Rais
Jakaya Kikwete akizungumza wakati wa uzinduzi wa mabango ya kuhamasisha
wananchi kupiga vita mauaji ya Tembo na Farubaada ya kuyazindua rasmi
kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Dar es Salaam.
Kulia ni Ofisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Jambo Concepts Tanzania
Limited, Juma Pinto. Kulia kwake ni Naibu Waziri wa Maliasili na
Utalii,Dk. Mahamoud Mgimwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Said
Meck Sadick.
RAIS Jakaya Kikwete, amesema Tanzania haitauza nje shehena ya meno ya
tembo yaliyokamatwa katika matukio mbalimbali nchini, ambayo
yamehifadhiwa.
Amesema yuko tayari kuamuru meno hayo yachomwe moto iwapo hayatakuwa na kazi mbadala lakini si
kuuzwa. Amesema hatatoa kibali cha kuuzwa meno hayo ili kusaidia harakati za kukabiliana na ujangili nchini.
Alisema hayo juzi usiku, alipozindua mabango ya kuhamasisha ushiriki wa Watanzania katika vita dhidi ya ujangili, akiwa njiani kwenda London, Uingereza, ambako leo atahutubia kwenye mkutano maalumu kuhusu kupambana na ujangili wa tembo.
Moja ya mabango hayo nje ya Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Dar es Salaam |
Mkutano huo umeitishwa na mtoto wa Malkia wa Uingereza, Prince Charles, ambapo viongozi wa mataifa zaidi ya 50 duniani watahudhuria, Rais Kikwete akiwa kiongozi wa kwanza kuhutubia.
Alisema miaka kadhaa iliyopita Tanzania ilifanikiwa kupambana na wimbi la ujangili lakini mambo yameharibika kutokana na kurejea kwa biashara ya meno ya tembo, ambayo vinara wa ununuzi ni mataifa makubwa.
“Tumewahi kukumbwa na majanga makubwa ya ujangili mara mbili, awamu ya kwanza ilikuwa miaka ya 70 hadi 1980. Wakati wa Uhuru tulikuwa na tembo zaidi ya 350,000 lakini walipungua hadi kufikia 50,000.”
Alisema hadi mwaka 2009 idadi ya tembo iliongezeka maradufu na kufikia zaidi ya 150,000 lakini sasa imeanza kuwa mbaya kutokana na kushamiri kwa ujangili.
Kuhusu faru, ambao wanakabiliwa na tishio la kutoweka kwa kasi, alisema mwaka 1989 walibaki wawili katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, ambapo wote walikuwa majike kabla ya kuingia dume kutoka Hifadhi ya Ruaha na kuanza kuzaliana.
“Sasa tuna faru 32 na tumeingia kwenye rekodi ya faru wanaozaliana kwa haraka duniani.”
Rais Kikwete alisema jitihada za ndani pekee haziwezi kuwa na mafanikio makubwa, hivyo ni lazima mataifa mengine yahusishwe.
“Nakwenda London kwa mazungumzo ambayo yalianza mwaka jana, yakilenga kufunga masoko ya meno ya tembo na faru. Nitakwenda kuwaambia wazungumze na wenzao kukomesha biashara ya meno ya tembo”
Rais Kikwete alisema pia kumeanza kushamiri biashara ya ngozi za simba, chui na wanyamapori wengine, ambayo inatishia ustawi wa wanyama hao nchini.
Awali, akizungumza kabla ya kuzinduliwa mabango hayo, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mahmoud Mgimwa, alisema lengo ni kuchochea ushiriki wa Watanzania katika kupambana na ujangili.
Tanzania haitauza meno ya Tembo
Serikali ya Tanzania haitawasilisha maombi ya kuuza akiba yake ya meno ya tembo kwa Chombo cha Kimataifa chenye jukumu la kusimamia Biashara ya Wanyamapori na Mimea ambao wako hatarini kutoweka (CITES) ikiwa ni kuunga mkono juhudi za Jumuiya ya Kimataifa za kupiga marufuku biashara haramu ya meno ya tembo duniani. Waziri wa Maliasili na Utalii Lazaro Nyalandu ameyasema hayo jijini London, Uingereza anakohudhuria Mkutano wa Kimataifa unaohusu Biashara Haramu ya Wanyamapori duniani.
0 comments:
Post a Comment