NINAKUMBUKA nilipokuwa mdogo kila tulipokuwa na mchezo wa kandanda
na timu nyingine ya mtaani, uwe wa kugombea kikombe au wa kirafiki,
tulikuwa tunalishana yamini (kula kiapo) kwa kila mmoja wetu
kuhakikisha tunashinda.
Katika kiapo kile tulikuwa tunafungishana pingu ya vidole vidogo vya
mkono wa kulia na baada ya kula kiapo ndipo pingu hukatwa.
Kila ninapokumbuka zama zile hucheka, lakini hujitosheleza kwa kusema zile zilikuwa ni zama za utoto na zimepita.
Kwa kawaida, kitendo cha kula kiapo hasa kwa waumini wa dini moja au
nyingine, si jambo la mchezo wala la kulifanyia mzaha na ndiyo maana
watu wanaokabidhiwa dhamana kubwa katika serikali hulishwa kiapo na
rais cha kuahidi uadilifu.
Lakini siku hizi tunasikia viongozi wa CCM, Zanzibar wanapokutana
wanalishana kiapo cha kung’ang’ania muungano wa mfumo wa serikali mbili
ambao umma tayari umeshatoa kauli ya kuagana nao na kusema unataka
serikali tatu.
Viongozi wa CCM wanapaswa kuelewa kuwa umma haukulishana kiapo
kufikia uamuzi wa kutaka serikali tatu, bali ilikuwa ni ridhaa yao,
hivyo ndivyo walivyoielekeza kwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba
inayoongozwa na Jaji Joseph Warioba, ilipozunguka Vsiwani na Bara
kukusanya maoni ya wananchi.
Kwa hakika viongozi wa CCM wamechelewa kutumia kiapo kakama njia ya kulazimisha kuendelea na mfumo wa serikali mbili.
Watu wamechoshwa na kauli za miaka nenda miaka rudi za kuambiwa:
“Tupo mbioni.” Haujulikani mwanzo wala mwisho kumaliza kero za Muugano.
Kwao matumaini ya kumaliza kero za muungano yapo kwa mfumo wa serikali
tatu.
Kama ni kulishna viapo ndio kungesaidia kuendelea na mfumo wa
serikali mbili basi ilikuwa vema kwa viogozi wa CCM kuzunguka nchi
nzima kabla ya kuanza mchakato wa kukusanya maoni na kuwalisha watu
viapo na si sasa wakati watu wameshaamua.
Kwa maana nyingine huu mwenendo wa kulishana viapo ni kama mchezo wa
kitoto wanaotaka ushindi wa lazima wa mchezo wa kandanda, hata ikiwa
uwezo wa kuifunga timu wanayopambana nayo haupo.
Siku hizi hubaki ninacheka tu ninapokuwa katika baraza za kahawa za
mjini Unguja pale ninapowaona watu kila mara wanafanya mzaha wa kuigiza
CCM kwa kulishana kiapo, hata kwa ahadi ya kukutana baadaye jioni.
Ni vizuri kwa viongozi wa CCM na vyama vingine vikawaachia viongozi
na wanachama wao kuwa huru kuamua aina gani ya Katiba na mfumo wa
muungano wanaoutaka. Hii ni kwa sababu Katiba na muungano si wa chama
chochote kile, bali ni wananchi (wakiwemo wale wasio mashabiki wa chama
chochote kile).
Hizi si tena zama za utamu wa chama kushika hatamu, bali ni zama za utamu wa umma kuamua nchi iwe na mwelekeo gani.
Kwa bahati mbaya baadhi ya viongozi wa CCM wameamua kumshikia bango
kumsakama Jaji Warioba. Wanamuonea mzee huyo ambaye tume anayoiongoza
haikufanya kazi hiyo kwa masilahi yake, ingawa watu walishajenga mazoea
ya kuiita tume ya Warioba. Hili si jambo geni, kwakuwa tuna utaratibu
wa kuipa taasisi au tume jina la kiongozi wake.
Mapendekezo yaliyotolewa na tume si ya Jaji Warioba pekee au pamoja
na wajumbe wenzake wa tume, bali ni ya wananchi. Kilichofanywa na tume
ni kuwasilisha yale waliyoambiwa na umma wakati wa zoezi la
kukusanya maoni na kama walivyotakiwa na hadidu rejea za kazi za tume
hiyo.
Labda lingelikuwa jambo la busara kama katika hadidu rejea tume
ingeambiwa kitakachotakiwa na CCM ndiyo hicho hicho na wengine
wasisikilizwe kwa vile “hawana akili timamu”.
Kama yupo mtu anayefaa kulaumiwa kwa kuchomoza pendekezo la serikali
tatu basi ni huyo aliyeunda hiyo tume, Rais Jakaya Kikwete, lakini
Waswahili wanasema: “Kamba hukatikia pabovu”.
