viongozi wa Kitaifa. Ni
imani yangu kwamba, Muungano huu utaendelea kudumu na watu watapata
maendeleo makubwa kwani Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ina fursa nyingi
zinazoweza kutumika kwa manufaa ya wote. Sote tukumbuke kuwa, UTANZANIA WETU NI MUUNGANO WETU, TUULINDE, TUUIMARISHE NA KUUDUMISHA!
Mabadiliko ya Katiba
22. Mheshimiwa Spika, tarehe
30 Desemba 2013, Tume ya Mabadiliko ya Katiba ilikamilisha Rasimu ya
Pili ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kuikabidhi kwa
Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi. Napenda kuishukuru Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyokuwa ikiongozwa na Mheshimiwa Jaji Joseph Sinde Warioba kwa kuandaa Rasimu ya Katiba Mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Rasimu hiyo imeliwezesha
Bunge Maalum la Katiba kuanza mjadala. Nitumie fursa hii kuwashukuru
Watanzania wote kwa kutoa maoni yaliyowezesha Tume kuandaa Rasimu hiyo
ya Katiba.
23. Mheshimiwa Spika, Bunge
Maalum la Katiba linaundwa na Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania, Wabunge wa Baraza la Wawakilishi na Wajumbe 201
walioteuliwa kwa mujibu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya mwaka 2011.
Naomba nitumie fursa hii kuwapongeza Wajumbe wote wa Bunge Maalum la
Katiba kwa kupata fursa hii ya kuwawakilisha Watanzania katika kuandaa
Katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Ni dhahiri kuwa dhamana
hii ni kubwa sana!
24. Mheshimiwa Spika, Bunge
Maalum la Katiba lilianza kazi rasmi tarehe 18 Februari, 2014 kwa
kumchagua Mheshimiwa Pandu Ameir Kificho kuwa Mwenyekiti wa muda wa
Bunge hilo. Nichukue fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Pandu Ameir Kificho
kwa kazi nzuri aliyoifanya ya kulisimamia Bunge Maalum hadi kuwezesha
kupatikana kwa Kanuni za kuliongoza Bunge hilo. Aidha, niwapongeze
Mheshimiwa Samwel John Sitta kwa kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti na
Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kuwa Makamu Mwenyekiti wa Bunge Maalum la
Katiba. Nampongeza Katibu wa Bunge la Katiba Bwana Yahaya Hamadi Khamis
na Naibu wake Dkt. Thomas Kashililah pamoja na Wajumbe wote
waliochaguliwa kuwa Wenyeviti na Makamu Wenyeviti wa Kamati 12 za Bunge
Maalum. Baada ya kukutana kwa muda wa siku 67, Bunge Maalum limeahirisha
Mkutano wake tarehe 25 Aprili, 2014 ili kupisha majadiliano ya Mpango
na Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2014/2015. Ni matumaini yangu kwamba,
Bunge Maalum la Katiba litakaporejea litakamilisha kazi hiyo kwa umakini
na kupata Rasimu ambayo hatimaye itapelekwa kwa wananchi kwa ajili ya
kura ya maoni.
Vitambulisho vya Taifa
25. Mheshimiwa Spika, katika
hotuba yangu ya Bajeti ya mwaka 2013/2014 nilielezea dhamira ya
Serikali ya kutoa Vitambulisho vya Taifa kwa Wananchi wake. Napenda
kuliarifu Bunge lako Tukufu kwamba, Serikali imekamilisha usajili na
utambuzi wa watu kwa upande wa Zanzibar, Watumishi wa Umma na vyombo vya
Ulinzi na Usalama pamoja na wakazi wa Mkoa wa Dar es Salaam. Serikali
pia, imekamilisha ujenzi wa vituo vya kuingiza na kuhakiki taarifa,
kituo cha kutengeneza Vitambulisho na kuhifadhi kumbukumbu pamoja na
kituo cha uokozi na majanga ya taarifa na takwimu. Katika mwaka
2014/2015, Serikali itaendelea na zoezi la Utambuzi na Usajili wa
Watanzania katika Mikoa mingine ili kwa pamoja tuweze kunufaika na
Vitambulisho vya Taifa katika nyanja za kijamii, kiuchumi na kiusalama.
Sensa ya Watu na Makazi
26. Mheshimiwa Spika,
katika mwaka 2013/2014, Serikali imeendelea kutoa machapisho mbalimbali
ya matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012. Machapisho hayo
yanajumuisha Taarifa ya Mgawanyo wa Watu kwa Maeneo ya Utawala; Mgawanyo
wa Watu kwa Umri na Jinsia na Taarifa za Msingi za Kidemografia,
Kijamii na Kiuchumi. Taarifa hizo zimebaini kuwa, katika miaka kumi
iliyopita kumetokea mabadiliko makubwa ya kiuchumi na kijamii katika
nchi yetu. Kiwango cha watu wanaojua kusoma na kuandika kimeongezeka
kutoka asilimia 69 mwaka 2002 hadi asilimia 78 mwaka 2012. Aidha,
uandikishaji halisi katika shule za msingi umeongezeka kutoka asilimia
69 mwaka 2002 hadi 77 mwaka 2012. Idadi ya watu wanaoishi kwenye nyumba
zenye kuta imara ni asilimia 74 na asilimia 65.4 wanaishi kwenye nyumba
zilizoezekwa kwa bati. Hata hivyo, pamoja na mafanikio hayo,
hali ya utegemezi nchini
ni kubwa kutokana na ukweli kuwa kati ya Watanzania Milioni 44.9,
Asilimia 50.1 ni watoto wenye umri chini ya miaka 18. Aidha, takwimu
zimebainisha kuwa Asilimia 7.7 ya Watanzania ni watoto yatima. Kutokana
na hali hiyo, ni jukumu letu kama Taifa kuweka mipango madhubuti ya
kukabiliana na changamoto hizo katika sekta za huduma za jamii ili
hatimaye kila mwenye uwezo wa kufanya kazi achangie ipasavyo katika
kukuza uchumi na maendeleo ya nchi yetu.
MASUALA YA UCHUMI
Hali ya Uchumi
27. Mheshimiwa Spika,
Pato la Taifa katika mwaka 2013 lilikua kwa Asilimia 7.0 ikilinganishwa
na ukuaji wa Asilimia 6.9 mwaka 2012. Ongezeko hilo limetokana na
ukuaji mzuri wa shughuli za huduma za mawasiliano, viwanda, ujenzi na
huduma za fedha. Kutokana na ongezeko hilo, wastani wa Pato la Mtanzania
limeongezeka kutoka Shilingi 1,025,038 mwaka 2012 hadi Shilingi
1,186,424 mwaka 2013, sawa na ongezeko la Asilimia 15.7. Mfumuko wa Bei
umepungua kutoka Asilimia 9.8 Machi 2013 hadi Asilimia 6.1 Machi 2014.
Kupungua kwa mfumuko wa bei kumechangiwa na kupungua kwa kasi ya kupanda
bei za bidhaa na vyakula hasa mahindi, mchele na aina nyingine ya
nafaka.
28. Mheshimiwa Spika,
pamoja na uchumi wetu kukua kwa kasi ya asilimia 7.0 kwa mwaka 2013 na
Pato la Mtanzania kuongezeka, kiwango hicho siyo kikubwa sana kuwezesha
umaskini wa wananchi kupungua kwa kasi. Utafiti wa kitaalam unaonesha
kwamba, ili umaskini upungue kwa kasi kubwa, uchumi unatakiwa kukua kwa
zaidi ya Asilimia 8 kwa kipindi cha miaka 10 mfululizo. Ukuaji huo pia
unatakiwa kulenga Sekta ambazo zinagusa maisha ya watu wengi, hususan
kilimo, mifugo na uvuvi. Mwelekeo wa Serikali ni kuweka mazingira
wezeshi kwa Sekta za kipaumbele kukua kwa kushirikisha Sekta Binafsi.
Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano
29. Mheshimiwa Spika, Serikali
inatekeleza Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano 2011/2012 – 2015/2016
ambao unatekelezwa katika kipindi cha mwaka mmoja mmoja. Katika mwaka
2013/2014, Serikali ilitekeleza Mpango huo kupitia Kauli mbiu ya
Tekeleza Sasa kwa Matokeo Makubwa. Msingi wa kauli mbiu
hii ni kuainisha maeneo machache ya kimkakati na kuyatengea
rasilimali za kutosha, kusimamia na kufuatilia utekelezaji kwa karibu
zaidi. Chombo maalum cha Ufuatiliaji wa Utekelezaji wa Miradi ya
kimkakati chini ya Ofisi ya Rais kinachojulikana kama President’s Delivery Bureau –
(PDB) kimeanzishwa na Watendaji Wakuu wameteuliwa. Ninapenda kuliarifu
Bunge lako Tukufu kwamba, matunda ya utekelezaji wa Mfumo huo yameanza
kuonekana katika maeneo makuu sita ya kipaumbele kitaifa ambayo ni
Nishati ya Umeme, Uchukuzi, Kilimo, Elimu, Maji na Ukusanyaji wa
Mapato. Utekelezaji wa miradi hiyo na mafanikio yaliyoanza kupatikana
yatatolewa maelezo na Mawaziri katika Sekta husika.
Maendeleo ya Sekta Binafsi na Uwekezaji
30. Mheshimiwa Spika, njia
ya uhakika ya kuliwezesha Taifa kuwa na uchumi imara na wa kisasa
utakaohimili ushindani katika masoko ya Kikanda na Kimataifa ni kuweka
mazingira wezeshi ya uwekezaji. Katika kufikia azma hiyo, tarehe 31
Januari, 2014 nilizindua rasmi Taarifa ya Tathmini ya Sera, Sheria na
Kanuni mbalimbali zinazosimamia Uwekezaji Tanzania. Mapendekezo ya
Taarifa hiyo yatatumika kuihuisha Sera ya Taifa ya Uwekezaji ya mwaka
1996 pamoja na Sheria ya Uwekezaji Tanzania ya mwaka 1997. Aidha, ili
kuwawezesha Wawekezaji na Wafanyabiashara kupata huduma na taarifa zote
muhimu kama vile Sheria, Kanuni na Taratibu mbalimbali kuhusu biashara
na uwekezaji kwa njia ya mtandao, Serikali imezindua upya Tovuti ya
Kituo cha Uwekezaji Tanzania. Kupitia Tovuti hii, Wawekezaji popote
duniani wanaweza kupata taarifa kuhusu usajili wa Kampuni na
viwango vya kodi kwa njia ya mtandao.
Dhamira ya Serikali ni
kuboresha mazingira ya uwekezaji na kupunguza gharama za kufanya
biashara nchini ili kukabiliana na ushindani mkubwa kutoka nchi nyingine
zilizotekeleza maboresho ya mifumo yao ya udhibiti wa biashara.
31. Mheshimiwa Spika,
Sekta Binafsi inaendelea kupewa nafasi kubwa katika kukuza uchumi
Nchini. Takwimu zinaonesha kwamba, Miradi iliyosajiliwa na Kituo cha
Uwekezaji Tanzania imeongezeka kutoka 869 yenye thamani ya Shilingi
Bilioni 31.5 mwaka 2012 hadi miradi 885 yenye thamani ya Shilingi
Bilioni 141.2 mwaka 2013.
Napenda pia kuliarifu
Bunge lako Tukufu kwamba Nchi nyingi duniani zinaendelea kuiamini
Tanzania kama Kituo maarufu cha uwekezaji Duniani. Mwezi Novemba, 2011
nilizindua Mpango wa Ushirikiano kati ya Tanzania na Uingereza
unaojulikana kama Partnership in Prosperity. Mpango huo umelenga
kuongeza uwekezaji kutoka Sekta Binafsi ya Uingereza kwenye mafuta na
gesi, kilimo na Nishati jadidifu. Lengo ni kuongeza uwekezaji kutoka
Nchi hiyo kwa zaidi ya maradufu ya kiwango cha sasa. Aidha,
tumekubaliana kushirikiana kuimarisha mazingira ya biashara ili
kurahisisha uwekezaji katika sekta hizo.
32. Mheshimiwa Spika, baadhi
ya Kampuni za Uingereza tayari zimeanza kutekeleza makubaliano hayo
kwenye Sekta ya kilimo. Kampuni ya Unilever kwa mfano, itawekeza zaidi
ya Shilingi Bilioni 275 kwenye kilimo cha chai kwa kushirikiana na
wakulima wadogo. Tayari Kampuni hiyo imeanza kupanua Kiwanda cha Chai
Kibwele, Mufindi na kufungua zaidi ya Hekta 300 za mashamba ya chai
katika Wilaya ya Mufindi. Aidha, Kampuni hiyo imeingiza nchini vipando
250,000 vya miche bora ya chai. Pia, Kampuni inaandaa zaidi ya miche
milioni 2 kwa ajili ya kuwagawia wakulima wadogo Wilayani Njombe ili
waongeze uzalishaji wa chai Nchini.
33. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/2014, Kituo
cha Uwekezaji kimeshirikiana na Uongozi wa Mikoa mbalimbali Nchini
kuratibu maandalizi ya Makongamano ya Uwekezaji yenye lengo la
kuhamasisha, kukuza na kutangaza fursa mbalimbali za uwekezaji zilizopo
kwenye Mikoa hiyo. Jumla ya Mikoa 11 imeshiriki kikamilifu kuandaa na
kufanikisha Makongamano ya Uwekezaji katika maeneo yao. Mikoa hiyo
ni Mwanza, Mara, Kagera, Geita, Simiyu, Shinyanga, Tabora, Manyara,
Tanga, Kilimanjaro na Arusha. Makongamano hayo yamechangia kwa kiasi
kikubwa kuzitangaza fursa za uwekezaji zilizopo kwenye Mikoa hiyo,
pamoja na kuihamasisha Mikoa na Halmashauri za Wilaya ndani ya Mikoa
hiyo kuainisha na kutenga maeneo kwa ajili ya uwekezaji. Aidha,
Wawekezaji wengi walioshiriki kwenye Makongamano hayo wameonesha nia na
utayari wa kuwekeza kwenye Mikoa husika. Jitihada hizi zitaendelezwa
katika kipindi kijacho.
Majadiliano na Sekta Binafsi
34. Mheshimiwa Spika, kwenye
hotuba yangu ya Bajeti mwaka 2013/2014, nilieleza kuhusu Mkutano wa
Kimataifa wa Majadiliano ya Ushirikiano kwa Manufaa ya Wote. Mkutano huo
ulifanyika kuanzia tarehe 28 Juni hadi tarehe 1 Julai 2013, Jijini Dar
es Salaam chini ya Uenyekiti wa Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete,
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mkutano huo ulitoa fursa ya
kipekee kwa Viongozi wa Serikali kujadiliana na kupata maoni ya makundi
mbalimbali ya Wananchi kuhusu mbinu za kuongeza kasi ya maendeleo ya
kiuchumi na kijamii. Serikali imedhamiria kufanya Majadiliano ya
Ushirikiano kwa Manufaa ya Wote kila mwaka kuanzia ngazi ya Wilaya, Mkoa
hadi Taifa kwa kuzingatia fursa kubwa za maendeleo shirikishi zilizopo
kwenye maeneo husika.
