WAZIRI wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna
Tibaijuka, ametangaza kiama kwa wananchi waliojitwalia na kumiliki ardhi
kinyume cha sheria.
Tibaijuka alisema kuanzia wiki ijayo wataendesha operesheni kubwa ya
kubomoa nyumba na majengo ya watu waliojenga kwenye maeneo ya wazi au
yasiyoruhusiwa.
Aliitoa kauli hiyo jana wakati wa ufunguzi wa semina ya wahariri wa
vyombo vya habari kuhusu elimu ya sera na sheria zinazosimamia sekta ya
ardhi.
Katika semina hiyo iliyoandaliwa na wizara yake, Profesa Tibaijuka
alisema kazi ya bomoabomoa hiyo wataifanya kwa weledi mkubwa zaidi na
kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi.
“Tuliweka mabango ya kutoa notisi katika maeneo yote ya wazi
yaliyovamiwa, lakini wahusika walikaidi, sasa tutavunja hayo majumba na
wale waliosema kuwa nimekwisha kisiasa nataka niwahakikishie kwamba
sijaisha,” alisema.
Waziri Tibaijuka pia aliwaonya baadhi ya matajiri wanaotumia mahakama
kuweka pingamizi ili kuzuia wasichukuliwe hatua, akisema safari hii
watafuata taratibu zote za kuvunja kwanza na atakayeshitaki wakutane
mahakamani.
“Hizo kuta nilizoziona maeneo ya Mbezi na maeneo mengine tutazivunja
bila kumwangalia mtu usoni. Hao wenye hati pandikizi wala
hatutabembelezana nao bali tutakutana mahakamani baada ya kuvunja,’’
alitamba waziri huyo.
Kuhusu hatua za kuwachukulia baadhi ya watendaji wa wizara hiyo
wanaokiuka taratibu na kugawa ardhi na hati kinyemela, alisema kuwa
ameweka mfumo mzuri wa kuondoa mianya ya rushwa ili kila kitu kifanyike
kwa uwazi.
“Nilisema kwamba mfumo uliopo sasa si mzuri kwani watendaji wa ardhi
hawako chini ya wizara yetu bali wako chini ya halmashauri (Tamisemi)
ambapo ilikuwa vigumu kuwabana.
“Ili kuwasaidia watendaji hawa wasiingie kwenye mitego ya rushwa,
tumeweka mfumo mzuri ambapo sasa kamishna wa ardhi hataweza kujifungia
mwenyewe ofisini na kuandika hati peke yake bila wenzake kujua anafanya
nini,” alisema.
Alibainisha kuwa kamishna wa ardhi sasa atalazimika kumshirikisha
katibu mkuu na watendaji wengine kuhusu hati anayotaka kuitoa kwa
mhusika.
Waziri Tibaijuka alijisifu kuwa amedumu katika wizara hiyo licha ya
kuwepo kwa mabadiliko ya wizara zaidi ya mara mbili, na hivyo akasema
kuwa atahakikisha pia wasaidizi wake nao wanadumu kwa kufanya kazi kwa
mujibu wa sheria.
Mapema akizungumza katika semina hiyo, Naibu Katibu Mkuu wa wizara
hiyo, Dk. Selassie Mayunga, alisema kuwa hivi sasa wameweka mkakati wa
kupima kila kipande cha ardhi nchini.
“Tutakwenda kijiji kwa kijiji, wilaya kwa wilaya tukianzia Wilaya ya
Mvomero mkoani Morogoro ambapo kila mtu atapimiwa eneo lake na
kukabidhiwa hati yake ya umiliki.
“Katika maeneo ya wafugaji tutaainisha sehemu za majosho na malisho
ili kuondoa usumbufu wa wafugaji kuvamia wakulima. Lengo ni kuhakikisha
migogoro ya ardhi nchini inakomeshwa,” alisema.
Aliongeza kuwa licha ya wizara yake kuwa na nia thabiti ya kutatua na
ikiwezekana kumaliza migogoro ya ardhi nchini, wanakabiliwa na tatizo
la uhaba wa fedha.
Alibainisha kuwa kama wangekuwa wanatengewa bajeti kubwa ya kupima na
kugawa ardhi, matatizo na migogoro mingi inayotokea hivi sasa
isingepata nafasi.
chanzo:Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment