Vigogo sita ambao wanatajwa kuwa wanajiwinda kwa ajili ya
kuwania urais kupitia CCM katika uchaguzi mkuu ujao, wameitwa mbele ya
Kamati ya Ndogo ya Maadili ya chama hicho, kwa ajili ya kuhojiwa kwa
tuhuma za kukiuka maadili.
Habari ambazo zililifikia gazeti hili jana
zinawataja vigogo hao kuwa ni Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa,
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu), Steven Wassira na
Waziri Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye.
Wengine ni Waziri wa mambo ya Nje na Ushirikiano
wa Kimataifa, Bernard Membe, aliyewahi kuwa Waziri wa Nishati na Madini,
William Ngeleja na Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia,
January Makamba.
“Wote wamepelekewa barua za wito wa kufika mbele
ya Kamati ya Maadili inayoongozwa na Mzee Mangula (Philip, Makamu
Mwenyekiti wa CCM, Bara), ambayo itakutana mjini Dodoma, Februari 14
(kesho kutwa) ,” kilisema chanzo chetu cha habari kutoka Ofisi Ndogo ya
CCM, Lumumba, Dar es Salaam na kuongeza:
“Barua hizo zimesainiwa na Mzee Kinana
(Abdulrahman, Katibu Mkuu wa CCM) mwenyewe na tayari zimeanza kusambazwa
leo (jana) mchana.”
Kamati hiyo ndogo ya maadili, inaundwa na Mangula,
Kinana, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge),
William Lukuvi, Shamsi Vuai Nahodha, Dk Maua Daftari na Naibu Waziri wa
Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Dk Pindi Chana.
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye
jana alithibitisha kuwapo kwa Kikao cha Kamati ya Maadili Februari 14
pamoja na kuitwa kwa baadhi ya wanachama kwa ajili ya kuhojiwa.
Hata hivyo, hakuwa tayari kutaja majina yao wala
idadi ya walioitwa... “Wewe fahamu tu kwamba kikao hicho kitafanyika
tarehe hiyo uliyoitaja, lakini masuala ya majina na idadi ya walioitwa
yatajulikana kwenye kikao, mimi sina kwa sasa,” alisema Nnauye.
Katika siku za karibuni kumekuwa na vita ya maneno
baina ya makada wa chama hicho, wakituhumiana kutangaza mapema kugombea
urais kabla ya ruhusa rasmi ya chama.
Kauli za walioitwa
Jana, gazeti hili lilizungumza na baadhi ya walioitwa na wengi wao walisema hawakuwa wamepokea barua za wito huo.
Sumaye kwa upande wake alisema: “Kwa sasa niko Mwanza na sijapata barua yoyote ya kuitwa katika kikao chochote cha chama.”
Lowassa alipigiwa simu mara kadhaa na kusema kuwa yuko kwenye kikao apigiwe baadaye. Alipigiwa mara sita na kusema alikuwa bado kwenye kikao.
Lowassa alipigiwa simu mara kadhaa na kusema kuwa yuko kwenye kikao apigiwe baadaye. Alipigiwa mara sita na kusema alikuwa bado kwenye kikao.
Membe kwa upande wake alisema: “Kwangu si mara ya
kwanza kuitwa Kamati ya Maadili, ifahamike kwamba unaweza kuitwa kutoa
ushahid, maelezo au ufafanuzi wa jambo lolote unalokuwa umeitiwa.”
Wassira pia alisema hakuwa amepata barua hiyo ya
wito... “Mimi ndiyo nimeshuka kutoka Bunda, sina hiyo barua ya kuitwa
kwenye Kamati ya Maadili. Mwaliko nilionao ni wa kikao cha Kamati Kuu
kesho (leo) ambao mimi ni mjumbe,” alisema Wassira.
Kwa upande wake, Makamba naye alisema alikuwa
hajapata wito huo, wakati Ngeleja hakukanusha au kuthibitisha kupokea
barua hiyo kwa maelezo kwamba yeye siyo msemaji wa CCM, hivyo asingeweza
kuzungumzia suala la kuitwa kwake.
“Kwa kweli wewe fahamu tu kwamba mimi siyo msemaji
wa chama. Chama chetu kina utaratibu wa wasemaji wake, waulize hao
maana watakuwa na taarifa sahihi,” alisema Ngeleja.
Katika hatua nyingine, Nnauye alisema Kamati Kuu
(CC) ya CCM, inakutana Dar es Salaam leo, huku Halmashauri Kuu (NEC) ya
chama hicho ikitarajiwa kukutana Jumamosi na Jumapili wiki hii mjini
Dodoma.
Vikao hivyo pamoja na mambo mengine vinatarajiwa
kujadili ushiriki wa wajumbe wake katika Bunge Maalumu la Katiba ambalo
limepangwa kuanza Februari 18, mwaka huu mjini Dodoma.
0 comments:
Post a Comment