35. Mheshimiwa Spika, Baraza
la Taifa la Biashara lilifanya Mkutano wake wa Saba tarehe 16 Desemba
2013 chini ya Kauli Mbiu ya “Ukuaji Shirikishi wa Uchumi”. Maazimio ya
Mkutano huo ni pamoja na kuunda Kamati Tatu ambazo zitashughulikia
Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi, Mazingira Wezeshi ya Biashara na Matumizi
Endelevu ya Maliasili za nchi. Kamati ya Mazingira Wezeshi ya Biashara
imeanza kuishauri Serikali kuhusu mikakati ya kuwavutia wawekezaji wa
ndani na nje na kuongeza ushindani wa bidhaa za Tanzania. Kazi hiyo
imefanyika kwa utaratibu wa Maabara chini ya Mfumo wa Tekeleza Sasa kwa
Matokeo Makubwa. Utaratibu huo ulianzisha maeneo sita muhimu ambayo
yakishughulikiwa yataboresha mazingira ya biashara nchini. Maeneo hayo
ni kuboresha Kanuni na Taasisi zinazosimamia biashara; upatikanaji wa
ardhi na haki za umiliki wake na kuimarisha ukusanyaji wa kodi na kupunguza wingi wa kodi na tozo mbalimbali. Maeneo
mengine ni kuzuia na kupambana na rushwa; kuboresha Sheria za Kazi na
kuimarisha mafunzo na stadi za kazi pamoja na kusimamia utekelezaji wa
mikataba na utawala wa sheria. Katika mwaka 2014/2015, Baraza la Taifa la Biashara litaendelea kuratibu utekelezaji wa maazimio hayo ya Mkutano wa Saba sanjari na kusimamia mikutano ya Mabaraza ya Wilaya na Mikoa.
UWEZESHAJI WANANCHI KIUCHUMI
36. Mheshimiwa Spika, dhamira
ya Serikali ya kubuni na kutekeleza Sera ya Uwezeshaji Wananchi
Kiuchumi ya mwaka 2004 ni kuhakikisha kwamba Watanzania wananufaika na
rasilimali za nchi yao badala ya kubaki kuwa watazamaji. Kwa kutambua umuhimu wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi, katika Mwaka 2013/2014 Serikali imeanzisha Taasisi ya Ujasiriamali na Ushindani wa Kibiashara (Tanzania Entrepreneurship Competitiveness Centre).
Taasisi hiyo itatekeleza jukumu la kutoa miongozo ya uandaaji wa
mitaala ya ujasiriamali katika ngazi tofauti na kuhamasisha uzalishaji
wa bidhaa bora zitakazohimili ushindani. Aidha, Serikali imeendelea
kusimamia Mifuko ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi na kuongeza ufanisi
wake. Hadi kufikia mwezi Februari 2013, Mfuko wa Uwezeshaji wa Mwananchi
ulikuwa umepokea Shilingi Bilioni 2.1 zilizotumika kudhamini mikopo ya
wajasiriamali kupitia Benki ya CRDB kwa makubaliano ya kukopesha mara
tatu ya dhamana ya Serikali. Kutokana na makubaliano hayo, hadi kufikia
mwezi Desemba 2013, mikopo yenye thamani ya zaidi ya Shillingi Bilioni
9.5 ilikuwa imetolewa kwa Wajasiriamali 9,790 waliojiunga kwenye Vikundi
283 na Vyama vya Akiba na Mikopo (SACCOS) 51 katika Mikoa 12 na Wilaya
27.
37. Mheshimiwa Spika, Kwa
upande wa Mfuko wa Kuendeleza Wajasiriamali Wadogo na wa Kati, hadi
kufikia Desemba 2013, ulikuwa umetoa mikopo yenye thamani ya
Shilingi Bilioni 36.39 kwa Wajasiriamali 62,720. Aidha, Mfuko wa
Maendeleo ya Vijana ulikuwa umetoa mikopo kwa Vijana yenye thamani
ya Shilingi Bilioni 1.22 kupitia SACCOS 244; na Mfuko wa Maendeleo
ya Wanawake ulikuwa umetoa mikopo yenye thamani ya Shilingi
Bilioni 5.44 kwa Wanawake 500,000 Nchini. Vilevile, Mradi wa
Mikopo kwa Wajasiriamali Wadogo (SELF) ulikuwa umetoa mikopo yenye
thamani ya Shilingi Bilioni 57.1 kupitia Asasi 375 za Kifedha ambapo
Wajasiriamali 95,034 walinufaika.
Mfuko wa Maendeleo ya Jamii – TASAF
38. Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Awamu ya Tatu ya Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF III) inatekeleza Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini zilizo katika Mazingira Hatarishi Tanzania Bara na Zanzibar. Katika
kutekeleza Mpango huo, utaratibu wa uhawilishaji fedha kwa kaya maskini
ulifanyika katika Mamlaka za Serikali za Mitaa 22 ambapo kaya 138,032
katika Vijiji na Shehia 1,179 zilitambuliwa na kuandikishwa katika Mfumo
wa Masijala wenye walengwa 464,552. Hadi sasa, Shilingi Bilioni 5.5
zimehawilishwa katika kaya hizo. Lengo ni kuziwezesha kaya hizo kupata chakula na kujiongezea fursa ya kipato.
39. Mheshimiwa Spika, Serikali
pia imejenga uwezo kwa Viongozi na Wataalam kutoka maeneo ya
utekelezaji wa Mpango huo. Uwezo umejengwa kwa kutoa mafunzo katika
masuala ya utambuzi, uandikishaji na ukusanyaji taarifa za kaya maskini.
Aidha, mafunzo ya usanifu wa miradi ya ujenzi yalitolewa kwa wataalam
kutoka Mamlaka za Serikali za Mitaa. Pia, Wajumbe 17 wa Baraza la
Wawakilishi na Wakuu wa Mikoa na Wilaya kutoka Zanzibar walitembelea
Vijiji vya Pongwe-Kiona na Malivundo (Bagamoyo) na Gwata (Kibaha) ili
kujifunza kuhusu utekelezaji bora wa Mpango huo. Katika mwaka 2014/2015,
Serikali itaendelea kufanya utambuzi na uandikishaji wa kaya maskini
kufikia maeneo yote 161 ya utekelezaji wa Mpango Tanzania Bara na
Zanzibar. Lengo ni kutambua na kuandikisha Kaya 920,000 kutoka Vijiji,
Mitaa na Shehia 9,000.
UZALISHAJI MALI
Uzalishaji wa Mazao
40. Mheshimiwa Spika, hali ya upatikanaji wa chakula ni ya kuridhisha katika maeneo mengi nchini kufuatia mavuno mazuri ya msimu wa 2012/2013. Uzalishaji
wa mazao ya chakula kwa msimu huo ulikuwa Tani Milioni 14.38
ikilinganishwa na mahitaji ya chakula ya Tani 12.15 kwa mwaka 2013/2014
ikiwa ni ziada ya Tani Milioni 2.3 za chakula. Ongezeko hilo limefanya
Taifa kujitosheleza kwa chakula kwa Asilimia 118 na hivyo, kufanya wastani wa bei za mazao ya chakula katika masoko Nchini kuwa za chini katika kipindi chote cha mwaka 2013/2014.
Ruzuku ya Pembejeo za Kilimo
41. Mheshimiwa Spika,
Serikali imeendelea na juhudi za kuongeza tija katika uzalishaji wa
mazao ya chakula na biashara kulingana na Mipango inayotekelezwa chini
ya Kaulimbiu ya KILIMO KWANZA, na Mpango wa Tekeleza kwa Matokeo Makubwa
Sasa. Katika mwaka 2013/2014, Serikali imesambaza jumla ya vocha za
ruzuku 2,796,300 zenye thamani ya Shilingi Bilioni 83 kwa ajili ya
mbolea na mbegu bora za mpunga na mahindi kwa Kaya 932,100. Pia,
Serikali ilitoa ruzuku ya dawa za korosho kiasi cha lita 158,845 na Tani
620 zenye thamani ya Shilingi Bilioni 1.5. Vilevile, ruzuku ilitolewa
kwa ajili ya uzalishaji wa mbegu bora za pamba Tani 4,000 zenye thamani
ya Shilingi Bilioni 4.8, miche ya kahawa 350,000 yenye thamani ya
Shilingi Milioni 100 na miche ya chai 1,850,000 yenye thamani ya
Shilingi Milioni 300.
42. Mheshimiwa Spika,
ongezeko la tija katika uzalishaji wa mazao unategemea sana huduma bora
za ugani kwa wakulima. Serikali katika mwaka 2013/2014, ilitoa kibali
cha kuajiri Maafisa Ugani 1,452 ili kufanikisha kufikiwa kwa malengo ya kuwa na Afisa Ugani wa Kilimo mmoja kwa kila kijiji. Vilevile, Serikali imeongezaMashamba Darasa kutoka 16,330 yenye wakulima 344,986 mwaka 2012/13 hadi 16,543 yenye wakulima 345,106 mwaka 2013/2014 ili kuimarisha utoaji wa mafunzo kwa wakulima.
43. Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kushirikisha Washirika wa Maendeleo kuchangia Programu ya Kuendeleza Kilimo katika Ukanda wa Kusini mwa Tanzania (SAGCOT). Miongoni mwa malengo ya Programu hiyo ni kuwaunganisha
wakulima wadogo na mnyororo wa thamani wa kibiashara wa Makampuni
makubwa ya ndani na nje ya nchi. Ili kufikia lengo hilo, Serikali
imeanzisha Mfuko Chochezi wa Uendelezaji wa Kilimo katika Ukanda wa
Kusini mwa Tanzania (SAGCOT Catalytic Trust Fund). Mfuko huo utatoa
mitaji itakayogharamia hatua za awali za miradi inayotoa tija ya haraka
ambayo imebainishwa kwenye Mpango Mkakati wa Uwekezaji. Vilevile, Mfuko
huo utahamasisha biashara inayolenga kumuinua Mkulima mdogo kwa
kumuunganisha na mnyororo wa thamani na kampuni kubwa kupitia madirisha
makuu mawili. Dirisha la kwanza ni Matching Grant Fund linalolenga
kuwezesha kampuni kubwa zilizoanzisha biashara ya Kilimo Nchini,
kuimarisha minyororo ya thamani inayowahusisha wakulima wadogo zaidi au
kuanzisha kilimo cha Mkataba kati ya wakulima wakubwa na wakulima
wadogo. Dirisha la pili ni Social Venture Capital Fund, linalolenga
kuziwezesha biashara changa na za kati kwenye Sekta ya Kilimo au
kuwezesha Kilimo cha mkataba kati ya wakulima wakubwa na wakulima
wadogo. Tayari Bodi ya Mfuko imeteuliwa na Mtendaji Mkuu wa Mfuko
ameajiriwa.
44. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2014/2015, Serikali
kupitia Mfumo wa Tekeleza Sasa kwa Matokeo Makubwa, inategemea kuvutia
uwekezaji na kuanzisha Kilimo cha mashamba makubwa 25 ya Kilimo cha
kibiashara kwa mazao ya mpunga na miwa kwa utaratibu wa kuwaunganisha
wakulima wakubwa na wadogo wanaozunguka mashamba hayo. Aidha,
itaanzisha, itaboresha na kuendesha kitaalamu maghala 275 ya kuhifadhi
mahindi kwa kuwaunganisha wakulima katika umoja wa kibiashara kwa ajili
ya kupata masoko ya pamoja.
Umwagiliaji
45. Mheshimiwa Spika,
katika juhudi za kuendeleza Kilimo cha umwagiliaji Nchini, Sheria ya
Umwagiliaji Namba 5 ya mwaka 2013 imeanza kutumika Mwezi Januari, 2014.
Sheria hiyo itaiwezesha Serikali kuanzisha Tume ya Umwagiliaji ambayo ni
chombo cha kitaifa chenye dhamana ya kusimamia, kuendeleza na kudhibiti
shughuli za Umwagiliaji Nchini. Sheria hiyo pia itaanzisha Mfuko wa
Taifa wa Umwagiliaji utakaosaidia kutekeleza mipango ya umwagiliaji kwa
kulipia gharama za umwagiliaji zinazofanywa na mkulima mmoja mmoja na
wawekezaji kupitia mikopo na dhamana. Serikali pia iliendelea na ujenzi
na ukabarati wa skimu 24 za umwagiliaji zilizopo katika wilaya 15
Nchini. Katika mwaka 2014/2015, Serikali itaendeleza Skimu za Umwagiliaji 39 kwa ajili ya Kilimo cha mpunga.
Miundombinu ya Masoko ya Mazao
46. Mheshimiwa Spika,
katika mwaka 2013/2014, Serikali kupitia Programu ya Miundombinu ya
Masoko, Uongezaji Thamani na Huduma za Kifedha Vijijini imekarabati kilometa
352 za barabara za vijijini kwa kiwango cha changarawe katika
Halmashauri za Iringa Vijijini, Njombe Vijijini, Singida Vijijini,
Mbarali, Lushoto, Same, Mbulu, Msalala na Mpanda. Halmashauri nyingine
ni Maswa, Songea Vijijini, Rufiji, Karatu na Kwimba. Vilevile, imejenga
maghala matano yenye uwezo wa kuhifadhi tani 1,000 za mazao kila moja
katika halmashauri za Iringa Vijijini, Njombe Vijijini, Same, Songea na
Mbarali na kukarabati maghala matatu katika Halmashauri za Sumbawanga,
Mbulu na Kahama. Aidha, Programu hiyo imezijengea uwezo benki tisa za
wananchi/ushirika ili kuimarisha mfumo wa kifedha Vijijini.
47. Mheshimiwa Spika,
katika mwaka 2014/2015, Serikali kupitia Programu hiyo imepanga
kukarabati kilometa 434 za barabara kwa kiwango cha changarawe, kujenga
maghala 14 na masoko saba katika Halmashauri 64 za Tanzania Bara na Wilaya 10 za Zanzibar. Aidha, wazalishaji wadogo kutoka Mikoa 24 ya Tanzania Bara
na Mikoa mitano ya Zanzibar watajengewa uwezo wa kuhifadhi mazao na
mbinu za kufikia masoko ambapo zaidi ya wananchi 100,000 watanufaika na
mafunzo hayo.
Maendeleo ya Ushirika
48. Mheshimiwa Spika, Sheria ya Ushirika Namba 6 ya mwaka 2013 imetungwa na imeanza kutumika Mwezi Januari, 2014. Sheria hiyo itawezesha kuanzishwakwa
Tume ya Maendeleo ya Ushirika ambayo itakuwa na majukumu ya kusimamia
moja kwa moja Vyama vyote vya Ushirika. Aidha, kupitia Sheria hiyo,
Serikali imetoa Waraka Namba 1 wa mwaka 2014 unaotoa ufafanuzi kuhusu
Chaguzi katika Vyama vya Ushirika. Ili kuondoa migogoro ya kimaslahi,
Waraka huo umewaondoaViongozi wa Siasa na
Serikali katika uongozi wa Vyama vya Ushirika katika ngazi zote. Katika
mwaka 2014/2015, Serikali itaimarisha uratibu wa Vyama
vya Ushirika kulingana na mahitaji ya Wananchi na kuunganisha Vyama vya
Ushirika na Taasisi za fedha ili kuboresha utoaji wa huduma za kifedha
kwa Vyama vya Ushirika.