Lakini kwa baadhi yetu tunaomwelewa vizuri Jaji Warioba kwa kufanya
naye kazi kwa karibu, kwa taarifa za viongozi wa CCM wasiomjua, huyu ni
mtu mkweli na huwa hayumbishwi na shinikizo wala vitisho.
Ni mtu anayejiamini na hayumbi katika kusimamia haki na viongozi wa
CCM Zanzibar inafaa niwakumbushe kwamba waliomwalika katika mkutano wao
katika Hoteli ya Bwawani wakati wa mtafaruku wa kisiasa aliwaambia
kama Zanzibar palikuwa na matatizo basi wao viongozi wa Serikali ya
Zanzibar (CCM) walikuwa na matatizo.
Niwakumbushe zaidi kuwa kauli ya Jaji Warioba ambayo iliwaudhi sana
pia iliungwa mkono na Rais Kikwete ambaye wakati ule alikuwa Waziri wa
Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa. Kwa maana hiyo, Jaji Warioba
wa juzi ndiye wa jana na ndiye wa leo….hayumbi katika kusema ukweli.
Sifa yake nyingine niliyoigundua kwa kufanya naye kazi akiwa waziri
mkuu, wakati nikiwa mwandishi wa Waziri Kiongozi wa Zanzibar, na
baadaye kwa zaidi ya miaka sita nikiwa naye pamoja katika Bodi ya
Baraza la Habari la Tanzania, ni kuridhia maoni ya wengi, hata kama
hakubaliani nayo.
Jaji Warioba siku zote, kwa ninavyomuelewa, amekuwa hakubali
kudanganya wala kudanganywa. Mara nyingi tulipokuwa tunajadili
malalamiko yaliyowasilishwa katika Baraza alikaa kimya kusikiliza
wajumbe wengine, bila ya kujali ni mtu aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa
Serikali, pia waziri mkuu.
Aliheshimu sana mawazo ya wanataaluma wa habari na wanasheria wenzake
ambao walikuwa na miaka michache katika taaluma hiyo kuliko yeye, kama
marehemu Sengondo Mvungi na Jenerali Ulimwengu.
Kama CCM ilikuwa na nia ya kuifanya tume ifanye kazi ya “danganya
toto” basi ilikosea tangu mwanzo kuchagua watu kama Jaji Warioba kuwa
Mwenyekiti na wajumbe wengine kama Jaji Agustino Ramadhani, waziri mkuu
mstaafu, Salim Ahmed Salim na mwandishi wa habari maarufu, Ally Saleh.
Hawa ni viumbe wenye kujiamini na si wale unaoweza kuwa na ndoto ya kuwaburuza na kuwatumia waseme uongo.
Nnaamini kwa dhati, kama nilivyoamini mapendekezo ya tume za
marehemu Jaji Francis Nyalali na ile ya Jaji Robert Kisanga,
yaliyowasilishwa na tume ya Jaji Warioba ndicho wanachokitaka
Watanzania, Bara na Visiwani.
Kama CCM ilitaka kuunda tume ili iwe kama muhuri wa kuhalalisha
kinachotakiwa na viongozi (baadhi yao si wote) wa CCM basi imechelewa
na isifanye ujanja, mtarimbo umeganda na hauugandui kwa shoka wala
mzinga, uwe wa nyuki au mwingine
Kinachohitajika ni kuendelea kuwa na mchakato ambao watu watakuwa
huru kuamua Katiba mpya iwe vipi. Inafurahisha kumsikia Rais Kikwete
akiweka wazi kuwa uamuzi wa mwisho si wa chama chochote kile cha siasa,
bali wa wananchi.
Si vitisho wala viapo vitakavyosaidia, bali nguvu ya hoja na itakayoeleweka kwa njia za kidiplomasia na kuheshimiana.
Inasikitsha kuwasikia baadhi ya viongozi wa CCM Zanzibar wakiwemo
wale waliotimuliwa kushika nafasi za juu katika serikali, wanazungumzia
nguvu za dola za kumiliki vifaru na ndege za kivita kuunganisha na hoja
zao.
Sasa hizi ndege za kivita na vifaru vilivyoonyeshwa wakati wa
kuadhimisha miaka 50 ya Mapinduzi ya Zanzibar zina uhusiano gani na
mchakato wa Katiba au mfumo wa Muungano? Acheni kutisha watu, jitisheni
wenyewe.
Tuwe watu wazima na tuachane na utoto, uwe wa kutishana au kulishana
viapo. Tuukubali ukweli uliopo mbele yetu. Nao ni wa serikali tatu na
kusema kwaheri serikali mbili.
.
0 comments:
Post a Comment