NAIBU Waziri wa Fedha na Uchumi (Sera), Mwingulu Lameck Nchemba,
amekimbilia kwa Mchungaji maarufu duniani, TB Joshua, wa nchini Nigeria,
kufanya toba, kuombewa na kupata kile kinachoaminika kuwa ni utakaso.
Mwingulu ambaye pia ni Mbunge wa Iramba Magharibi (CCM), anaongeza
idadi ya wanasiasa nchini wanaokimbilia kwa TB Joshua kuombewa, kufanya
toba na kupata utakaso unaoaminika kwamba unaweza kuwasaidia katika
harakati zao za kisiasa.
Mmoja wa wanasiasa waliopata kufika kwa mchungaji huyo nchini Nigeria
na kuibua mjadala nchini ni pamoja na Waziri Mkuu wa zamani, Edward
Lowassa, Mbunge wa Monduli (CCM).
Akiwa kanisani hapo juzi, huku akionekana moja kwa moja na Kituo cha
Televisheni cha Emmanuel, Mwigulu akiwa amevalia skafu shingoni kama
kawaida yake, aliinuliwa na TB Joshua na kujitambulisha kwa majina yake
matatu kwamba anaitwa Mwigulu Lameck Nchemba.
Kabla ya kumuinua Mwigulu, Nabii Joshua alikuwa akizungumzia namna ya
kumuita Yesu Kristo. Aliwaambia waumini wake waliofurika katika kanisa
hilo maarufu duniani kuwa jina la Yesu linaitwa mara moja na anasikia na
kutenda kazi mara moja, lakini ukiona unamwita Yesu mara nyingi bila
kukuitikia, ujue huyo si Yesu Kristo Mnazareth.
Wakati akisema maneno hayo, Mchungaji Joshua alisogea hadi mahala
alipokuwa ameketi Mwigulu na waumini wengine na kumtaka asimame, huku
akiwaomba waumini waangalie mfano aliokuwa akiutoa kwa Naibu Waziri huyo
wa Fedha.
Mazungumzo kati ya Mwingulu na Mchungaji Joshua yalikuwa hivi:
TB Joshua: Wewe Bwana unaitwa nani
Mwigulu: Naitwa Mwingulu
TB Joshua: Taja majina yako matatu
Mwingulu: Naitwa Mwigulu Lameck Nchemba
Baada ya utambulisho huo, TB Joshua alijaribu kuyaita majina yote
matatu ya Mwigulu, lakini alishindwa kwa kutamka vibaya na baadaye
akamtaka Mwigulu amwite Mchungaji Joshua kwa jina lake.
Kabla ya Mwigulu hajaanza kumwita, Mchungaji Joshua alisogea hatua
takriban kumi mbele ya Mwigulu, akiwa amempa mgongo Mwigulu na kumtaka
amuite kwa jina lake.
Mwigulu alianza kumuita TB Joshua zaidi ya mara saba, lakini Naibu
Waziri huyo hakugeuka nyuma wala kuitikia na ndipo alipowarejea waumini
wake kwa kusema ukiona unaita jina la Yesu mara nyingi bila kuitikiwa,
ujue unayemuita si Yesu.
Katika ibada hiyo, TB Joshua pia alisema Tanzania, Nigeria na nchi
nyingine zinazokabiliwa na uchaguzi mkuu hivi karibuni zitakumbwa na
matatizo makubwa ya hekaheka za uchaguzi, lakini aliwaonya viongozi
watakaohusika na uvunjifu wa amani, hawataachwa salama na mkono wa
Mungu.
Gazeti hili halikuweza kumpata Mwigulu kueleza kwa undani
kilichompeleka nchini Nigeria katika kipindi hiki, lakini wadadisi wa
mambo ya siasa wanasema kuwa ziara ya Mwigulu kwa Mchungaji Joshua,
huenda na bila shaka ina nia ya kufanya toba kwa yote aliyoyafanya
dhidi ya viongozi wa CHADEMA kwa malengo ya kisiasa.
Lakini pia huenda alikuwa na lengo la kutoa asante kwa kuteuliwa kuwa
Naibu Waziri wa Fedha na Uchumi, hivyo kuondokana na siasa za
kushambuliana moja kwa moja na wapinzani kama alivyokuwa akifanya kwenye
nafasi yake ya awali.
Mwigulu aliyetamba kuhusika katika mkakati wa uzushi kwamba viongozi
wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), walipanga njama za
kutaka kumteka Naibu Mhariri Mtendaji wa Mwananchi Communications, Denis
Msaky, alionekana ‘live’ kwenye ibada ya juzi Jumapili mbele ya TB
Joshua na kuonyeshwa moja kwa moja na Kituo cha Emmanuel TV cha nchini
Nigeria.
Katika sakata hilo lililoonekana kama sinema na ambalo hadi sasa bado
liko mahakamani, Mwigulu alisababisha Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama,
Wilfred Lwakatare na Ludovick Joseph wakamatwe na kufunguliwa mashitaka
ya kula njama za kutaka kumuua Msaky, lakini baadaye waliachiwa kisha
kukamatwa tena na kusota kwa muda mrefu rumande bila dhamana. Hata hivyo
watuhumiwa hao sasa wako nje kwa dhamana.
Lengo la mkakati huo haramu wa Mwigulu unadaiwa ni kutaka
kuiaminisha jamii kwamba CHADEMA ni chama cha vurugu, kinachosababisha
mauaji ili wananchi wasikiamini kushika dola.
Ndani ya Bunge la Muungano, Mwigulu ambaye amepata kuwa Naibu Katibu
Mkuu wa CCM (Bara), alikuwa kinara wa kuibua hoja za uzushi na uongo
dhidi ya viongozi wa CHADEMA, hususan Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman
Mbowe.
Mwaka juzi Lowassa, mwanasiasa anayetajwa ‘kujipanga kugombea urais
mwaka 2015,’ alitinga nchini Nigeria kufanya maombi kwa Mchungaji
Joshua, ambaye alimtabiria ushindi unaoelezwa kuwa ni wa urais.
Ziara ya Lowassa kwa TB Joshua ilielezewa kama ‘kukata rufaa kwa
nabii, kutafuta utakaso kisiasa, kupata nguvu na ujasiri’ kabla ya
kuingia katika kinyang’anyiro cha nafasi ya juu ya kisiasa nchini.
Misa ya Nabii Joshua ilionyeshwa katika Emmanuel TV ya Nigeria, ambayo inaonekana duniani kote, Lowassa alionekana akiwa katika jumba la maombi la Nabii Joshua.
0 comments:
Post a Comment