Maendeleo ya Sekta ya Mifugo
49. Mheshimiwa Spika,
kupitia Mpango wa Ruzuku ya dawa ya kuogeshea mifugo, Serikali ilitoa
jumla ya lita 11,020 zenye thamani ya Shilingi Milioni 181.8 na
kusambazwa nchini. Vilevile, ilitoa chanjo kwa ajili ya kudhibiti
magonjwa ya mifugo ambapo dozi 150,000 za chanjo ya Ugonjwa wa Homa ya
Bonde la Ufa zenye thamani ya Shilingi milioni 119 ilitolewa katika
Mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Manyara, Tanga na Dodoma. Vilevile,
Serikali imeimarisha Kituo cha Uhamilishaji kilichopo katika eneo la Usa
River, Arusha pamoja na Vituo vingine vitano vya Kanda kwa kusimika
mitambo ya kuzalisha kimiminika cha naitrojeni na kujenga Vituo vitano
vya madume bora. Vilevile, ng’ombe walionenepeshwa wameongezeka kutoka
132,246 mwaka 2011/2012 hadi kufikia 175,000 mwaka 2013/2014. Ili
kuboresha upatikanaji wa maziwa Nchini, Serikali imeongeza uzalishaji
mitamba katika mashamba yake kutoka mitamba 943 kwa mwaka 2012/2013 hadi
mitamba 1,046 mwaka 2013/2014 na kusambaza Mbuzi wa maziwa 9,530
kupitia Mpango wa Kopa Mbuzi lipa Mbuzi. Jitihada hizi, zimesaidia
wafugaji kuongeza tija na hivyo kuchangia ongezeko la uzalishaji wa
maziwa kutoka lita Bilioni 1.9 mwaka 2012/2013 hadi lita Bilioni 2 mwaka
2013/2014.
50. Mheshimiwa Spika,
katika mwaka 2014/2015, Serikali itatoa ruzuku ya dawa za kuogesha
mifugo na kununua dozi milioni moja kwa ajili ya chanjo ya ugonjwa wa
Homa ya Bonde la Ufa kwa Mikoa ya Arusha, Tanga, Tabora na baadhi ya
mikoa katika Kanda ya Ziwa. Vilevile, Serikali itaimarisha Vituo vya
uhamilishaji, mashamba ya kuzalisha mifugo bora na yale yanayozalisha
mbegu bora za mifugo pamoja na kununua mifugo wazazi.
Maendeleo ya Sekta ya Uvuvi
51. Mheshimiwa Spika, katika
mwaka 2013/2014, Serikali kwa kushirikiana na wadau ilihuisha Sera ya
Taifa ya Uvuvi ya mwaka 1997 na Sheria ya Uvuvi Namba 22 ya mwaka 2003
ili ziendane na mabadiliko ya kiuchumi, kisayansi na kiteknolojia.
Katika kuimarisha ufugaji wa samaki, wakulima 2,604 walipewa mafunzo ya
ufugaji bora wa samaki na mabwawa 64 yalichimbwa. Hatua hiyo imeongeza
idadi ya mabwawa ya Samaki kufikia 20,198 yenye uwezo wa kuzalisha Tani
3,029.7 za samaki ikilinganishwa na mabwawa 20,134 yaliyokuwepo mwaka
2012/2013. Vituo vya kuzalisha vifaranga wa samaki kwa wingi kwa
kutumia teknolojia ya ndani viliongezeka kutoka kituo kimoja mwaka 2012/2013 hadi kufikia vituo vitano mwaka
2013/2014 vyenye uwezo wa kuzalisha vifaranga bora vya samaki Milioni
10 kwa mwaka. Serikali pia, ilijenga matanki sita yenye lita za ujazo
8,000 kila kimoja kwa ajili ya kuzalisha vifaranga vya samaki.
52. Mheshimiwa Spika,
katika mwaka 2014/2015, Serikali itaanzisha Vituo vya kuzalishia
vifaranga vya samaki katika maeneo ya Bacho Dareda - Manyara, Hombolo –
Dodoma, na Kigoma. Vilevile, itajenga bwawa la kufuga samaki katika
Kituo cha Mafunzo ya Kilimo cha Kilimanjaro – KATC; na kutoa ruzuku kwa
ajili ya kuchimba mabwawa na kuzalisha vifaranga wa samaki.
Ufugaji Nyuki
53. Mheshimiwa Spika,
Sekta ya ufugaji nyuki imeendelea kuimarika na kuchangia kuongeza ajira
na kupunguza umaskini. Mwaka 2013, thamani ya mauzo ya asali nje
yalifikia Shilingi Milioni 287.3 ikilinganishwa na mauzo ya Shilingi
Milioni 262 mwaka 2012. Katika kipindi hicho, jumla ya Tani 384 za nta
zenye thamani ya Shilingi Milioni 4,660 ziliuzwa nje ikilinganishwa na
Tani 277 zenye thamani ya Shilingi Milioni 2,583 zilizouzwa mwaka 2012.
Nchi zilizoongoza katika ununuzi wa Asali na Nta ya Tanzania ni
Ujerumani, Oman, China, Japan, Yemen, India, Ubelgiji, Botswana, Kenya
na Marekani. Kutokana na maendeleo haya mazuri katika mwaka 2013/2014, Serikali imetenga maeneo 20 yenye ukubwa wa Hekta 58,445 sehemu mbalimbali Nchini kwa ajili ya hifadhi za nyuki. Aidha, imetoa mafunzo kwawafugaji
nyuki 924 na vikundi 49 kutoka Wilaya 12 pamoja na kutoa elimu ya
miongozo na sheria za ubora wa mazao ya nyuki kwa wafanyabiashara wa
mazao ya nyuki.
54. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/2014, Tanzania ilishiriki kwenye Kongamano la
Ufugaji nyuki lililofanyika Kiev, Ukraine. Katika Kongamano hilo, mazao
ya nyuki kutoka Tanzania yalikuwa kivutio kikubwa na yaliwezesha kupata
medali ya Banda Bora la Asali kutokana na asali yake kuwa na viwango vya ubora na usalama vinavyokubalika Kimataifa. Aidha, kampuni mbalimbali zilionesha nia ya kuwekeza kwenye Sekta ya ufugaji nyuki Nchini. Kama ambavyo nimesisitiza mara kwa mara, sekta ya
nyuki ina fursa kubwa ya kibiashara hapa nchini na nje ya nchi. Ni
sekta inayoweza kuleta mapinduzi makubwa katika maeneo mengi kwani
yanahitajika mafunzo kidogo na vifaa vichache ambavyo vinaweza kutumika
kikamilifu kupata asali na mazao yake. Niendelee kusisitiza kwamba, tuwahimize wananchi katika Majimbo yetu watumie fursa za ufugaji nyuki zinazopatikana katika maeneo yao ili kujiongezea kipato.
Maendeleo ya Viwanda
55. Mheshimiwa Spika, Sekta
ya Viwanda Vidogo na Biashara Ndogo imeendelea kutoa mchango muhimu
katika upatikanaji wa ajira, ongezeko la kipato na ukuaji wa uchumi.
Katika mwaka 2013/2014, Serikali imefungua Vituo vya Teknolojia Mikoani
kwa ajili kuhudumia Wajasiriamali wanaotengeneza mashine za kusindika
mazao na kutengeneza bidhaa mbalimbali za uzalishaji mali. Vituo hivyo
vimewezesha kuanzishwa kwa miradi mipya 4,127 ya uzalishaji mali kwenye
mikoa ya Lindi, Mbeya, Iringa, Arusha, Kigoma na Kilimanjaro. Aidha,
Wajasiriamali 23,546 walipatiwa mafunzo ya ujasiriamali na ujuzi maalum
wa ufundi na utumiaji wa mashine za uzalishaji mali. Vilevile, huduma za
ushauri na ugani zilitolewa kwa Wajasiriamali 20,769 kwenye Vikundi na
Vyama vyao vya Biashara kwa kuviimarisha na kuviwezesha kujenga misingi
ya kujitegemea.
56. Mheshimiwa Spika, Serikali
inatekeleza Mkakati wa “Wilaya Moja, Bidhaa Moja” kwa kujenga uwezo wa
kuzalisha bidhaa kutokana na malighafi zilizopo kwenye Wilaya husika.
Kupitia Mkakati huo, Serikali imejenga uwezo wa kuongeza thamani ya
mazao na bidhaa mbalimbali, kuzalisha mitambo na vipuri pamoja na zana
za kilimo ambapo viwanda vidogo 198 vilianzishwa na kuwezesha upatikaji
wa ajira 1,809. Aidha, Serikali inatekeleza Mradi wa Kuendeleza
Ujasiriamali Vijijini (MUVI) kwa kutumia dhana ya kuimarisha mlolongo wa
thamani kimikoa kwa mazao mbalimbali. Mradi umewezesha uanzishwaji wa
miradi midogo 15,580 Vijijini; urasimishaji wa Vikundi 65,308 vya
uzalishaji na upatikanaji wa ajira 39,574.
57. Mheshimiwa Spika, Serikali pia iliendelea na
juhudi za kuhamasisha uwekezaji kwenye miradi mipya katika Maeneo
Maalum ya Uzalishaji (Export Processing Zones) na Maeneo Maalum ya
Kiuchumi (Special Economic Zones). Hadi kufikia mwezi Desemba 2013,
kampuni 32 zilikuwa zimesajiliwa na Mamlaka ya EPZ kwa ajili ya
kuanzisha viwanda vipya kwenye maeneo hayo. Aidha, Serikali imekamilisha
utafiti kwenye Mradi wa Makaa ya Mawe Mchuchuma na kuthibitisha uwepo
wa tani Milioni 370 za makaa ya mawe katika eneo la kilomita za mraba 30
kati ya kilomita za mraba 140 zilizotengwa kwa ajili ya Mradi huo.
Aidha, utafiti huo ulithibitisha uwepo wa tani Milioni 219 za madini ya
chuma katika eneo la kilomita za mraba 10 kati ya kilomita za mraba 166
zilizotengwa kwa ajili ya mradi huo. Ujenzi wa mradi wa makaa ya mawe
Mchuchuma na madini ya chuma Liganga unatarajiwa kuanza mwaka 2014 na
kukamilika mwaka 2018. Katika mwaka 2014/2015,
Serikali itajielekeza
katika kuendeleza viwanda vya kuongeza thamani ya mazao na bidhaa za
kilimo. Aidha, itaendelea kujenga Mradi wa Makaa ya Mawe ya Mchuchuma na
Ngaka na Mradi wa Chuma Liganga.
Sekta ya Utalii
58. Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kutangaza fursa za utalii zilizopo nchini kwa kutumia
mbinu mbalimbali kama vile vipeperushi, majarida, matangazo ya
Televisheni na kutumia Balozi za Tanzania zilizoko nje ya nchi. Mbinu
nyingine zilizotumika ni kutumia maonesho ya Kimataifa na kuweka matangazo kwenye viwanja sita vya Ligi Kuu ya Mpira wa Miguu ya Uingereza. Pamoja na matangazo hayo, huduma
za kitalii hususan hoteli, miundombinu ya barabara na mawasiliano
zimeimarishwa na hivyo kuwashawishi watalii wengi kutembelea nchini. Kutokana
na hatua hizo, idadi ya watalii walioingia nchini imeongezeka kutoka
Watalii 1,077,058 mwaka 2012 hadi 1,135,884 mwaka 2013, sawa na ongezeko
la Asilimia 5.46. Watalii hao wameliingizia Taifa Dola za Marekani
Bilioni 1.8 ikilinganishwa na Dola za Marekani Bilioni 1.7
zilizopatikana mwaka 2012. Vilevile, Serikali imeanzisha utalii wa usiku
katika Hifadhi ya Taifa ya Ziwa Manyara; utalii wa kuangalia wadudu
katika Hifadhi ya Taifa ya Kitulo na Hifadhi ya Amani; utalii wa makasia
katika Hifadhi ya Arusha – Ziwa Momela na Utalii wa kutembea katika
Hifadhi za Mahale na Gombe.
59. Mheshimiwa Spika,
Serikali kwa kushirikiana na Sekta binafsi kupitia Baraza la Taifa la
Biashara, imeandaa mkakati maalum wa kukuza sekta ya utalii hasa kuondoa
vikwazo vinavyokwamisha kasi ya ukuaji wa sekta hii. Aidha, katika
kukuza utalii wa ndani, Serikali inatumia fursa za
maonesho na matamasha mbalimbali ya ndani kuelezea vivutio vya utalii na
imeandaa kijitabu cha utalii wa Utamaduni kwa lengo la kutangaza
vivutio vya utalii. Katika mwaka 2014/2015, Serikali itatafsiri
tovuti ya Bodi ya Utalii pamoja na vielelezo mbalimbali kwa lugha za
Kifaransa, Kijerumani, Kichina na Kihispaniola ili zitumike kutangaza
utalii kwa nchi zinazotumia lugha hizo. Hatua hiyo itasaidia kupanua
wigo wa utalii katika masoko hayo yenye fursa kubwa.
Wanyamapori
60. Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea na juhudi za kuhifadhi
wanyamapori katika Hifadhi na Mapori ya Akiba Nchini kwa nia ya
kuwalinda na kuendeleza utalii. Katika mwaka 2013/2014, Serikali
imeendesha doria mbalimbali ndani na nje ya hifadhi zilizowezesha
kukamatwa watuhumiwa 391 pamoja na silaha 73 zikiwemo bunduki 22 za
kivita. Jumla ya kesi 277 zilifunguliwa ambapo kesi 123 zimemalizika na
kesi 154 zinaendelea. Vilevile, katika kuhamasisha wananchi wanaoishi
kando kando ya hifadhi hizo kuzilinda, Halmashauri 38 zenye vitalu vya
uwindaji zilipatiwa Shilingi Bilioni 8.7 kama mgawo wa Asilimia 25 ya
fedha zinazotokana na uwindaji wa kitalii kwa ajili ya shughuli za
maendeleo ya wananchi.
61. Mheshimiwa Spika, katika
mwaka 2014/2015, Serikali itaanza utekelezaji wa Mkakati wa Kitaifa wa
Kupambana na Ujangili. Mkakati huo umeainisha uwezo tulionao, upungufu
uliopo na mahitaji muhimu ambayo yataimarisha uhifadhi Nchini na
kupunguza migongano iliyopo ya matumizi ya ardhi. Vilevile, itaanzisha
Mamlaka ya Wanyamapori Tanzania itakayosimamia shughuli zote zinazohusu
uhifadhi wa wanyamapori ikiwa ni pamoja na kukusanya mapato, kuendeleza
hifadhi na kuimarisha ulinzi wa wanyamapori.
Sekta ya Madini
62. Mheshimiwa Spika, katika
mwaka 2013/2014, Serikali imeimarisha ukaguzi kwenye uzalishaji na
biashara ya madini. Hatua zilizochukuliwa ni pamoja na kuweka Wakaguzi
katika migodi yote mikubwa na baadhi ya mitambo ya uchenjuaji madini.
Aidha, imeanzisha dawati maalum la kukagua madini yanayosafirishwa nje
ya Nchi kupitia viwanja vya ndege ili kudhibiti utoroshaji wa madini.
Kutokana na jitihada hizo, madini ya dhahabu na vito yenye thamani ya
Shilingi Bilioni 1.9 yalikamatwa na kuwasilishwa kwenye vyombo husika
kwa hatua za kisheria.
