MAMLAKA ya Chakula na Dawa Tanzania (TFDA) imeingia kwenye kashfa ya
kumwajiri mtumishi asiye na cheti cha kitaaluma kuwa msaidizi wa maabara
ya dawa kuanzia Desemba 2, 2013.
Mkurugenzi wa TFDA, Hiiti Sillo, jana alithibitisha kufanyika kwa
udanganyifu huo lakini akafafanua kuwa baada ya kujiridhisha na tuhuma
hizo, mtumishi huyo, Pilly Komba Kilongosi, amekabidhiwa barua ya
kuachishwa kazi rasmi kuanzia Januari 28, 2014.
Uchunguzi wa gazeti hili ulibaini kuwa TFDA kupitia gazeti la
serikali la Daily News la Julai 1, 2013 ilitangaza nafasi za kazi saba
ikiwemo hiyo ya msaidizi wa maabara ya dawa ambapo mwombaji alitakiwa
kuwa na sifa za elimu ya kidato cha nne na mwenye uzoefu usiopungua
miaka mitatu katika kazi hiyo.
Vigezo vingine ni mwombaji kuambatanisha barua ya maombi, wasifu wake
(CV), nakala za vyeti na hati ya matokeo (transcripts), picha mbili za
pasipoti na majina ya wadhamini wawili.
Vyanzo vyetu vilibaini kuwa Pilly alituma barua ya maombi Julai 5,
2013, akionyesha kuwa amehitimu kidato cha nne katika Sekondari ya
Temboni jijini Dar es Salaam na kisha kuhudhuria kozi ya msaidizi wa
maabara ngazi ya III na II katika Chuo cha Veta cha Dar es Salaam mwaka
2011/2012.
Katika barua hiyo, Pilly anadai kuwa anao uzoefu katika kazi hiyo kwa
zaidi ya miaka mitatu akifanya kazi kama mfanyakazi wa muda TFDA na TBS
wakati ukweli ni kwamba amefanya mafunzo kwa vitendo kwa miezi 12 pekee
yaani TFDA mizei tisa na TBS miezi mitatu.
Pilly aliongeza kuwa ameambatatisha nakala za vyeti kikiwemo kile cha
kidato cha nne ambacho hana kutokana na kupata daraja sifuri katika
mtihani wake wa mwisho, CV na hati ya matokeo ya kitaaluma.
Katika hatua inayotia shaka kwamba Pilly aliandaliwa mapema kupewa
ajira hiyo, majukumu saba yanayotajwa katika tangazo kwa mwombaji
kuyajua, ndiyo hayo hayo yameorodheshwa na Pilly katika CV yake neno kwa
neno kuanzia namba moja hadi saba.
Kwa mujibu wa vielelezo ambayo gazeti hili linavyo, Pilly alihitimu
kidato cha nne mwaka 2010, ambapo alifanya mtihani kwa namba S3799/0098
na kupata daraja sifuri la alama 35 akiwa amepata F katika masomo yake
yote ya Uraia, Historia, Jiografia, Kiswahili, Kiingereza, Baiolojia na
Hesabu.
Pamoja na kukosa vigezo tajwa, Pilly aliajiriwa kama mtumishi wa TFDA
tangu Desemba 2, 2013 hadi Januari 28, 2014, alipofukuzwa baada ya
kubainika alipenyezwa kinyemera.
Alipohojiwa Mkurugenzi wa TFDA kuhusu hatua zilizochukuliwa kwa
waliofanya udanganyifu huo, alisema kuwa hizo ni taratibu za ndani za
utumishi ambazo zinaendelea kufanyika.
“Ni kweli huyo binti aliajiriwa kwetu lakini kama unavyosema baada ya
kufanyika uchunguzi tulibaini makosa yalifanyika wakati wa mchakato wa
usaili, hivyo jana amepatiwa barua ya kuachishwa kazi rasmi na amehojiwa
na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU),” alisema Sillo.
Akizungumza na gazeti hili kuhusu madai hayo, Pilly alithibitisha
kupewa barua ya kuachishwa kazi juzi akielezwa kuwa alikosa sifa ya
kutokuwa na cheti cha kitaaluma cha kidato cha nne na kwamba alihojiwa
pia na TAKUKURU ili kutoa maelezo.
“Alipoulizwa alipataje kazi wakati hakuwa na vigezo, Pilly alijitetea
kuwa: “Kazi zilitangazwa nikaomba na nikapata, hivyo siwezi kujua
vigezo gani walitumia katika mchakato wa usaili”.
“Alipoulizwa alipataje kazi wakati hakuwa na vigezo, Pilly alijitetea
kuwa: “Kazi zilitangazwa nikaomba na nikapata, hivyo siwezi kujua
vigezo gani walitumia katika mchakato wa usaili”.
0 comments:
Post a Comment