Serikali inapenda kuwaarifu waombaji wa nafasi za kazi kwa tangazo la tarehe 27 Novemba, 2013 wa kada za Kilimo, Mifugo, Uvuvi na Udereva kuwa usaili utaanza tarehe 4 Machi, 2014 takriban katika mikoa yote Tanzania Bara na kituo cha Zanzibar.
Katibu wa Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma Bw. Xavier Daudi amesema hayo leo ofisini kwake wakati akiongea na baadhi ya wadau waliomtembelea kwa lengo la kufahamu masuala mbalimbali ya uendeshaji wa mchakato wa ajira serikalini. Amesema usaili huo unaoanza tarehe 4 Machi katika mikoa takribani yote nchini utahusisha jumla ya wasailiwa 6,075 wa fani za Kilimo, Mifugo, Uvuvi na udereva. Amefafanua kuwa vigezo vya kupanga mikoa ya usaili kwa wasailiwa wa kada zisizo za maafisa vimetokana na anwani ambazo waombaji waliwasilisha katika barua zao za maombi husika ya kazi.
Daudi
alibainisha kuwa kila mwombaji aliyekidhi vigezo na kuchaguliwa kwa
ajili ya usaili anapaswa kwenda kufanyia usaili katika mkoa aliopangiwa
kama anwani yake inavyoonyesha katika tangazo kwenye tovuti ya
Sekretarieti ya Ajira, isipokuwa kwa waombaji wa mkoa wa Katavi wao
wataenda kufanyia usaili mkoa wa Rukwa na waombaji waliotumia anwani za
mkoa wa Singida wao watafanyia usaili mkoa wa Manyara kutokana na sababu
zisizozuilika.
Aliongeza
kuwa kwa mwombaji ambae hatazingatia anwani, siku na muda aliopangiwa
na kuamua kwenda mkoa mwingine tofauti na utaratibu uliopangwa ajue wazi
hatasailiwa kwa kuwa ratiba na idadi ya majopo ilishapangwa kwa kila
mkoa na haitabadilishwa ili kuweza kurahisisha kazi hiyo kukamilika kwa ufanisi.
Aidha, amewataka waombaji wote wa tangazo hilo kutembelea tovuti ya Sekretarieti ya Ajira ambayo ni www.ajira.go.tz wao
wenyewe ili kuweza kujua kiundani endapo wamechaguliwa kufanya usaili,
kufahamu tarehe, mahali na muda wa kuanza usaili ili kuepuka usumbufu
usiokuwa na lazima.
Daudi
aliendelea kufafanua kuwa kwa waombaji waliotumia anuani za mkoa wa Dar
es Salaam kwa nafasi ambazo sio za maofisa usaili utafanyika tarehe 11
Machi, 2014. Aidha, kwa nafasi za Maofisa Kilimo, Mifugo na Uvuvi wote
usaili wao utafanyika jijini Dar es Salaam kuanzia tarehe 10 hadi 14
Machi, 2014.
Katibu amewataka
waombaji wote kuhakikisha pindi wanapoenda kwenye usaili wawe
wamejiandaa vya kutosha ikiwemo kubeba nyaraka muhimu hususani vyeti
halisi vya taaluma zao maana vitahitajika kwa ajili ya uhakiki siku ya
usaili. Aidha, amewasihi waombaji wa matangazo mengine ya nafasi za kazi
kuwa na subira wakati uchambuzi ukiendelea na pindi utakapokamilika
wahusika watataarifiwa.
Alimaliza
kwa kuwasisitiza wadau wa Sekretarieti ya Ajira kuwa pindi wanapoona
matangazo ya kazi, ikiwemo kuitwa kwenye usaili au kupangiwa vituo vya
kazi katika vyombo mbalimbali vya habari hususani baadhi ya mitandao ya
kijamii wajiridhishe kwanza kwa kuangalia taarifa hizo katika tovuti ya
Sekretarieti ya Ajira, ili kuepuka taarifa zisizokuwa za kweli ambazo
zimekuwa zikitolewa nyakati nyingine na baadhi ya watu wasio waaminifu
kwa lengo la kupotosha Umma.
BOFYA HAPA
http://www.ajira.go.tz/index.php?option=com_content&view=article&id=168:mifugo
0 comments:
Post a Comment