63. Mheshimiwa Spika,
Serikali inathamini mchango wa Wachimbaji Wadogo wa Madini katika
kukuza uchumi wa Nchi yetu. Katika mwaka 2013/2014, Serikali imewajengea
uwezo wachimbaji wadogo kwa kuwapatia mafunzo na mikopo ili kuongeza
uzalishaji. Kutokana na juhudi hizo, jumla ya kilo 237 za dhahabu zenye
thamani ya Shilingi Bilioni 14.5 zilizalishwa na kuingiza mrabaha wa
Shilingi Milioni 519. Aidha, Serikali imetenga maeneo mapya ya uchimbaji
ya Isamilo na lwenge (Geita); Rwabasi (Butiama) na Saza na Itumbi “B”
(Chunya). Jitihada hizo zimefanya shughuli za wachimbaji wadogo hasa
katika uchenjuaji wa madini ya dhahabu kukua.
64. Mheshimiwa Spika,
katika mwaka 2014/2015, Serikali itakamilisha Mkakati wa utekelezaji wa
Sera ya Madini ya mwaka 2009, Sheria ya Uongezaji Thamani Madini na
Sheria ya Baruti pamoja na Kanuni zake. Serikali pia itahamasisha
uwekezaji kwenye sekta ya Madini na kuziwezesha taasisi zake kama vile
Tanzania Extractive Industrials Transporency Initiatives (TEITI) na
Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) ili ziweze kufanya kazi kwa
ufanisi. Vilevile, itatenga maeneo zaidi kwa ajili ya wachimbaji wadogo
na kuwawezesha kupata mitaji na teknolojia. Pia, itaboresha Mfumo wa
utoaji na usimamizi wa leseni za madini kwa kuanzisha huduma za kuomba
leseni kwa njia ya mtandao.
65. Mheshimiwa Spika, ardhi
ni msingi na kichocheo muhimu cha maendeleo ikiwa itapangiwa matumizi
bora, itapimwa na kusimamiwa ipasavyo. Ili kufanikisha azma hiyo,
Serikali inachukua hatua madhubuti kuhakikisha kuwa kila kipande
cha ardhi Nchini kinapangwa, kupimwa, kumilikishwa na kutumiwa kwa
mujibu wa Sheria. Katika mwaka 2013/2014, Serikali imekamilisha sehemu
ya kwanza ya ujenzi wa Mfumo Unganishi wa Kuhifadhi Kumbukumbu za Ardhi
(Integrated Land Management Information System) na kurahisisha
upatikanaji wa ardhi kwa ajili ya uwekezaji na matumizi mengine.
Sambamba na hatua hiyo, Serikali inaboresha utunzaji wa kumbukumbu za
upimaji Ardhi kwa kuzibadili zilizopo kuwa katika mfumo wa Kanzidata za
Kielektroniki ili ziweze kuunganishwa na Mfumo Unganishi wa Kutunza
Kumbukumbu za Ardhi. Hatua hiyo inalenga kurahisisha upatikanaji wa
taarifa za upimaji ardhi na kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.
Hadi mwezi Februari 2014, kumbukumbu za ramani 5,000 za Jiji la Dar es
Salaam zimebadilishwa na kuwekwa katika ramani unganishi. Katika mwaka
2014/2015, Serikali itaandaa Kanzidata ya viwanja 300,000 katika Miji
mbalimbali Nchini.
66. Mheshimiwa Spika, kwa
muda mrefu Sekta ya Ardhi imekumbwa na tatizo la migogoro ya mara kwa
mara inayotokana na matumizi mbalimbali ya ardhi hususan baina ya
wakulima na wafugaji. Aidha, migogoro hiyo imekuwa ikihusisha wananchi
na maeneo ya hifadhi, Vijiji kuwepo ndani ya maeneo ya hifadhi, wananchi
dhidi ya wawekezaji na baina ya wananchi wenyewe kwa wenyewe.
Migogoro hii imekuwa ikiongezeka zaidi katika siku za hivi karibuni
kutokana na kuongezeka kwa idadi ya watu, mifugo na shughuli za kiuchumi
zinazotegemea ardhi kama vile madini, utalii, viwanda, kilimo na
makazi. Migogoro ya ardhi ina athari kubwa kwa wananchi ikiwemo
uvunjifu wa amani, uharibifu wa mali na hata vifo. Serikali imekuwa
ikichukua hatua kudhibiti migogoro hiyo kila inapotokea. Ili kupata
suluhisho la kudumu la kushughulikia migogoro ya ardhi, Serikali
imeanza kusimika mifumo ya kisasa kwa ajili ya upimaji, umilikishaji na
usimamizi wa sekta ya ardhi. Hii ni kwa sababu uzoefu umeonesha kwamba
ukosefu wa ramani, mipaka rasmi na miliki kamilifu ndicho chanzo kikuu
cha migogoro inayojitokeza mara kwa mara. Katika mwaka 2014/2015,
Serikali itatoa kipaumbele katika Sekta ya Ardhi hasa kushughulikia
maeneo yanayolenga kutatua migogoro ya ardhi kama vile upimaji wa mipaka
ya vijiji, kutoa hati miliki na kuandaa mipango ya matumizi bora ya
ardhi ya Vijiji. Aidha, Serikali itajenga Mfumo Unganishi wa Kutunza
Kumbukumbu za Ardhi, kukamilisha usimikaji wa alama za msingi za
upimaji, kurasimisha hati milki na kupima mipaka ya Kimataifa.
Nishati
67. Mheshimiwa Spika, Serikali
imeimarisha huduma za upatikanaji wa umeme Nchini kwa kutekeleza miradi
mbalimbali ili kuongeza idadi ya Watanzania wanaopata umeme. Mwaka
2013/2014, Serikali imekamilisha kwa Asilimia 90 Awamu ya Kwanza ya
Mradi Kabambe wa Usambazaji wa Umeme unaotekelezwa katika Mikoa 16
Nchini. Pia, Mradi huo unajumuisha usambazaji wa umeme Vijijini ambapo
wateja 15,305 kati ya wateja 22,000 waliolengwa wameunganishiwa umeme.
Vilevile, Wakala wa Nishati Vijijini imesaini Mikataba 35 na Wakandarasi
kwa ajili ya kutekeleza miradi ya usambazaji wa umeme Vijijini kupitia
Mradi Kabambe wa Usambazaji wa Umeme Vijijini. Aidha, tarehe
8 Septemba 2013, Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania alizindua mtambo wa kufua umeme wa Megawati 60
unaotumia mafuta mazito katika eneo la Nyakato, Mwanza. Mtambo huo
umeongeza uwezo wa kufua umeme kwenye gridi ya Taifa na kufikia Megawati
1,583. Mtambo huo umeimarisha upatikanaji wa umeme katika Mikoa ya
Mwanza, Geita na Mara. Kutokana na juhudi za kusambaza umeme Mijini na
Vijijini hadi mwezi Machi 2014, zaidi ya Asilimia 30 ya Watanzania
wamepatiwa huduma hiyo, na hivyo kuvuka lengo la Asilimia 30
lililotarajiwa kufikiwa mwaka 2015.
68. Mheshimiwa Spika, kutokana
na kukua kwa kasi kwa Sekta ya gesi, Serikali katika mwaka 2013/2014,
imeandaa Sera ya Gesi Asilia ambayo inatoa miongozo ya kusimamia
rasilimali hiyo. Serikali pia inatekeleza miradi mbalimbali chini ya
sekta ndogo ya gesi ikiwa ni pamoja na kuendelea na Mradi wa Ujenzi wa
Bomba la Kusafirisha Gesi Asilia kutoka Mtwara na Lindi hadi Dar es
Salaam. Hadi sasa, mabomba yote kwa ajili ya kutekeleza mradi huo wenye
urefu wa Kilomita 542 yamewasili na kazi ya kuunganisha inaendelea.
Ujenzi wa Bomba la Kusafirishia Gesi pamoja na mitambo miwili ya
kuchakata gesi hiyo inatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwaka 2014.
Aidha, Awamu ya Kwanza ya Mradi wa Kinyerezi utakaozalisha Megawati
150 kwa kutumia Gesi Asilia umeanza kutekelezwa. Katika hatua
nyingine, Serikali imepitia upya miundo ya Shirika la Maendeleo ya
Petroli Tanzania na Shirika la Umeme Tanzania kwa lengo la kuongeza tija
na ufanisi wa utendaji wa Mashirika hayo.
69. Mheshimiwa Spika, katika
mwaka 2014/2015, Serikali itakamilisha mchakato wa Maboresho ya sera
mbalimbali za Nishati ikiwemo Sera ya Nishati ya Mwaka 2003; Sera Mpya
ya Mafuta na Sera Mpya ya Uwezeshaji Wazawa. Kukamilika kwa sera hizo
kutaimarisha usimamizi wa Sekta ya Nishati kwa maendeleo ya Nchi yetu.
Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano
70. Mheshimiwa Spika, Serikali imekamilisha Awamu ya Kwanza na ya Pili ya ujenzi wa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano wenye urefu wa kilomita 7,560 ambao
pia unatoa maunganisho ya mawasiliano kwa Nchi jirani. Awamu ya Tatu ya
ujenzi itakayoziunganisha Unguja na Pemba na Mkongo wa Taifa imeanza
mwezi Desemba, 2013 na inatarajiwa kukamilika katika miezi 18. Mkongo
umesaidia watoa huduma kufikisha huduma za mawasiliano kwa Wananchi kwa
uharaka zaidi, uhakika na kwa gharama nafuu. Hatua hiyo inaharakisha
maendeleo ya Taifa kwa Wananchi kupata fursa ya kutumia TEHAMA
katika kupambana na umaskini na kujiletea maendeleo kwa kasi zaidi. Pia,
Serikali kwa kutumia ruzuku imeendelea kupeleka huduma za mawasiliano
katika maeneo yasiyokuwa na mvuto wa kibiashara kwa kushirikiana na
Sekta binafsi. Katika mwaka 2013/2014 jumla ya Kata 52 zenye Vijiji 316
vimefikishiwa huduma za mawasiliano kupitia Mpango huo. Aidha, Serikali
imetia saini makubaliano na watoa huduma za mawasiliano kufikisha huduma
hizo katika Kata nyingine163 zenye Vijiji 922. Watu 1,211,841
watanufaika na juhudi hizo. Katika mwaka 2014/2015, Serikali itaendelea na ujenzi wa Mkongo maeneo ya mijini katika Miji ya Morogoro, Arusha, Mwanza na Dodoma na kuendelea kuunganisha Unguja na Pemba na Mkongo huo.
Simu za Mkononi na Intaneti
71. Mheshimiwa Spika,
mazingira mazuri yaliyowekwa na Serikali kwenye Sekta ya Mawasiliano
yameonesha matokeo chanya na ya kuridhisha sana. Idadi ya watumiaji wa
huduma za mawasiliano Nchini imeongezeka kutoka laini za simu za
mkononi Milioni 2.96 mwaka 2005 hadi Milioni 27.45 mwaka 2013. Watumaji
wa mfumo wa intaneti nao wameongezeka kutoka Milioni 3.56 mwaka 2008
hadi Milioni 9.3 mwaka 2013. Pia, kuna ongezeko kubwa la huduma kupitia
mawasiliano ya simu za mkononi. Huduma hizo ni pamoja na miamala ya
kifedha na ununuzi wa huduma na bidhaa kwa kutumia miamala ya
kibenki. Hivi sasa wananchi wanaweza kufanya malipo ya huduma
mbalimbali wanazozitumia kupitia simu za kiganjani. Hatua hiyo imesaidia
kuokoa muda na kupunguza msongamano sehemu za kulipia na kupata huduma
hizo.
Mfumo wa Kuhakiki na Kusimamia Huduma za Mawasiliano
72. Mheshimiwa Spika,
Serikali ililiahidi Bunge lako Tukufu kwamba ingesimika Mfumo wa
Kusimamia Mawasiliano ya Simu Nchini. Lengo la kujenga Mfumo huo ni
kubaini takwimu zinazopita katika mitandao ya mawasiliano. Mfumo huo
unaweza kutoa takwimu za mawasiliano yanayofanyika ndani na nje ya
Nchi; kutambua mapato na miamala ya fedha; kufuatilia na kugundua
mawasiliano ya ulaghai; na kutambua taarifa za laini ya simu na za
kifaa cha mawasiliano. Napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu kuwa, tayari Mtambo
wa kuwezesha Mfumo wa Kusimamia Mawasiliano Tanzania umejengwa kwa
gharama ya Dola za Marekani Milioni 25 kwa kutumia utaratibu wa Ubia
kati ya Serikali na Sekta Binafsi (Build, Operate and Transfer).
Ili kuweza kutumia Mfumo huo ipasavyo, Serikali imekamilisha Kanuni za
Uhakiki na Mgawanyo wa Mapato yatokanayo na simu zinazoingia Nchini
kutoka nje ya Nchi. Mfumo huo umeanza rasmi kutumika mwezi Oktoba, 2013
na kwa kipindi cha miezi mitatu ya Oktoba hadi Desemba, 2013 umeingizia
Serikali Shilingi Bilioni 5. Katika mwaka 2014/2015, Serikali
itaendelea kuboresha taarifa za kiutendaji zitakazowezesha kupunguza
kasi ya udanganyifu wa simu zinazoingia nchini kwa lengo la kuongeza
mapato. Vilevile, Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania itasimamia miamala ya
malipo ya fedha kupitia simu za mkononi yanayofanywa na kampuni za simu.
Mfumo wa Utangazaji wa Digiti
73. Mheshimiwa Spika,
itakumbukwa kwamba, Serikali ilianza kutekeleza awamu ya kwanza ya
zoezi la kuhama kutoka mfumo wa utangazaji wa Analojia kwenda Digiti
tarehe 31 Desemba, 2012. Awamu hiyo ilihusisha Miji Saba ya Dar es
Salaam, Mbeya, Tanga, Mwanza, Arusha, Dodoma na Moshi. Uhamaji huo
ulifanyika kwa mafanikio makubwa na tathmini ilifanywa ili kuweka
mazingira bora zaidi ya kuendelea na zoezi hilo. Kufuatia tathmini hiyo,
Awamu ya Pili ilianza kutekelezwa kuanzia tarehe 31 Machi, 2014 na
inatarajiwa kukamilika tarehe 30 Septemba, 2014. Miji kumi itakayohusika
na zoezi hilo ni Singida na Tabora, ikifuatiwa na Miji ya Musoma,
Bukoba, Kigoma, Kahama, Iringa, Songea, Morogoro na Lindi. Uzimaji wa
mitambo ya utangazaji ya Analojia unahusisha maeneo yote yanayopata
huduma za matangazo kupitia mitambo ya kusimikwa ardhini tu, ambayo ni
Asilimia 24 ya eneo lote la Nchi yetu. Maeneo yanayopata huduma za
matangazo kupitia mitambo ya Satellite na Cable hayahusiki na
zoezi hilo.
Serikali
imelenga ifikapo mwezi Oktoba, 2014 mitambo yote ya Analojia iwe
imezimwa Nchini. Napenda kurudia wito wangu kwamba, zoezi hili ni la
muhimu na lina lengo la kuifanya Nchi yetu iendane na mabadiliko
yanayotokea duniani ambayo hayakwepeki. Wadau wote watoe ushirikiano
kwa vyombo vinavyohusika.
Barabara na Madaraja
74. Mheshimiwa Spika, katika
mwaka 2013/2014, Serikali imekamilisha ujenzi wa kilometa 505.7 za
Barabara Kuu na kukarabati kilometa 146.6. Aidha, imejenga kwa kiwango
cha lami kilometa 22.3 za Barabara za Mikoa na kukarabati kilometa 145.1
kwa kiwango cha changarawe. Serikali inaendelea kukamilisha ujenzi wa madaraja ya Kigamboni – Dar es Salaam na Mto Malagarasi - Kigoma. Katika
mwaka 2014/2015, Serikali itajenga Barabara mpya zenye urefu wa
kilometa 633 za Barabara kuu na Barabara za Mikoa kwa kiwango cha lami.
