Kadiri siku zinavyokwenda kumekuwapo na ugunduzi wa vitu mbalimbali vinavyochangia kuleta mabadiliko katika jamii.
Mabadiliko hayo yanaweza kuwa hasi au chanya kutegemea na aina ya bidhaa iliyogunduliwa na matumizi yake.
Zipo bidhaa zinazoonekana kuwa na matokeo ya
haraka na mazuri baada ya kutumika, lakini wakati huo huo kuwa na
madhara kiafya kwa mtumiaji.
Nchi nyingi zinazoendelea hasa zilizopo barani
Afrika ikiwamo Tanzania zimekuwa ndizo waathirika wakubwa wa bidhaa
zinaotajwa kuwa na madhara huku vijana wakiwa ndiyo kundi kubwa
linaloathirika.
Sababu za kundi hilo kuathirika zaidi ni kutaka
kwenda na wakati kwa kujaribu kutumia kila bidhaa zinazotoka nje ya nchi
bila kujua madhara yake.
Miongoni mwa bidhaa hizo ni nguo za ndani
zilizoundwa maalumu kwa ajili ya kupunguza unene, pia kutengeneza umbile
la mvaaji katika mwonekano wenye mvuto aupendao.
Nguo hizo zimetengenezwa kwa mtindo wa mbano,
(Skin tight)ambapo ikivaliwa hubana eneo la tumboni hadi kwenye mapaja
na hufanya kazi ya kupunguza unene, zikiufanya mwili kuwa mwembamba
kulingana na nguo husika ilivyo.
Licha ya kufanya kazi hiyo kwa ufanisi na kusaidia
kwa kiasi kikubwa watu wengi kupunguza miili yao, utafiti wa kisayansi
unaonyesha kuwa nguo hizo za ndani huchangia kwa kiwango kikubwa
uwezekano wa mvaaji kupata matatizo ya kiafya.
Utafiti uliofanywa na wataalamu mbalimbali wa
nchini Uingereza, unaonyesha kuwa uvaaji wa nguo hizo unaweza kumfanya
mvaaji kupata maradhi ya mgongo, saratani na kiwango kikubwa cha asidi
mwilini.
Mmoja wa wataalamu wa afya katika Hospitali ya The
London Clinic, Dk Johnson Wilson, anasema kubana kwa nguo hizo katika
eneo la tumbo huzuia mzunguko wa asidi inayozalishwa ndani ya mwili na
kuisababisha kupanda juu, badala ya kushuka chini.
Anasema kuwa hali hiyo inatokana na msukomo
unaotokea kwenye tumbo, hivyo kusababisha mlundikano wa asidi ndani ya
mwili ambayo hupaswa kutoka baada ya kuzalishwa.
“Nguo hii inapovaliwa inatenganisha eneo la
kifuani na tumbo, hivyo asidi inayozalishwa inashindwa kushuka chini na
matokeo yake inashia kwenya usawa wa matiti na kurudi kwenye mrija
unaopitisha chakula,”anasema DkWilson.
Kuhusu hatari ya saratani, Dk Wilson anasema kuwa kulundikana
kwa asidi katika mrija wa chakula, kunamweka mhusika katika hatari ya
kupata saratani ya koo na kinywa.
Anasema kwamba licha ya kuwa siyo watu wengi
walioathirika na uvaaji wa nguo hizo, lakini matokea yake huonekana
baada ya muda mrefu kutokana muda ambao mhusika atavaa nguo hizo.
“Hatari ipo zaidi kwa wanaovaa nguo hizi mara kwa
mara, madhara yake hayawezi kuonekana kwa haraka zaidi, lakini kiafya
kuna hatari ya kutengeneza saratani ya koo kutokana na kuzuia asidi na
kusababishia irudi na kulundikana kwenye mrija unaosafirisha
chakula,”anaonya.
Pamoja na hatari hiyo uvaaji wa nguo hizoi pia
unachangia kusababisha ugonjwa wa ngozi unaotokana na mwili kubanwa
kupita kiasi, hivyo hewa kushindwa kupita.
Dk Wilson anafafanua kuwa ikifikia hatua hiyo,
kuna uwezekano wa kutengeneza mazingira ya bakteria na fangasi kujificha
kwenye mwili hivyo kusababisha mvaaji kupata maradhi ya ngozi yaliyo
magumu kutibika.
Mtaalamu wa ngozi Dk Sam Bunting anasema, kubanwa
kwa ngozi pamoja na joto linalosababishwa na msuguano, vinachangia
kuleta madhara makubwa katika mwili wa binadamu.
“Hali hii inasababisha ugonjwa unaofahamika kwa
jina la kitaalamu kama Intertirgo, ambao huwatokea watu wanaovaa nguo
maalumu za kubana kwa ajili ya kutengeneza maumbile,”anasema.
Nguo hizo pia huchangia kuifanya misuli ya tumbo
kuwa dhaifu, kutokana na kubanwa muda mwingi, hata inapoachwa huru
inashindwa kuwa na nguvu yake ya kawaida.
“Kwa asili misuli ya tumbo haina nguvu na
unapoibana kwa muda mrefu unaisababishia kushindwa kufanya kazi yake kwa
ufanisi, hivyo hulegea na kuwa dhaifu zaidi hata inapofunguliwa au
kutolewa nguo inayobana,”anasema.
Kwa upande mwingine, mtaalamu wa misuli Dk Robert
Shanks anasema kuwa nguo hizo zinachangia pia kusababisha maumivu ya
mgongo kwa mvaaji.
Anasema nguo hiyo inapovaliwa, kunakuwapo na ugumu
kwa viungo vya mgongo kujongea kwa urahisi, hivyo kusababisha maumivu
ya mgongo mara kwa mara.
“Viungo na mifupa iliyopo kwenye mgongo inapaswa
kujongea, lakini kuibana kupita kiasi kutasababisha kushindikana kwa
hali hiyo hivyo mvaaji lazima atakumbana na maumivu ya mgongo mara kwa
mara
Pamoja na madhara hayo, nguo hizi pia huweza kusababisha kizuizi
katika mzunguko wa damu kwani mishipa inayotakiwa kufanyakazi hiyo
inashindwa, kutokana na maeneo ya tumbo hadi kwenye nyonga yanakuwa
yamebanwa.
“Ni vigumu mzunguko wa damu kufanyika vizuri
katika maeneo yaliyobanwa kupita kiasi; ni wazi kuwa nguo hizi siyo
rafiki, huifanya damu isizunguke inavyopaswa,”anasema Dk Shanks na
kuongeza:
“Ikifikia hatua hiyo, kuna dalili mvaaji kuweza
kupata maimivu ya miguu kwa kuwa mishipa ya damu iliyopo katika maeneo
hayo inashindwa kufanya kazi yake vizuri.”
Kwa upande wake mtaalamu wa masuala ya ngozi
nchini Tanzania, Dk Isack Maro, anasema kuwa madhara yanayotokana na
uvaaji huo siyo makubwa ikilinganishwa na ripoti ya utafiti unavyoeleza.
“Inawezekana kukawapo uwezekeno wa kupata maradhi
ya ngozi kutokana na mwili kubanwa kwa muda mrefu, hivyo jasho kushindwa
kutoka na kutengeneza mazingira ya fangasi,”anasema Dk Maro na
kuongeza:
“Madhara yapo, lakini siyo kwa ukubwa huo.
Inawezekana kuwakumba watu wachache mno kati ya wengi, lakini sidhani
kama yanaweza kuwa kwa ukubwa huo.”
0 comments:
Post a Comment