Monday, 27 January 2014

RAIS KIKWETE AAMRISHA JESHI KUSIMAMIA UTOAJI HUDUMA KWA WAATHIRIKA WA MAFURIKO MOROGORO

Filled under:



Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi la Ulinzi na Usalama, Rais Jakaya Mrisho Kikwete ameliamuru Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kuanza mara moja kazi ya kusimamia utoaji huduma kwa watu walioathiriwa na mafuriko katika Mkoa wa Morogoro, ikiwa ni pamoja na kusimamia ujenzi wa nyumba za muda wa waathirika hao.
Rais pia ameliamuru Jeshi kupeleka mashine za kusafisha maji katika makambi ambako waathirika hao wa mafuriko ya Januari 22, mwaka huu wanaishi kwa muda.
Aidha, Rais Kikwete amewahakikishia waathirika wa mafuriko hayo kuwa Serikali itahakikisha inawapatia huduma zote za msingi ikiwa ni pamoja na chakula, malazi, maji na huduma za afya hadi hapo watakapokuwa na uwezo wa kuanza kujitegemea tena.
Rais Kikwete ametoa amri hizo kwa Jeshi leo, Januari 27, 2014, wakati alipotembelea kambi za waathirika wa mafuriko hayo kuwajulia hali walioathirika katika makambi yaliyoko Shule ya Sekondari ya Magole katika eneo la Dumila na katika Kijiji cha Mateteni kilichoko Dakawa, Wilaya ya Kilosa.
Katika hotuba zake fupi baada ya kuwa ametembelea na kuona mahema ambamo waathirika hao wanalala, Rais Kikwete amesema   ameagiza Jeshi kuongoza harakati za kuwahudumia wahanga hao kwa sababu zikifuatwa taratibu za kawaida za Kiserikali huduma zitachelewa sana kuwafia waathirika.
“Kazi yetu ni kusimamia maisha ya watu hasa   kipindi cha shida za namna hii. Tukifuata taratibu za kawaida za Kiserikali za tenda tutachelewesha sana huduma za dharura kwa waathirika. Ndiyo maana nimeliamuru Jeshi kufanya kazi hii ikiwa ni pamoja na kujenga haraka makazi ya muda wa waathirika,” amesema Rais Kikwete na kuongeza:
“Katika mazungumzo hayo na Mkuu wa Majeshi, nimemwagiza pia kuleta mashine za kusafishia maji ili kuhakikisha kuwa watu wanakunywa maji salama kwa sababu katika hali ya sasa maji yasiyokuwa salama yanaweza kuwa chanzo cha magonjwa.”
Kuhusu upatikanaji wa chakula cha msaada kwa wahanga, Rais Kikwete amesema kuwa Serikali inacho chakula cha kutosha kwa ajili yao. “Tunacho chakula cha kutosha na hata kile tusichokuwa nacho tutanunua. Tutabanana ndani ya Serikali ili tupate fedha za kutosha za kuwahudumia.”
Kuhusu malazi, Rais amesema:”Naambiwa kuna upungufu wa magodoro. Tutahakikisha kuwa yanapatikana na yatafika katika siku mbili zijazo. Hatutaki watu walale chini na waje kupata vichomi.”
Kuhusu maji, Rais Kikwete amesema kuwa Serikali itaendelea kutoa huduma ya maji bure kwa wahanga. “Tutaendelea kutoa bure huduma hii mpaka hapo huduma ya kawaida ya maji itakapoanza kupatikana tena.”
Kuhusu huduma za afya, Rais amesema kuwa anafurahi kuwa kila kambi ya wahanga inayo huduma ya afya ambayo itaendelea kutolewa kwa kadri watu wanavyozidi kuishi kwenye makambi.
Rais ameagiza kuwa baada ya muda mfupi viongozi wa Mkoa wa Morogoro na wilaya husika wakae chini ya viongozi wa ngazi za chini na wahanga kujadili na kutafuta mwafaka kuhusu maisha ya baadaye ya wahanga – hasa kuhusu namna gani wanaweza kupatiwa maeneo yaliyoko nje ya mikondo ya mafuriko.
“Hili ni lazima kwa sababu hata kama imechukua miaka mingi kwa mafuriko ya sasa kutokea ni dhahiri kuwa iko siku yatakuja tena – inaweza kuwa hata mwaka huu kwa sababu zipo mvua za masika. Kwa hiyo ni lazima tukubaliane jinsi gani ya kurudi ama kutokurudi katika maeneo yetu tulikotoka.”

0 comments:

Post a Comment