Vilevile, itakarabati kilometa 165 za barabara za lami na kilometa 1,150
za barabara za changarawe katika Barabara Kuu na Barabara za Mikoa.
Aidha, itaendelea na ujenzi wa madaraja 57 ya barabara hizo.
Msongamano wa Magari Jijini Dar es Salaam
75. Mheshimiwa Spika, msongamano
wa magari katika Jiji la Dar es Salaam umekuwa kikwazo katika
utekelezaji wa shughuli za kila siku za kiuchumi na kijamii.
Katika kukabiliana na tatizo hilo, mwaka 2013/2014, Serikali
imekamilisha ujenzi wa barabara za lami za Ubungo Bus Terminal - Kigogo -
Kawawa yenye urefu wa kilometa 6.4; barabara ya Jet Corner –Vituka -
Davis Corner yenye urefu wa kilometa 10.3 na barabara ya Ubungo Maziwa - Mabibo External yenye urefu wa kilometa 2.25 pamoja na daraja la External. Ujenzi wa barabara ya Mzunguko wa Kigogo - Jangwani yenye kilometa 2.72 na zile zitakazotumika kwa Mabasi yaendayo haraka unaendelea.
76. Mheshimiwa Spika, katika
mwaka 2014/2015, Serikali itajenga barabara sita Jijini Dar es Salaam
kwa kiwango cha lami. Barabara hizo ni Tabata Dampo - Kigogo (km 1.6);
Kifuru - Kinyerezi (km 4); Goba - Mbezi Mwisho (km 7); Tangi bovu
(Samaki) - Goba (km 9); Kimara Baruti - Msewe (km 2.6) na Kimara -
daraja la Maji Chumvi External (km 3). Tayari Serikali imesaini mikataba
na wakandarasi kwa ajili ya ujenzi wa barabara hizo ambazo zinatarajiwa
kukamilika kati ya miezi 8 hadi 18.
HALI YA UCHUKUZI
Reli ya Kati na TAZARA
77. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/2014, Serikali imefanya upembuzi
yakinifu na usanifu wa awali wa ujenzi wa reli ya Arusha – Musoma yenye
urefu wa Kilomita 600. Lengo ni kuimarisha usafiri na usafirishaji wa
mizigo kwa Mikoa ya Kaskazini na Nchi jirani ya Uganda kupitia Bandari
ya Tanga. Vilevile, Serikali imekamilisha usanifu wa kina wa mradi wa
ujenzi wa reli kwa kiwango cha kimataifa yenye urefu wa Kilometa 1,464
kutoka Dar es Salaam - Isaka - Keza - Kigali na Kilometa 197 kutoka
Keza hadi Msongati.
78. Mheshimiwa Spika, Mkataba wa Maelewano kati ya Tanzania na Burundi kwa ajili ya ujenzi wa Reli ya Uvinza hadi Msongati umesainiwa. Kuhusu Reli ya TAZARA, Serikali
inatekeleza Makubaliano ya Itifaki ya 15 iliyosainiwa mwezi Machi, 2012
kati ya Serikali ya Watu wa China na Serikali za Tanzania na Zambia
ambapo ununuzi wa vichwa vinne vya treni, vichwa vinne vya Sogeza
umefanyika pamoja na ununuzi wa mabehewa 18 ya abiria ya Reli ya TAZARA.
Katika mwaka 2014/2015, Serikali itaboresha Kilometa 308 za miundombinu
ya Reli ya Kati na vituo vya Bandari kavu vya kuhifadhi Makasha vya
Ilala na Isaka. Aidha, Kampuni ya Reli (TRL) itakarabati vichwa nane vya treni na kununua vichwa vipya 12 na mabehewa 204 ya mizigo na kukarabati majengo ya Stesheni.
79. Mheshimiwa Spika, kijiografia
nchi yetu imejaliwa kuwa na eneo kubwa la maziwa na bahari ambalo
limetuwezesha kuwa na bandari zinazohudumia pia Nchi jirani zisizopakana
na bahari. Ili kutumia fursa hii kikamilifu, Serikali katika mwaka
2013/2014, imekamilisha upembuzi yakinifu kwa ajili ya kuboresha Gati namba 1 hadi 7 katika Bandari ya Dar es Salaam. Vilevile, inatekeleza miradi ya ujenzi wa magati kwenye Bandari za Ziwa Victoria, Tanganyika na Nyasa. Aidha, kupitia Mfumo wa Tekeleza Sasa kwa Matokeo Makubwa, Mamlaka
ya Bandari imevuka malengo kwa kuhudumia zaidi ya tani Milioni 13 za
mizigo hadi Desemba 2013, ikilinganishwa na tani Milioni 12 kwa mwaka
2012. Vilevile, Serikali imeanza kutekeleza utaratibu
wa kufanya kazi bandarini kwa saa 24 kwa siku zote za juma ili kuongeza
kasi ya uondoshaji wa mizigo inayotoka. Hatua hiyo imesaidia
kupunguza msongamano wa mizigo katika Bandari ya Dar es Salaam na
kupunguza malalamiko kutoka kwa watumiaji wa bandari hiyo. Aidha,
kumekuwa na ongezeko la ufanisi katika kuhudumia wasafirishaji wa mizigo
katika maeneo ya mipakani, hususan Rusumo, Tunduma, Namanga, Kasumulo
na Mtukula. Wasafirishaji wanatumia muda mfupi hivi sasa ikilinganishwa
na hapo awali. Kwa mfano, muda wa huduma katika mpaka wa Rusumo,
umepungua kutoka siku tatu hadi nusu saa.
80. Mheshimiwa Spika, katika
mwaka 2014/2015, Serikali itaanza kuboresha Gati namba 1 hadi 7 ili
kuwezesha Bandari ya Dar es Salaam kuhudumia mizigo tani Milioni 18
kutoka tani Milioni 13.5 za sasa. Aidha, itakamilisha ujenzi wa magati
katika Bandari ya Mtwara, kukamilisha majadiliano na kuanza ujenzi wa
Bandari ya Bagamoyo na kuendelea na miradi ya ujenzi wa magati kwenye Bandari za Ziwa Victoria, Tanganyika na Nyasa. Vilevile,
itakarabati meli za MV Umoja, MV Victoria, MV Butiama, MV Serengeti, MV
Liemba, MT Sangara, MT Ukerewe na meli ya MV Songea ili kuboresha
usafiri na usafirishaji katika maziwa.
81. Mheshimiwa Spika, Serikali imeboresha
miundombinu ya viwanja vya ndege Nchini na kuviwezesha kutoa huduma kwa
kuzingatia Sheria na Kanuni za uendeshaji za kimataifa. Katika mwaka
2013/2014, jumla ya viwanja vya ndege 13 ikiwemo Viwanja vya Mwanza, Musoma, Bukoba,
Kigoma, Tabora, Arusha, Tanga, Lindi, Mtwara, Iringa, Songea,
Nachingwea na Kilwa Masoko vilifanyiwa ukaguzi na kupata leseni ya
uendeshaji. Aidha, Serikali imeanza mradi wa ujenzi wa jengo jipya la tatu la abiria katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere utakaogharimu Shilingi Bilioni 518. Mradi huo ambao umewekwa jiwe la msingi na Mheshimiwa Dkt
Jakaya Mrisho Kikwete tarehe 24 Aprili, 2014 unatarajiwa kukamilika
mwezi Oktoba, 2015. Jengo hilo litakuwa na ukubwa wa meta za mraba
70,000 ambao ni zaidi ya mara nne ya ukubwa wa jengo lililopo sasa lenye
ukubwa wa meta za mraba 15,000. Baada ya kukamilika kwa jengo hilo na
miundombinu yake, Uwanja huo utakuwa na uwezo wa kuegesha ndege kubwa za
abiria. Aidha, utahudumia abiria milioni sita kwa mwaka ikilinganishwa
na abiria milioni 2.5 kwa sasa. Vilevile, Uwanja huo utatoafursa mbalimbali za kiuchumi, kibiashara na kukuza utalii nchini. Aidha, utazalisha ajira mpya zaidi ya 7,000 kwa Watanzania.
82. Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua
umuhimu wa kuboresha miundombinu ya usafiri wa anga ili kuimarisha
huduma za usafiri nchini pamoja na kuvutia uwekezaji na utalii. Kwa
kuzingatia azma hiyo, mwezi Oktoba 2013, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete alizindua rasmi Uwanja wa
Ndege wa Mafia baada ya ujenzi wake kukamilika kwa kiwango cha lami.
Kuzinduliwa kwa uwanja huo kumefungua fursa za kibiashara, hususan
ya utalii katika kisiwa hicho. Vilevile, mwezi Julai 2013, Mheshimiwa
Rais, aliweka jiwe la msingi la ujenzi wa njia ya kuruka na kutua ndege
kwa kiwango cha lami katika Uwanja wa Ndege wa Bukoba. Katika
mwaka 2014/2015, Serikali itaendelea na ujenzi wa jengo jipya la abiria
katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere na kukamilisha
ujenzi wa Uwanja mpya wa Kimataifa wa Ndege wa Songwe, Mbeya. Serikali
pia itakamilisha ukarabati wa Viwanja vya ndege vya Mwanza, Bukoba,
Kigoma na Tabora na kuanza kukarabati viwanja vya ndege vya Shinyanga,
Mtwara na Sumbawanga.
83. Mheshimiwa Spika, ili kuhakikisha kuwa utoaji wa elimu unafuata Sera, Miongozo na Mitaala, Serikali imeendelea kupitia Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 1995. Aidha, kupitia Mfumo wa Tekeleza Sasa kwa Matokeo Makubwa katika elimu ya msingi,
utaratibu wa kupima stadi za Kusoma, Kuandika na Kuhesabu (K3) kwa
wanafunzi wa darasa la Kwanza na la Pili umeanzishwa kwa lengo la kupima
na kuweka msingi wa kuboresha stadi husika kabla ya kuingia darasa
linalofuata. Katika mwaka huu wa fedha, Serikali imeajiri jumla ya
walimu 17,928 wa shule za msingi na kupangiwa katika Mamlaka za Serikali
za Mitaa. Kuajiriwa kwa walimu hao kutapunguza pengo la walimu
lililopo.
84. Mheshimiwa Spika, katika
mwaka 2014/2015, Serikali kupitia Mfumo wa Tekeleza Sasa kwa Matokeo
Makubwa, itaimarisha elimu ya msingi kwa kuongeza uwazi wa kiutendaji,
kuwajengea walimu uwezo wa kutoa msaada wa kimasomo kwa wanafunzi wenye
uhitaji maalum, kuinua ubora wa mazingira ya kufundishia na kujifunzia,
kuongeza upatikanaji wa vifaa vya kufundishia na kujifunzia na kuongeza
uwajibikaji wa watendaji katika utoaji wa elimu.
Elimu ya Sekondari
85. Mheshimiwa Spika, katika
mwaka 2013/2014, Serikali imeweka juhudi kubwa katika kuimarisha Elimu
ya Sekondari hasa ujenzi wa madarasa, nyumba za walimu, maabara, ununuzi
wa madawati na vitabu pamoja na kuboresha miundombinu na mazingira ya
kujifunzia na kufundishia. Aidha, Serikali imeajiri Walimu wapya wa
Sekondari 18,410 na kutoa mafunzo kazini kwa Walimu 12,476. Kati ya hao,
Walimu 8,400 ni wa masomo ya Sayansi na Hisabati. Hatua hizo
zimechangia kuongeza ufaulu wa Wanafunzi waliofanya Mtihani wa Kidato
cha Nne mwaka 2013 kufikia Asilimia 58.25 ikilinganishwa na Asilimia
43.08 mwaka 2012. Katika mwaka 2014/2015, Serikali itatoa kipaumbele cha
uwekezaji kwenye miundombinu ya Shule za Sekondari, Walimu, Ukaguzi na
Vitendea kazi.
86. Mheshimiwa Spika, Serikali
imeanza kutekeleza Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya
Ufundi Stadi wa mwaka 2013/2014 hadi 2017/2018. Mpango huo unalenga
kuongeza udahili katika ngazi mbalimbali za Elimu na Mafunzo ya Ufundi
ili kujenga uwiano wa nguvukazi katika ngazi mbalimbali kwa kila fani.
Vilevile, unalenga kujenga nguvukazi yenye kuhimili ushindani wa soko la
ajira kwa kuinua ubora wa elimu na mafunzo ya ufundi ili kukidhi
mahitaji ya soko la ndani na nje ya Nchi. Ili kutekeleza mpango huo,
katika mwaka 2013/2014, Serikali ilianza kutumia Vyuo vya Maendeleo ya
Wananchi 25 kutoa mafunzo ya masomo ya ufundi stadi ili kuongeza udahili
wa wanafunzi. Katika mwaka 2014/2015, Serikali itaanza ujenzi wa vyuo vya ufundi stadi katika Mikoa ya Rukwa, Geita, Simiyu na Njombe.
87. Mheshimiwa Spika, Serikali imeboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia masomo ya sayansi na teknolojia kwenye Vyuo Vikuu nchini. Katika mwaka 2013/2014, kupitia
Mradi wa Sayansi, Teknolojia na Elimu ya Juu, Serikali imekamilisha
ujenzi wa vyumba 48 vya Mihadhara, Maabara 93 za sayansi na Ofisi 302
za wafanyakazi katika Vyuo Vikuu mbalimbali vya Umma nchini. Aidha,
vifaa vya kufundishia na kujifunzia na vya TEHAMA vilinunuliwa katika
Vyuo hivyo na kuziunganisha Taasisi 28 za elimu ya juu katika Mkongo wa
Taifa wa Mawasiliano.
88. Mheshimiwa Spika, kutokana na kuwepo kwa malalamiko mengi kuhusu Vyuo Vikuu nchini kutoza ada tofauti kwa mafunzo ya aina moja, Serikaliimekamilisha Mwongozo wa Gharama Halisi ya Kumsomesha Mwanafunzi wa Elimu ya Juu. Mwongozo huo unatoa ukomo
wa ada inayotakiwa kutozwa na chuo kwa kila programu au kozi kwa
mwanafunzi. Lengo ni kuondoa upangaji na upandishaji wa ada kiholela
kwa wanafunzi wanaosoma elimu ya juu pasipo kuzingatia gharama halisi ya
kumsomesha mwanafunzi husika kulingana na kozi anayosoma. Katika mwaka 2014/2015, Serikali itasimamia utekelezaji wa Mwongozo huo.
