Tuesday, 11 February 2014

MWALIMU AMKATA MWANAFUNZI KIGANJA CHA MKONO KISA KUKATALIWA PENZI

Filled under:



''Ndoto yangu ilikuwa nisome  hadi kufanikiwa kuwa daktari wa binadamu..lakini baada ya kukatwa kikatili kabisa kiganja changu cha mkono wangu wa kulia  kwa wivu wa mapenzi  na Mwalimu wangu  nikiwa kidato cha nne..kila kitu kimeharibika,” anasikitika  Anocietha Theobert (24 ).

Anocietha anasema  tukio hilo lilitokea  Julai  2008 wakati akiwa mwanafunzi wa kidato cha nne katika shule ya sekondari ya Rwambaizi, kata ya Kanoni  wilayani Karagwe,mkoani Kagera.

Mwalimu aliyemkata kiganja hicho, anamtaja kuwa ni  Alliamin Mtabuzi ambaye Novemba  mwaka jana alihukumiwa kifungo cha miaka saba jela na kutakiwa kumlipa fidia ya sh. tano.

''Ilikuwa siku mbaya kuliko zote katika maisha yangu..pale  Mwalimu wangu  alipofika nyumbani kwetu majira ya  jioni moja  na kunifanyia ukatili huu wa kunifyeka kiganja cha  mkono wangu wa kulia na vidole vya mkono wa kushoto.Tukio hilo liliyeyusha  ndoto ya maisha yangu, '' alisema Anocietha.

Mwalimu huyo inadaiwa kuwa,baada ya kufika nyumbani kwa Anocetha  alianza kumshabulia mama mzazi wa mlalamkaji kisha  kumshambulia malalamikaji  kwa panga na kumjeruhi kwa kumkata kiganja cha mkono wa kulia kilichong’oka kabisa kwa kile alichodai kuwa msichana huyo alikuwa mchumba wake ambaye amehamishia mapenzi kwa mtu mwingine.

Baada ya kukatwa mkono anasema kuwa,  alipelekwa katika hospitali ya  Nyakayanga Iliyopo Wilayani Karagwe kwa msaada wa wanakijiji na mama yake mzazi.Alipelekwa  Hospitali akiwa amepoteza fahamu.

Anocietha alitoa ushuhuda huo katika  semina  iliyoandaliwa na Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (TAMWA) iliyoongozwa na Mwezeshaji Ndimara Tegambwene akisaidiana na mratibu wa mpango wa kuwajengea uwezo waandishi wa  habari kuandika na kufichua habari za vitendo vya kupinga ukatili wa kijinsia  wa taasisi hiyo Godfrida Jola.

Ukatili huo anasema, kwa kiasi kikubwa ulichangia kumuathiri kisaikolojia  kwa jamii kumtazama kama mkosaji  hata  kusababisha ashindwe kufanya vizuri katika mtihani wake wa mwisho wa kidato cha nne na kuambulia ushindi wa  daraja la nne alama za mwisho.

Mwalimu Mtabuzi aliyemfanyia  ukatili huo anadai kuwa ulitokana na kumsaliti kimapenzi baada ya baada ya kugundua kwamba alikuwa na mpenzi mwingine wakati tayari walishaahidiana kuoana baada ya kumaliza masomo yake.

''Madai hayo si ya kweli  hata kidogo sikupata hata siku moja kuingia makubaliano ya kufunga ndoa na mwalimu Mtabuzi mara baada ya kumaliza masomo yangu ya sekondari..kama alivyodai ...Ukweli ni kwamba alikuwa ananitaka kimapenzi kwa nguvu kutokana na dhamana yake,''alisema mama huyo.

Anasema  alipenda sana masomo na hivyo  asingeweza kuingia katika makubaliano na mwanaume ili aolewe baada ya kumaliza elimu ya sekondari na kwamba alikuwa na matumaini ya kutaka kutimiza  ndoto yake ya kuwa daktari.

Baada ya mkasa huo na kutibiwa, Anocietha aliamua kuchukua hatua za kisheria.Hata  hivyo  kesi hiyo, ilichukua muda mrefu kusikilizwa na kutolewa hukumu kutoka  mwaka 2008 ilipofunguliwa  hadi Novemba  2013  mtuhumiwa alipohukumiwa gerezani kifungo cha miaka sana  na kutakiwa kumlipa fidia ya shilingi milioni saba.

Hata hivyo, adhabu hiyo anaiona kuwa  haiwezi kumrejeshea kiungo chake muhimu kilichokatwa.

Anakiri kuwa elimu inayotolewa na mashirika ya utetezi ya kiraia kikiwemo Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA) imechangia   kutoa msukumo kwa mashahidi wake kuwa na  ujasiri  kutoa ushahidi mahakamani vinginevyo kesi ingeshindikana.

TAMWA imekuwa ikielimisha kuhusu haki za wanawake na kupambana na ukatili wa kijinsia.

Anocetha baada ya kushindwa kuendelea na masomo ya elimu ya juu baada ya kushindwa kufanya vizuri, aliolewa  ndoa ya kimila na Geofrey France ambaye  ni dereva wa magari yatoayo huduma binafsi  mwaka 2008 siku chache  baada ya mkasa huo na amebahatika kupata mtoto mmoja.

