KITUO
cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), kimestushwa na kitendo cha Rais
Jakaya Kikwete kuivunja mapema Tume ya Mabadiliko ya Katiba na kusema
haikustahili kuvunjwa wakati Bunge Maalumu la Katiba bado linaendelea.
Kauli hiyo ilitolewa mjini hapa juzi na mjumbe wa Kamati Maalumu ya
Katiba kutoka LHRC, Exavery Lwaitama, alipokuwa akitoa mada kwenye
warsha ya jukwaa la mchakato wa katiba mpya, ulioandaliwa na Mtandao wa
Kufuatilia Sera Mwanza (MPI), na kuwashirikisha viongozi wa asasi na
mashirika mbalimbali kutoka wilaya za Ukerewe, Nyamagana, Ilemela, Magu
za mkoani Mwanza, pamoja na Wilaya ya Karagwe, Kagera.
Lwaitama ambaye pia ni mhadhiri mwandamizi mstaafu wa Chuo Kikuu cha
Dar es Salaam (UDSM), alisema kuvunjwa kwa tume hiyo wakati Bunge la
Katiba halijamalizika, ni kuharibu mwenendo na mchakato mzima wa
Watanzania kupata katiba wanayoitaka.
Alisema haiwezekani Rais Kikwete aivunje tume hiyo kisha majukumu
yake kuchukuliwa na serikali ambayo tangu awali imekuwa ikikataa
kutungwa kwa katiba mpya.
“Utavunjaje tume wakati Bunge la Katiba halijaisha? Sasa hii rasimu
ya katiba inayojadiliwa bungeni itasimamiwa na nani kama tume imevunjwa?
Itawezekanaje isimamiwe na serikali ambayo tangu mwanzo haitaki
kutungwa kwa katiba mpya?
“Tunakumbuka mwaka 2011 Mwanasheria Mkuu wa Serikali (Jaji Fredrick
Werema), na viongozi wengine wa serikali walikataa kutungwa katiba mpya.
Sasa leo rais anaivunja tume, hivi tunategemea kuna upatikanaji wa
katiba hapa?” alihoji Lwaitama.
Wakizungumza katika warsha hiyo, viongozi wa mashirika na asasi hizo,
walisema hawaoni mwelekeo wa Watanzania kupata katiba mpya wanayoitaka,
hivyo wakasema ni bora Bunge hilo likavunjwa, ili kuepusha matumizi
mabaya ya fedha.
Mratibu wa MPI, Jonathan Kassim, alisema wameandaa warsha hiyo ili
kutoa sauti ya pamoja kwa asasi na mashirika hayo kuhusu mwenendo wa
Bunge hilo na kuwaomba wajumbe na serikali kwa ujumla kuwatendea haki
wananchi kwa kupitisha maoni yao.
0 comments:
Post a Comment