MAENDELEO YA SEKTA YA AFYA
Huduma ya mama na mtoto
89. Mheshimiwa Spika, Serikali
inaendelea kuimarisha huduma ya afya ya Mama na Mtoto kwa kutekeleza
Mpango Mkakati wa Kuongeza Kasi ya Kupunguza Vifo vitokanavyo na
Matatizo ya Uzazi na Vifo vya Watoto wa mwaka 2008 hadi 2015. Katika
kutekeleza Mkakati huo, Serikali imeandaa Mpango Kazi wa Uzazi wa Mpango Uliothaminiwa. Mpango
Kazi huo unalenga kununua na kusambaza dawa na vifaa vya uzazi wa
mpango nchini. Aidha, Serikali imeimarisha mfumo wa rufaa kwa mama
wajawazito kwa kununua vyombo vya usafiri kwa wahudumu wa afya ngazi ya
jamii na kuvisambaza katika mikoa yenye kiwango cha juu cha vifo vya
mama vitokanavyo na matatizo ya uzazi. Vilevile, Serikali inatekeleza
Mpango Mkakati wa Kutokomeza Maambukizi Mapya ya VVU kutoka kwa mama
kwenda kwa mtoto ambao ulizinduliwa tarehe Mosi, Desemba, 2012 na
Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania. Awamu ya kwanza ya Mpango huo ilianza
mwezi Oktoba, 2013 na kuhusisha Mikoa tisa yenye uambukizo mkubwa wa VVU
kwa wajawazito. Mikoa hiyo ni Iringa, Njombe, Mbeya, Tabora, Simiyu,
Shinyanga, Mwanza, Geita na Kagera. Awamu ya pili imeanza mwezi
Januari, 2014 kwa Mikoa 16 iliyobakia.
90. Mheshimiwa Spika, katika
mwaka 2014/2015, Serikali itakamilisha mapitio ya Mpango Mkakati wa
Kuongeza Kasi ya Kupunguza Vifo vya Mama vitokanavyo na Uzazi na Vifo
vya Watoto na kutekeleza afua nyingine za kipaumbele. Aidha, kupitia
Mpango wa Kitaifa wa Uzazi wa Mpango dawa na vifaa vyote vya uzazi wa
mpango vitanunuliwa na kusambazwa ili viweze kuwafikia wananchi
wanaovihitaji. Lengo ni kufikia Asilimia 60 ya kiwango cha utumiaji
huduma za uzazi wa mpango kama ilivyoanishwa kwenye Malengo ya Maendeleo
ya Milenia.
Udhibiti wa Maambukizi ya Malaria
91. Mheshimiwa Spika, katika
kukabiliana na maambukizi ya ugonjwa wa malaria, Serikali imeendelea
kugawa vyandarua shuleni na kuhimiza matumizi endelevu. Katika mwaka
2013/2014, Serikali iligawa vyandarua 510,000 katika shule 2,302 za
msingi na Sekondari za Mikoa ya Lindi, Mtwara na Ruvuma kupitia Programu
ya Wanafunzi Shuleni. Aidha, kupitia mikakati na afua nyingine Serikali
ilisambaza vyandarua 879,856 vyenye viuatilifu vya muda mrefu kupitia Mpango wa Hati Punguzo kwa wajawazito na watoto wenye umri chini ya mwaka mmoja.
92. Mheshimiwa Spika,
Serikali kwa kushirikiana na Serikali ya Cuba, inatekeleza Mpango wa
kuangamiza Viluwiluwi vya Mbu kwa kutumia njia za Kibaiolojia katika
Jiji la Dar es Salaam. Mpango huo pia, utatekelezwa katika Mikoa mingine
mitano. Aidha, Serikali kwa kushirikiana na wadau iliendelea na zoezi
la kupulizia dawa ya ukoko katika kaya 838,000 zilizopo kwenye Mikoa ya
Kagera, Mara na Mwanza ambapo zaidi ya Wananchi 4,505,752 wamekingwa
dhidi ya maambukizi ya ugonjwa wa malaria. Pia, Serikali imekamilisha
kusambaza kipimo cha malaria kinachotoa majibu ya haraka katika
vituo vyote vya kutolea huduma Nchini. Vilevile, jumla ya
dozi 14,655,000 za Dawa Mseto na Vitendanishi 9,853,710 vimenunuliwa na
kusambazwa katika vituo vya huduma na hivyo kuimarisha upatikanaji wa
dawa na vitendanishi Nchini.
Mheshimiwa Spika,
katika mwaka 2014/2015, Serikali itaendelea kugawa vyandarua Milioni 7.2
vyenye viuatilifu vya muda mrefu kupitia Mpango wa Hati Punguzo, na
kuendeleza kampeni maalum ya kugawa vyandarua kwa jamii katika ngazi ya
kaya. Aidha, zoezi la kugawa vyandarua kwa wanafunzi shuleni
litaendelezwa kwa Mikoa ya Kusini. Sambamba na hatua hizo, mradi wa
kuangamiza viluwiluwi vya mbu katika mazalia utapelekwa katika Mikoa
mingine mitano kwa kutumia viuatilifu (Biolarvicides) vitakazozalishwa
katika kiwanda kinachojengwa Kibaha, Mkoa wa Pwani ambacho kinatarajiwa
kuanza kazi mwaka huu wa 2014.
Huduma kwa Wazee na Watu Wenye Ulemavu
93. Mheshimiwa Spika, Sera
ya Taifa ya Wazee ya mwaka 2003 na Sera ya Taifa ya Huduma na Maendeleo
kwa Watu Wenye Ulemavu ya mwaka 2004 zinasisitiza kuwa makundi hayo
yana haki ya kupata matunzo katika jamii. Katika mwaka 2013/2014,
Serikali ilitoa huduma za msingi kwa wazee na watu wenye ulemavu
wasiojiweza wanaotunzwa na kulelewa katika Makazi 17 ya Serikali. Jumla
ya wahudumiwa 1,235 walipatiwa huduma za msingi ikiwemo chakula, malazi,
mavazi pamoja na kuwapatia vifaa yakiwemo magodoro, mashuka, vitanda na
nyenzo za kujimudu. Vilevile, Serikali iliratibu huduma za matunzo
katika Makazi 24 yanayoendeshwa na Mashirika Yasiyo ya Kiserikali ili
kupunguza malalamiko kuhusu upungufu wa huduma zinazotolewa.
94. Mheshimiwa Spika,
naomba nitumie fursa hii kusisitiza kuwa, wazee na watu wenye ulemavu
na wasiojiweza wanahitaji kupatiwa matunzo katika jamii zao. Huduma
zinazotolewa kwenye vituo na taasisi za Serikali na zisizo za Serikali
ni hatua ya mwisho pale ambapo itathibitika kuwa mzee au mlemavu huyo
hana mtu kabisa wa kumtunza katika familia na jamii. Natoa rai kwa
wananchi kuendeleza utamaduni wa kuwatunza wazee wetu na watu wenye
ulemavu. Huu ni utamaduni mzuri sana. Aidha, nazikumbusha Halmashauri
kutenga fedha za kuyahudumia makundi hayo. Katika mwaka 2014/2015,
Serikali itazindua Baraza na Mfuko wa Taifa wa Huduma kwa Watu wenye
Ulemavu ili kuwajengea na kuongeza uwezo wao katika kuzifikia fursa za
maendeleo na kuimarisha utawala bora.
Lishe
95. Mheshimiwa Spika,
katika mwaka 2013/2014, Serikali imeendelea kusimamia Kanuni za
Uongezaji wa Virutubishi katika vyakula ambapo viwanda vikubwa sita vya
kusindika unga wa ngano na viwanda vitatu vya kusindika mafuta ya kula
vinaweka virutubishi katika vyakula vinavyotengenezwa. Takwimu
zinaonesha kuwa, takribani watu milioni 10 wanatumia unga wa ngano
uliorutubishwa na Milioni 4 wanatumia mafuta ya kupikia yaliyorutubishwa
na vitamin A. Vilevile, Serikali imeandaa Mpango wa Uongezaji wa
Virutubishi kwenye vyakula Ngazi ya jamii ambapo utekelezaji wake
ulishaanza katika Mikoa ya Iringa, Njombe, Arusha na Dar es Salaam.
Mpango huo unalenga uwekaji virutubishi kwenye unga wa mahindi
unaozalishwa na wajasiriamali wadogo na kusagwa kwenye viwanda vya kati
na vidogo.
96. Mheshimiwa Spika, Sekta
binafsi inashirikishwa kikamilifu katika mapambano dhidi ya utapiamlo
nchini. Mwezi Mei 2013, Serikali ilikabidhi tani nane za Madini joto kwa
Muungano wa Wasindikaji wa Chumvi katika maeneo mbalimbali Nchini kama
sehemu ya mchango wa Serikali wa kuimarisha Sekta Binafsi katika
mapambano dhidi ya utapiamlo. Serikali pia imeimarisha Maabara za
uwekaji madini joto katika chumvi kwa kununua na kugawa vitendanishi
katika Maabara 13 za Mikoa. Lengo ni kupanua wigo wa Wananchi wanaopata
vyakula vyenye virutubishi. Natoa wito kwa Viongozi katika ngazi zote.
Kusimamia juhudi hizo za Serikali na kuhakikisha zinaendelezwa katika
maeneo yao. Aidha, ninawasihi Wafanyabiashara wote wenye viwanda vya
chakula kutekeleza jukumu hilo kikamilifu. Kwa wale ambao
hawajakamilisha taratibu za ufungaji wa mashine za kuongeza virutubishi
wafanye hivyo mapema iwezekanavyo.
HALI YA UPATIKANAJI WA MAJI NCHINI
Huduma ya Maji Vijijini
97. Mheshimiwa Spika,
Serikali inatekeleza Sera ya Taifa ya Maji ya mwaka 2002 inayolenga
kuboresha huduma ya maji Mijini na Vijijini kwa kushirikisha Wananchi na
Sekta Binafsi. Katika kutekeleza azma hiyo, Serikali iliweka lengo la
kutoa huduma za maji kwa Asilimia 65 Vijijini katika umbali usiozidi
mita 400. Ili kuongeza kasi ya kufikia lengo hilo, katika mwaka
2013/2014, Serikali iliongeza bajeti ya maji kwa Shilingi Bilioni 184 kwa ajili ya kuendeleza miradi mbalimbali ya maji.
98. Mheshimiwa Spika, utekelezaji
wa Mradi wa Maji kwa Vijiji Kumi kwa kila Halmashauri upo katika hatua
mbalimbali za utekelezaji ambapo ujenzi na ukarabati wa miradi ya maji
248 katika Vijiji 270 umekamilika. Pia, jumla ya vituo 10,393 vya
kuchotea maji vinavyohudumia Watu 2,598,250 vimejengwa. Ujenzi wa
miundombinu ya maji kwenye Vijiji 613 upo katika hatua mbalimbali za
utekelezaji na miradi katika Vijiji 374 inafanyiwa tathmini ya zabuni.
Aidha, katika kipindi hicho, vyombo vya watumia maji 373 vimeundwa.
Vilevile, katika kipindi cha miezi sita ya utekelezaji
wa miradi ya maji chini ya BRN! kinachoishia Desemba 2013, Wanavijiji
2,390,000 wamefikishiwa huduma za maji safi na salama, ikilinganishwa na
Wanavijiji 300,000 hadi 500,000 waliokuwa wakipatiwa huduma za maji
safi Vijijini kabla ya mpango huo kuanza.
99. Mheshimiwa Spika,
Serikali pia inatekeleza Awamu ya Pili ya mradi wa maji wa Chalinze
ambao utatoa huduma ya maji kwa Vijiji 47 vyenye Watu 197,684 katika
Wilaya za Bagamoyo, Pwani. Hadi kufikia Desemba 2013, utekelezaji wa
mradi ulikuwa umefikia Asilimia 88. Vilevile, Serikali inaendelea na
ujenzi wa mabwawa katika maeneo mbalimbali hususan maeneo kame kwa lengo
la kuwapatia wananchi huduma ya maji kwa matumizi ya nyumbani na
mifugo. Ujenzi wa mabwawa ya Iguluba (Iringa Vijijini) na Wegero
(Butiama, Mara) na ukarabati wa Bwawa la Ingodini –Longido Arusha
umekamilika. Ujenzi wa mabwawa ya Kawa (Nkasi, Rukwa), Sasajila
(Chamwino, Dodoma), Mwanjoro (Meatu, Shinyanga) na Kidete (Kilosa,
Morogoro) umekamilika kwa zaidi Asilimia 75. Mabwawa yaliyokamilika kwa
wastani wa Asilimia 50 ni Habiya (Itilima, Simiyu), Sekeididi (Kishapu,
Shinyanga) na Matwiga (Chunya, Mbeya). Natoa wito kwa Wananchi kulinda
vyanzo na miundombinu ya maji. Vilevile, natoa wito kwa Viongozi katika
Mamlaka za Serikali za Mitaa kusimamia vyema Vyombo vya watumia maji ili
miradi hii iwe endelevu.
Huduma ya Maji Mijini
100. Mheshimiwa Spika,
Mamlaka za Majisafi na Usafi wa Mazingira katika miji mikuu ya mikoa
zinatoa huduma ya maji kwa wakazi wake kwa wastani wa Asilimia 80.
Katika Jiji la Dar es Salaam, upatikanaji wa huduma ya maji utaongezeka
zaidi mara baada ya upanuzi na ujenzi wa bomba kuu la maji kutoka Ruvu
Juu na Ruvu Chini kukamilika. Kazi ya kulaza bomba la maji kutoka mtambo
wa Ruvu Chini hadi Dar es Salaam lenye urefu wa kilometa 55.5
umekamilika kwa Asilimia 60.5 na kazi ya kupanua mtambo wa Ruvu Juu na
kulaza bomba hadi Dar es Salaam imeanza mwezi Februari, 2014. Katika
mwaka 2014/2015, Serikali itaanza kutekeleza Mpango Maalum wa Kuhifadhi
na Kutunza Vyanzo vya Maji wa Miaka Mitano (2014/2015 – 2018/2019) ili
kuimarisha ushirikishwaji wa wadau katika shughuli za uhifadhi, utunzaji
na ulinzi wa rasilimali za maji. Aidha, Serikali itaendelea kutekeleza
Mradi wa Maji kwa Vijiji Kumi kwa kila Halmashauri.
UTAMADUNI NA MICHEZO
Utamaduni
101. Mheshimiwa Spika, katika
mwaka 2013/2014, Serikali imeendelea na urasimishaji wa tasnia za
filamu na bidhaa zake kwa kushirikiana na taasisi zinazohusika ili
kuiongezea Serikali mapato na kulinda kazi za wasanii. Moja ya hatua
zilizochukuliwa ni kufanyika kwa operesheni ya kufuatilia matumizi ya
stempu za kodi za Mamlaka ya Mapato Tanzania ambapo zaidi ya stempu
milioni moja za bidhaa za filamu zimetolewa. Jumla ya operesheni nane za
kufuatilia filamu zilizoingia sokoni kinyume na taratibu zimefanyika na
jumla ya filamu 301 zilibainika kuingia sokoni kinyume na taratibu na
wahusika kuchukuliwa hatua. Natoa wito kwa mamlaka husika kuhakikisha
kuwa zoezi hili linafanyika Nchi nzima na linakuwa endelevu. Vilevile,
natoa rai kwa wananchi kununua bidhaa za filamu zenye viwango zinazothibitishwa na uwepo wa stika maalumu.
Michezo
102. Mheshimiwa Spika, katika
mwaka 2013/2014, Serikali kwa kushirikiana na Wadau wa maendeleo ya
michezo imetekeleza Mradi wa Kimataifa wa Kukuza Ari ya Michezo wenye
lengo la kuimarisha ushiriki wa vijana na watoto katika michezo bila
kujali jinsia ama uwezo. Kutokana na juhudi hizo, katika mashindano ya
Kombe la Dunia kwa Watoto wa Mitaani yaliyofanyika Nchini Brazil mwezi
Aprili 2014, Timu yetu ya Watoto wa Mitaani ya Mkoani Mwanza imetwaa
Kombe la Dunia la Watoto wa Mitaani. Napenda kuwapongeza Vijana hao kwa
kuiletea Nchi yetu heshima kubwa. Vijana hao wanapaswa kuendelezwa ili
waweze kutuwakilisha vyema katika mashindano mengine ya Kimataifa.