Kwa sasa ni wakazi wa kitongoji cha Katoma,kijiji cha Kayanga Kata ya  Bugene, wilayani Karagwe . Annocietha ni mama wa nyumbani

Akiwa mtoto wa kwanza katika familia ya Mzee Theobert yenye watoto wanne, mkasa huo ulimkuta miezi mitatu tangu Baba yake mzazi  afariki dunia na kubakia yeye, mama yake mzazi na wadogo zake watatu.

Mtu anayedaiwa kumtendea ukatili huo alimtaja kwa jina la Mwalimu Alliamin Mtabuzi aliyedai kumtendea ukatili huo, uliotokana na wivu wa mapenzi baada ya Mwalimu huyo kudai kuwa alikuwa amemsaliti baada ya kugundua kuwa alikuwa na mpenzi mwingine wakati tayari walisha ahidiana kuoana mara baada ya kumaliza masomo madai nayoyapinga Anocietha.

''Madai hayo si ya kweli mimi sikupata hata siku moja kuingia makubaliano ya kuoana na mwalimu Mtabuzi mara baada ya kumaliza masomo yangu ya sekondari..kama alivyodai ...badala yake alikuwa ananitaka kimapenzi kwa nguvu kutokana na dhamana yake''alidai Anocietha.

Anadai kutokana na kupenda sana shule asingeweza kuingia katika makubaliano na mwanaume kwa lengo la kuolewa baada ya kumaliza elimu ya sekondari na badala yake  na matumaini ya kufikia ndoto yake ya kuwa daktari.

Hicho ndicho kisa cha kupoteza kiganja cha mkono wangu wa mkono wakulia..na kidole cha mkono wakushoto katika tukio la kinyama ambalo ni vigumu kuamini kulitenda kwa binadamu tena mwenye elimu ya kutosha..aliyestaarabika.

Hukumu ya shauri hilo ilitolewa  na Jaji Peragia Hadai wa Mahakama kuu  ya Tanzania kanda ya Bukoba katika kikao kilichofanyika wilayani Karagwe Novemba 27 aliyemtia hatiani mshitakiwa Alliamin Mtabuzi (25) kwenda gerezani miaka  saba na  kumlipa Anocietha fidia ya shilingi milioni 5.

''Kitendo hicho kilikuwa kimekatisha ndoto ya kuendelea na masomo  yake,''alieleza  Jaji Hadai katika hukumu yake.

Hukumu hiyo ilivuta hisia za wengi kwa kuzingatia kuwa ilitolewa wakati wa maadhimisho  ya kilele cha siku 16 za kupinga vitendo vya ukatili kilichofanyika Kitaifa mkoani Mwanza.

Mahakama kuu ilitupilia mbali utetezi wa mshtakiwa aliyedai kuwa, alighafilika  baada  kugundua kuwa msichana aliyekuwa akimhudumia kwa mahitaji muhimu ikiwemo ada ya shule kwa makubaliano kuwa angefunga naye ndoa mara baada ya kumaliza shule, kumbe alikuwa na mpenzi mwingine.

Wakili wa Serikali, Safina Simba aliiomba mahakama kuu kumtia hatiani na mshtakwa na kumpa adhabu kali ili liwe fundisho kwa watu wengine wa aina hiyo.

Mwanafunzi huyo katika ushahidi wake, aliiambia mahakama kwamba,  hakuwa na makubaliano ya uchumba kati yake na mwalimu huyo  na kukanusha kumtambua kama mchumba wake.

Naye Wakili wa utetezi wa mshtakiwa aliiambia mahakamani  kuwa inastahili  kumpunguzia adhabu mshtakiwa kwa kuzingatia kwamba alikuwa mchumba wa mlalamkaji kwa makubaliano  ya kumuoa baada ya kumaliza shule.

Aliongeza kudai kuwa, wakati anasoma alikuwa akimgharamia malipo ya karo ya shule na mahitaji mengine yote mhimu hivyo alighafirishwa na kitendo cha kubaini  alikuwa na mchumba mwingine na kuiomba mahakama impunguzie adhabu.

Utetezi huo, ulitupiliwa mbali na mahakama na  mshtakiwa  kutakiwa kutumikia adhabu hiyo ili liwe fundisho kwa watu wengine wenye tabia kama hiyo ya kikatili na kukiuka sheria na haki za binadamu.
.
Mkurugenzi Mtendaji wa Mtandao wa Jinsia Tanzania(TGNP) Usu Mallya , akizungumzia adhabu hiyo alisema kuwa ni ndogo kulingana na uzito wa kosa.Hata hivyo ameridhishwa  kwa kuwa ni hatua moja mbele.

Alisema kuwa hatua ya kesi hiyo kufunguliwa mwaka 2008 na kutolewa hukumu mwaka 2013  mazingira kama hayo yamekuwa yakichangia kesi nyingi kushindwa kumalizika kwa mashahidi kufariki au wengine kuhama na  wengine kuwa na hofu ya kulipizwa visasi.

Naye mwakilishi wa Mtandao wa Kutetea Haki za binadamu na Kupinga Vitendo vya kikatli mkoani Kagera (KAWEF)  Elika Karembo anasema kuwa hukumu hiyo imefungua ukurasa upya, katika safari ngumu ya kutetea haki za binadamu mkoani Kagera na kanda ya ziwa akidai hatua hiyo ni matokeo ya elimu kwa jamii ya kupinga na kufichua vitendo vya ukatili.

0 comments:

Post a Comment