Aidha, mafanikio hayo yawe chachu ya kuendeleza michezo mingine Nchini.
Ni muhimu tukakumbuka kwamba vipaji vya michezo viko vingi na
vimejificha. Kinachotakiwa ni kufanyika jitihada za dhati kuviibua na
kuvitumia. Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo ishirikiane
kwa karibu na Maafisa Utamaduni wa Halmashauri zote nchini kubuni
mkakati maalum wa kuibua vipaji vya michezo kuanzia ngazi ya kitongoji.
USHIRIKIANO WA KIMATAIFA NA KIKANDA
103. Mheshimiwa Spika, Nchi yetu imeendelea kufanya vyema katika medani za Kimataifa kufuatia kazi nzuri inayofanywa na Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Napenda
kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa kutunukiwa Tuzo tarehe 9 Aprili, 2014
kwa kuwa Kiongozi Mwenye Mchango Mkubwa Zaidi katika Maendeleo Barani
Afrika kwa mwaka 2013, huko Jijini Washington, Marekani. Tuzo hiyo ya
heshima kubwa inayotolewa kwa Viongozi wa Afrika ambao hutoa mchango
mkubwa zaidi wa kiuchumi na kijamii kila mwaka kwa watu wao, hutolewa na
jarida maarufu la kimataifa la African Leadership Magazine Group. Tuzo
hiyo imetolewa kutokana na mwelekeo wake thabiti na wenye mafanikio
makubwa kwa masuala ya utawala bora. Vilevile, napenda
kumpongeza Dkt. Stergomena Lawrence Tax kwa kushinda kinyang’anyiro cha
nafasi ya Katibu Mtendaji wa Jumuiya ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC)
mwezi Agosti, 2013. Namtakia kila la kheri katika kutekeleza majukumu
yake na kuendelea kupeperusha vyema bendera ya Nchi yetu.
104. Mheshimiwa Spika, tarehe
1 hadi 2 Julai, 2013 Watanzania walipokea ugeni mkubwa wa Kiongozi wa
Taifa la Marekani, Rais Barack Obama aliyeambatana na mamia ya
Wafanyabiashara. Kupitia ziara hiyo, Marekani ilizindua Mpango wa Umeme Afrika (Power Africa), ambao
utaongeza kwa mara mbili upatikanaji wa umeme katika Bara la Afrika.
Tanzania ni miongoni mwa Nchi zitakazonufaika na Mpango huo unaolenga
kuzalisha zaidi ya Megawati 8,000 za umeme katika Nchi za Afrika Kusini
mwa Jangwa la Sahara. Serikali ya Marekani imeahidi kutoa zaidi ya Dola
za Marekani Bilioni 7. Kampuni za Marekani, Ulaya, Asia na Afrika
ziliahidi kutoa zaidi ya Dola za Marekani Bilioni 9 kwa ajili ya Mradi
huo kwa miaka mitano ijayo. Nchi yetu pia kupitia ziara hiyo ilipata
fursa ya kujitangaza na kujiweka katika nafasi nzuri ya kukuza Uchumi,
Biashara, Utalii na Uwekezaji.
105. Mheshimiwa Spika,
utekelezaji mzuri wa Malengo ya Maendeleo ya Milenia ambayo yatafikia
ukomo wake mwaka 2015 umeifanya Nchi yetu izidi kung’ara Kimataifa na
hivyo kuwa kati ya Nchi 30 zitakazounda kikundi kazi kitakachoandaa
Malengo ya Maendeleo Endelevu yatakayotekelezwa baada ya mwaka 2015.
Aidha, katika Mkutano wa Jukwaa la Uchumi (WEF) uliofanyika mjini
Davos, Uswisi mwezi Februari 2014, Mpango wa WEF wa kuvutia uwekezaji
katika miundombinu muhimu ulijadiliwa ambapo Bandari ya Dar es Salaam
ilichaguliwa kuwa miongoni mwa Bandari zitakazonufaika na Mpango huo.
Tayari Timu ya Wataalam imefika Nchini kufanya tathmini ya awali ya
mradi huo. Aidha, Kongamano maalum lililohusisha Nchi kadhaa
zinazohusika na Mpango wa Uchukuzi wa Ukanda wa Kati lilifanyika tarehe
15 Aprili, 2014. Kongamano hilo lilizinduliwa na Mheshimiwa Dkt. Jakaya
Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Vita Dhidi ya Rushwa
106. Mheshimiwa Spika, katika
mwaka 2013/2014, Serikali imeendelea na mapambano dhidi ya rushwa kwa
kutoa elimu kuhusu rushwa, athari zake na wajibu wa wananchi katika
mapambano dhidi ya rushwa kupitia semina, midahalo, maonesho ya kitaifa,
vipindi vya Radio na Televisheni pamoja na machapisho. Aidha, tuhuma
3,872 zikiwemo tuhuma mpya 679 zilichunguzwa, ambapo hadi sasa uchunguzi
wa tuhuma 589 umekamilika. Majalada 4 ya tuhuma za rushwa kubwa
yalifikishwa kwa Mkurugenzi wa Mashtaka kwa hatua za kisheria. Katika
mwaka 2014/15, TAKUKURU itaendelea kuchunguza tuhuma 3,193 zilizopo na
mpya zitakazojitokeza na kuendesha kesi 635 zilizopo Mahakamani hivi
sasa na zitakazoendelea kufunguliwa. Vilevile, itaendelea na uchunguzi
wa tuhuma zitokanazo na taarifa za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za
Serikali za mwaka 2011/2012.
107. Mheshimiwa Spika, Serikali
imetekeleza Awamu ya Kwanza ya Mpango wa Uendeshaji wa Shughuli za
Serikali kwa Uwazi. Lengo ni kuendesha shughuli zake kwa uwazi zaidi ili
kuimarisha utoaji wa huduma kwa Wananchi, kusikiliza Wananchi,
kupambana na rushwa na kujenga dhana ya kuaminika kwa Wananchi. Katika
mwaka 2013/2014 Serikali imechapisha, Bajeti yake kwa lugha
rahisi za Kiswahili na Kingereza na kuiweka katika Tovuti ya Wizara ya
Fedha ili iweze kusomwa na Wananchi wote. Aidha, imeanzisha Tovuti ya
Serikali (Government Portal) yenye anuani ya http://www.egov.go.tz/ na
Kituo Maalum cha Mawasiliano kwa masuala ya OGP Nchini pamoja na
kuimarisha Tovuti ya Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za
Serikali. Katika mwaka
2014/2015, Serikali itaanza kutekeleza Awamu ya Pili ya Mpango huo kwa
kufanya shughuli mbalimbali ikiwa ni pamoja na kutunga Sheria ya Uhuru
wa Habari; kukamilisha na kuimarisha Mfumo wa Kuweka Wazi Taarifa na
Takwimu kwenye Tovuti.
Maafa
108. Mheshimiwa Spika,
Nchi yetu imeendelea kukumbwa na Maafa ambayo yameleta athari kwa
Wananchi na mali zao. Katika mwaka 2013/2014, ukame umesababisha
upungufu wa Chakula kwa Watu 828,063 katika Wilaya 54 za Mikoa 14
Nchini. Serikali ilitoa tani 26,663 za chakula cha msaada chenye thamani
ya Shilingi Bilioni 15.2 pamoja na Shilingi Bilioni 2.2 kwa ajili ya
kukisafirisha hadi kwa walengwa. Mafuriko makubwa pia yametokea katika
maeneo mengi hususan, Mikoa ya Morogoro, Dar es Salaam, Pwani, Mbeya,
Tanga, Kilimanjaro, Lindi, Dodoma, Iringa, Kagera na Mara na kusababisha
vifo, majeruhi na uharibifu wa mali na miundombinu. Katika kukabiliana
na athari zilizojitokeza, Serikali na wadau mbalimbali imetoa misaada
ya dharura ya kibinadamu kwa waathirika na imechukua hatua za kurejesha
miundombinu ya maji, elimu, afya, barabara na madaraja na umeme. Nitumie
fursa hii kulipongeza Jeshi la Wananchi wa Tanzania, TANROADS,
Wakandarasi, Wadau mbalimbali pamoja na Wananchi wote kwa kazi kubwa
waliyoifanya na misaada waliyoitoa kwa Waathirika wa Maafa
yaliyojitokeza. Napenda kurudia wito wangu kwa Wananchi wote
wanaoishi katika maeneo hatarishi hasa mabondeni, kutii maagizo ya
Serikali kuondoka katika maeneo hayo na kuhamia maeneo yaliyoainishwa
ambayo ni salama kwa maisha yao.
Aidha,
ninatoa wito kwa Wananchi wote kufuata Sheria ili kuepuka uvunjifu wa
amani na kusababisha maafa kutokana na mapigano, hasa ya kugombea ardhi
na malisho.
109. Mheshimiwa Spika, mafunzo
ya kuijengea jamiii uwezo wa kukabiliana na maafa ikiwemo kupokea na
kugawa misaada wakati wa maafa yametolewa katika ngazi za Mkoa na Wilaya
kwa Mikoa ya Mara, Geita, Singida, Simiyu, Shinyanga, Manyara,
Kilimanjaro, Dodoma, Tabora na Arusha. Pia, Mipango ya Kujiandaa
Kukabili Maafa katika Halmashauri za Wilaya za Maswa, Bariadi, Meatu,
Mwanga na Same imeandaliwa. Katika mwaka 2014/2015, Serikali itafanya
Tathmini ya Maafa yanayoweza kutokea na uwezo wa kuyakabili pamoja na
mipango ya kujiandaa na kukabiliana na maafa katika Halmashauri za
Wilaya za Mtwara Mjini, Mtwara Vijijini, Masasi, Mvomero na Kilosa.
Vilevile, itaanza Ujenzi wa Kituo cha Dharura cha Utendaji na
Mawasiliano (Emergency Operation and Communication Centre) katika eneo
la Mabwepande Wilayani Kinondoni.
Udhibiti wa Dawa za Kulevya
110. Mheshimiwa Spika, pamoja
na juhudi kubwa zinazofanywa na Serikali dhidi ya uingizaji na
utumiaji wa Dawa za Kulevya, tatizo hili limeendelea kuwa kubwa kutokana
na wanaojihusisha na Dawa hizo kubuni mbinu mpya za kukwepa mkono wa
Sheria. Katika mwaka 2013/2014, Serikali imeendeleza
mapambano dhidi ya dawa hizo kwa kuelimisha Umma kuhusu madhara ya dawa
hizo. Serikali pia imepanua huduma za matibabu kwa watumiaji wa dawa
za kulevya kwa kutumia dawa ya Methadone. Huduma za tiba hiyo
zinapatikana katika kliniki zilizopo katika Hospitali ya Muhimbili,
Mwananyamala na Temeke. Vilevile, imeendesha operesheni zilizowezesha
kilo 12,820 za mirungi kukamatwa, ekari 127 za mashamba ya bangi, na
kilo 3,445 za mbegu za bangi na magunia 1,107 ya bangi kavu kuteketezwa.
Pia, kilo 236.5 za Heroin na kilo tatu za Cocaine zilikamatwa.
111. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2014/2015, Serikali itaendelea kutoa elimu kwa umma na huduma za matibabu kwa watumiaji wa Dawa za Kulevya. Serikali pia itaendelea kuwachukulia hatua kali wahalifu wote wanaojihusisha na biashara haramu ya Dawa za Kulevya. Vilevile, ili kuondoa mianya inayojitokeza katika kupambana na uhalifu utokanao na biashara ya Dawa za Kulevya, Serikali itakamilisha kutunga Sheria mpya ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya itakayowezeshakuimarisha mapambano dhidi ya tatizo hilo.
Mazingira
112. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/14, Serikali
imeandaa Mpango Kazi wa Taifa wa Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira wa
mwaka 2013 hadi 2018, utakaoziwezesha sekta zote kujumuisha masuala ya
mazingira kwenye majukumu yao na mipango yao ya maendeleo. Sambamba na
hatua hiyo, Serikali iliratibu utekelezaji wa
miradi ya kuhimili mabadiliko ya tabianchi. Moja ya miradi hiyo ni Mradi
wa Kuhimili Mabadiliko ya Tabianchi (African Adaptation Programme) wenye thamani ya Dola za Marekani Milioni 2.5 unaofadhiliwa na Serikali ya Japan.
Fedha
hizo zimetumika kuanzisha miradi ya majaribio ya kuhimili mabadiliko ya
tabianchi katika Wilaya za Misenyi (Kagera), Mbinga (Ruvuma), Igunga
(Tabora) na Zanzibar. Mradi mwingine ni Mradi wa Vijiji vya Mfano vya
Mazingira (Eco-Village) wenye thamani ya Euro Milioni 2.2
unaofadhiliwa na Jumuiya ya Ulaya chini ya utaratibu ujulikanao kama
Climate Change Alliance Initiative. Hadi sasa mradi umeainisha Vijiji
vya mfano na kutekeleza miradi ya kuhimili mabadiliko ya tabianchi
katika Mikoa ya Morogoro, Kigoma, Dodoma na Pemba. Katika mwaka 2014/2015, Serikali itaendelea kutoa elimu ya hifadhi ya mazingira kwa umma kuhusu Sera, Sheria na Mikataba ya Kimataifa ya kuhusu Mazingira pamoja na kuendelea kuhamasisha kampeni ya upandaji miti Nchi nzima.
Udhibiti wa UKIMWI
113. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/2014, Serikali
imeanza kutekeleza Mkakati wa Tatu wa Taifa wa Kudhibiti UKIMWI wa
mwaka 2013 hadi 2018. Mkakati huo una shabaha ya kufikia Malengo ya
Kimataifa ya Sifuri Tatu, ikimaanisha Kutokuwa na Maambukizi Mapya,
Kutokuwa na Vifo Vitokanavyo na UKIMWI na Kuondokana kabisa na
Unyanyapaa na Ubaguzi. Hadi Desemba 2013, kati ya watu 1,261,931
walioandikishwa kuwa wanaishi na VVU, watu 669,730 walianzishiwa dawa.
Aidha, ili kurahisisha upimaji wa VVU, Serikali imeipatia Mikoa ya
Mbeya, Ruvuma, Katavi na Rukwa mashine kubwa za kupima kiwango cha kinga
(CD4). Serikali pia imeidhinisha kuanzishwa kwa Mfuko wa UKIMWI,
utakaojulikana kama AIDS Trust Fund. Kuanzishwa kwa Mfuko huo
kutawezesha kupunguza utegemezi wa Wahisani kwenye shughuli za UKIMWI
kwa wastani wa Asilimia 40.
114. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2014/2015, Serikali itaendelea
kuimarisha kampeni za uraghibishaji zinazolenga mabadiliko ya tabia ili
kuachana na mila na desturi hatarishi. Vilevile, Serikali imepanga
kuimarisha kampeni za kinga kwa vijana wenye umri wa kuanzia miaka
15 hadi 24 dhidi ya maambukizi ya VVU kwa kutoa elimu. Juhudi zaidi
zitaelekezwa kwenye mikoa 10 yenye maambukizo zaidi ya wastani wa
Kitaifa wa Asilimia 5.1. Mikoa hiyo ni Njombe (14.8), Iringa (9.1),
Mbeya (9.0), Shinyanga (7.4), Ruvuma (7.0), Dar es Salaam (6.9). Rukwa
(6.2), Katavi (5.9), Pwani (5.9) na Tabora (5.1). Aidha, Serikali itakamilisha maandalizi ya Sheria ya Mfuko wa UKIMWI.
Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu
115. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/2014, Serikali imeendeleza miundombinu
muhimu katika Manispaa ya Dodoma. Ujenzi wa Barabara zenye urefu wa
kilomita 47.55 kwa kiwango cha lami katika maeneo ya Kisasa,
Chang’ombe, Kikuyu, Area A pamoja na eneo la Uwekezaji la Njedengwa
umekamilika. Aidha, ujenzi wa mitaro ya maji ya mvua yenye urefu wa
kilomita 6.4 katika eneo la Nkuhungu na Mwangaza umekamilika. Serikali
pia imefungua barabara zenye urefu wa kilomita 105 kwenye maeneo
yaliyopimwa ya Miganga, Iyumbu na Ndachi. Katika mwaka 2014/2015,
Serikali itajenga mitaro ya maji ya mvua katika maeneo ya Ilazo, Kisasa
na Ipagala na kupima viwanja vipya 1,850. Pia ,Serikali itaandaa mpango
wa matumizi ya ardhi katika maeneo ya Mkonze Mashariki, C-centre,
Nkuhungu na maeneo yanayozunguka Chuo Kikuu cha Dodoma.
HITIMISHO
116. Mheshimiwa Spika, kwa
muhtasari nimeelezea baadhi ya shughuli ambazo zimetekelezwa na
Serikali katika mwaka 2013/2014. Aidha, nimetoa Mwelekeo wa Kazi
zitakazotekelezwa katika mwaka 2014/2015. Kwa kuhitimisha, napenda
kusisitiza mambo yafuatayo:
a. Uchumi
wetu unakua kwa kasi nzuri, kwa mfano katika mwaka 2011 ulikua kwa
asilimia 6.4, mwaka 2012 ulikua kwa asilimia 6.9 na mwaka 2013 kwa
asilimia 7.0. Ukuaji huu ni mkubwa ikilinganishwa na Nchi nyingine za
Afrika, Kusini mwa Jangwa la Sahara ambapo Wastani wa ukuaji wa uchumi
kwa nchi hizo ulikuwa asilimia 4.6 mwaka 2011, asilimia 3.5 mwaka 2012
na asilimia 4.5 mwaka 2013. Takwimu zinaonesha pia kwamba kiwango cha
ukuaji wa uchumi wa Tanzania ni cha juu ikilinganishwa na wastani wa
ukuaji wa uchumi kwa Nchi za Afrika Mashariki. Kwa mfano, uchumi wa
Kenya ulikua kwa asilimia 4.4 mwaka 2011, asilimia 4.6 mwaka 2012 na
asilimia 5.0 mwaka 2013. Uchumi wa Uganda ulikua kwa asilimia 6.6 mwaka
2011, asilimia 4.6 mwaka 2012 na asilimia 6.3 mwaka 2013. Takwimu hizo
zinadhihirisha kwamba uchumi wetu unaendelea kuimarika ikilinganishwa na
nchi nyingine, jambo tunalopaswa kujivunia. Mabadiliko makubwa
yanayoonekana Nchini katika sekta za mawasiliano, ujenzi, viwanda na
biashara ni matokeo ya ukuaji huu wa uchumi. Tunahitaji kufanya kazi kwa
bidii na maarifa ili kuhakikisha kwamba ukuaji huu unakuwa endelevu na
kuelekeza juhudi zaidi katika sekta nyingine hususan kilimo, ufugaji na
uvuvi kwani ndizo zinazotegemewa na Watanzania wengi.
b. Tumeadhimisha
Miaka 50 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar kwa amani na utulivu.
Muungano huu ni wa kipekee na wa kupigiwa mfano duniani kote. Aidha, ni
kielelezo kamili cha umoja, mshikamano na upendo miongoni mwa wananchi
jambo lililowezesha kuwepo kwa amani na usalama Nchini. Muungano
umetuletea maendeleo makubwa katika miaka 50 ya uhai wake. Ni wajibu
wetu kuendelea kuenzi, kulinda na kudumisha Muungano huu kwa nguvu zetu
zote.
c. Tumeingia
katika kipindi muhimu katika historia ya Nchi yetu ambapo Bunge Maalum
la Katiba limeanza mjadala wa kutunga Katiba Mpya. Ni matumaini yangu
kuwa Bunge Maalum litakamilisha kazi ya kuandaa Rasimu ya Tatu
itakayopelekwa kwa Wananchi kwa ajili ya kupigiwa kura ya maoni.
Ninawasihi Wananchi wawe watulivu katika kipindi hiki maalum na
kufuatilia kwa makini mjadala wa Katiba kwa kupima mawazo yanayotolewa
wakati wa mjadala ili hatimaye kupiga kura ya maoni vyema. Ni matarajio
yangu kuwa Katiba Mpya itakayopatikana itatusaidia kuleta mabadiliko
makubwa kiuchumi, kijamii na kisiasa kwa kupata muafaka wa kitaifa wa
uendeshaji wa Nchi yetu katika miaka mingi ijayo.
d. Sote
tumeshuhudia juhudi za Serikali katika kuimarisha upatikanaji na
usambazaji wa nishati Nchini. Mradi wa Ujenzi wa Mitambo ya Kusafisha
Gesi Asilia na Bomba la kusafirishia gesi kutoka Mtwara hadi Dar es
Salaam unaoendele kujengwa utasaidia sana kuongeza umeme wa gharama
nafuu kwenye Gridi ya Taifa. Natoa wito kwa wananchi wote kushirikiana
na Serikali kufanikisha miradi hiyo kwa kulinda miundombinu yake pamoja
na kutumia fursa za kiuchumi zinazotokana na uwepo wa miradi hiyo.
117. Mheshimiwa Spika, kabla
ya kumaliza Hotuba yangu, nimwombe Mheshimiwa Hawa Abdulrahman Ghasia,
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu - Tawala za Mikoa na Serikali za
Mitaa atoe maelezo ya Mapitio ya Kazi zilizofanyika mwaka 2013/2014 na
Mwelekeo wa Kazi za Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kwa mwaka
2014/2015.
SHUKRANI
118. Mheshimiwa Spika, nitumie
fursa hii sasa kuwashukuru Mawaziri na Naibu Mawaziri kwa ushirikiano
walionipa katika kipindi hiki. Aidha, nawashukuru Watumishi wote wa
Serikali na Taasisi zake chini ya Uongozi wa Katibu Mkuu Kiongozi,
Balozi Ombeni Yohana Sefue kwa kusimamia Shughuli za Serikali vizuri.
Nawashukuru Watanzania wote na Washirika wetu wa Maendeleo kwa michango
yao ambayo imewezesha Serikali kutoa huduma mbalimbali kwa Wananchi.
119. Mheshimiwa Spika, napenda kuwashukuru Mheshimiwa
Dkt. Mary Michael Nagu, Mbunge wa Hanang na Waziri wa Nchi
(Uwekezaji na Uwezeshaji); Mheshimiwa William Vangimembe Lukuvi, Mbunge
wa Ismani na Waziri wa Nchi (Sera, Uratibu na Bunge); Mheshimiwa Hawa
Abdulrahman Ghasia, Mbunge wa Mtwara Vijijini na Waziri wa Nchi, Tawala
za Mikoa na Serikali za Mitaa; Mheshimiwa Aggrey Joshua Mwanri, Mbunge
wa Siha, Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na
Serikali za Mitaa; na Mheshimiwa Majaliwa Kassim Majaliwa, Mbunge wa
Ruangwa, Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali
za Mitaa (Elimu) kwa ushirikiano walionipa katika utekelezaji wa
majukumu ya Ofisi ya Waziri Mkuu. Nawashukuru pia Wakuu wa Mikoa na
Wilaya kwa kusimamia shughuli za Serikali vyema katika Mikoa na
Wilaya.
120. Mheshimiwa Spika,
ninawashukuru vilevile Wafanyakazi wote wa Ofisi ya Waziri Mkuu, chini
ya Uongozi wa Makatibu Wakuu, Dkt. Florens M. Turuka na Bwana Jumanne A.
Sagini, kwa kazi nzuri wanayoifanya. Ninawashukuru Naibu Makatibu
Wakuu, Bibi Regina L. Kikuli, Bwana Kagyabukama E. Kiliba, Bwana Zuberi
M. Samataba, Naibu Katibu Mkuu (Elimu), Dkt. Deo M. Mtasiwa, Naibu
Katibu Mkuu (Afya) kwa ushauri wao wa kitaalam ambao wamenipa mimi na
Waheshimiwa Mawaziri wa Nchi katika kipindi hiki. Ninawashukuru kwa
kukamilisha maandalizi yote ya Makadirio ya Matumizi ya Fedha ya Ofisi
ya Waziri Mkuu kwa mwaka 2013/2014.
121. Mheshimiwa Spika, ninapenda kumshukuru kwa
dhati Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania kwa uongozi wake mahiri na maelekezo anayonipatia
katika kutekeleza majukumu yangu. Pia, ninamshukuru Mheshimiwa Dkt.
Mohamed Gharib Bilal, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
na Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa
Baraza la Mapinduzi kwa ushirikiano wao mkubwa. Vilevile, ninawashukuru
Waheshimiwa Wabunge wote, Viongozi wote wa Kitaifa na wa ngazi nyingine
zote kwa ushirikiano wanaonipa katika kutekeleza majukumu yangu.
Ninawashukuru sana Wapiga Kura wangu wa Jimbo la Katavi kwa ushirikiano
wanaonipa katika kuleta maendeleo ya Jimbo letu.
122. Mheshimiwa Spika, kwa
namna ya pekee, naomba uniruhusu kutumia fursa hii kumshukuru sana Mama
Tunu Pinda na Familia yangu yote kwa kuniombea, kunitia moyo na
kunivumilia kwa kila hali katika utekelezaji wa majukumu yangu ya
Kitaifa. Ninawashukuru sana!!
MAKADIRIO YA
MATUMIZI YA FEDHA YA OFISI YA WAZIRI MKUU, OFISI YA WAZIRI MKUU -
TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA NA OFISI YA BUNGE YA MWAKA
2014/2015
123. Mheshimiwa Spika, kwa mwaka 2014/2015, Ofisi ya Waziri Mkuu na Taasisi zake inaliomba Bunge lako Tukufu kuidhinisha jumla ya Shilingi Bilioni Mia Moja na Tano, Milioni Mia Tano Ishirini na Saba na Ishirini na Nne Elfu (105,527,024,000). Kati ya fedha hizo, Shilingi Bilioni Themanini, Milioni Mia Saba Sitini na Tano na Ishirini na Tisa Elfu (80,765,029,000) ni za Matumizi ya Kawaida na Shilingi Bilioni Ishirini na Nne, Milioni Mia Saba Sitini na Moja, Mia Tisa Tisini na Tano Elfu (24,761,995,000) ni za Miradi ya Maendeleo.
124. Mheshimiwa Spika, Ofisi ya Waziri Mkuu - Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Taasisi zake inaombewa jumla ya Shilingi Bilioni Mia Nne Sabini na Tisa, Milioni Mia Mbili Ishirini na Nne na Sitini na Mbili Elfu (479,224,062,000). Kati ya fedha hizo, Shilingi Bilioni Mia Mbili Sabini na Tatu, Milioni Sitini na Tano, Mia Nane Tisini na Tano Elfu (273,065,895,000) ni za Matumizi ya Kawaida na Shilingi Bilioni Mia Mbili na Sita, Milioni Mia Moja Hamsini na Nane, Mia Moja Sitini na Saba Elfu (206,158,167,000) ni za Miradi ya Maendeleo.
125. Mheshimiwa Spika, Ofisi za Wakuu wa Mikoa zinaombewa jumla ya Shilingi Bilioni Mia Mbili Sitini na Saba, Milioni Mia Tisa na Tisa, Mia Tatu Tisini Elfu (267,909,390,000). Kati ya fedha hizo, Shilingi Bilioni Mia Mbili na Mbili, Milioni Mia Tatu na Kumi, Mia Mbili Themanini na Sita Elfu (202,310,286,000) ni za Matumizi ya Kawaida na Shilingi Bilioni Sitini na Tano, Milioni Mia Tano na Tisa, Mia Moja na Nne Elfu (65,509,104,000) ni za Miradi ya Maendeleo. Halmashauri zote zinaombewa jumla ya Shilingi Trilioni
Nne, Bilioni Mia Mbili Thelathini na Moja, Milioni Mia Nne Arobaini na
Mbili, Mia Tisa Sabini na Nne Elfu (4,231,442,974,000). Kati ya fedha hizo, Shilingi Trilioni Tatu na Bilioni Tisini, Milioni Mia Tatu Sabini, Mia Tatu na Nane Elfu (3,090,370,308,000) ni za Matumizi ya Kawaida na Shilingi Bilioni Mia Sita Themanini na Mbili, Milioni Mia Sita na Mbili na Arobaini na Nne Elfu (682,602,044,000) ni za Miradi ya Maendeleo. Aidha, jumla ya Shilingi Bilioni Mia Nne Hamsini na Nane, Milioni Mia Nne Sabini, Mia Sita Ishirini na Mbili Elfu (458,470,622,000) ni mapato ya ndani ya Halmashauri zote.
126. Mheshimiwa Spika, Ofisi ya Bunge la Jamhuri ya Muungano inaombewa jumla ya Shilingi Bilioni Mia Moja Thelathini na Mbili, Milioni Mia Sita Tisini na Sita, Mia Nane Tisini na Nne Elfu (132,696,894,000) kwa ajili ya Mfuko wa Bunge ambapo Shilingi Bilioni Mia Moja Ishirini na Tatu, Milioni Mia Tisa Arobaini na Moja, Mia Nne Hamsini na Tano Elfu (123,941,455,000) ni za Matumizi ya Kawaida na Shilingi Bilioni Nane, Milioni Mia Saba Hamsini na Tano, Mia Nne Thelathini na Tisa Elfu (8,755,439,000) ni za Miradi ya Maendeleo.
MUHTASARI
127. Mheshimiwa Spika,
kwa muhtasari, naomba sasa Bunge lako Tukufu likubali kuidhinisha
Makadirio ya Matumizi ya Fedha kwa mwaka 2014/2015 ya jumla ya Shilingi Trilioni Tano, Bilioni Themanini na Nne, Milioni Mia Moja na Tatu, Mia Nne Hamsini Elfu (5,084,103,450,000) kwa ajili ya Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Waziri Mkuu - Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa; na jumla ya Shilingi Bilioni Mia Moja Thelathini na Mbili, Milioni Mia Sita Tisini na Sita, Mia Nane Tisini na Nne Elfu (132,696,894,000) kwa ajili ya Mfuko wa Bunge, ikiwa ni Matumizi ya Kawaida na Fedha za Maendeleo za Ndani na Nje kwa ujumla wake.
128. Mheshimiwa Spika, pamoja
na Hotuba hii, yapo Majedwali ambayo yanafafanua kwa kina Makadirio ya
Matumizi ya Fedha ya Ofisi ya Waziri Mkuu na Taasisi zake, Ofisi ya
Waziri Mkuu - Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Bunge.
129. Mheshimiwa Spika, naomba kutoa Hoja.