KAMANDA wa Polisi Kanda Maalumu ya Tarime Rorya, Justus Kamugisha,
anatumia madaraka yake vibaya kumnyanyasa askari wake, G. 2751 PC.
Japhet Samwel, aliyeumia mkono akiwa kazini mgodini Nyamongo.
Licha ya kumnyima fedha za matibabu na hivyo kumsababishia ulemavu wa
mkono wake, kamanda huyo sasa amefikia hatua ya kutaka kumuhamisha kwa
nguvu kwenda mkoani Mwanza kuanzia Januari 20, mwaka huu.
Samwel ambaye mkono wake hauwezi kufanya kazi kwa sasa, na hivyo
kushindwa kuisaidia familia yake, alikuwa ni miongoni mwa askari 31
waliopelekwa mgodini Nyamongo wakitokea mjini Tarime kuanzia Septemba 30
hadi Desemba 25, mwaka jana.
Taarifa hizo zilifichuliwa kwa mara ya kwanza na gazeti hili mwaka
jana, hatua iliyosababisha Makao Makuu ya Jeshi la Polisi kuingilia kati
kuchukua hatua, juhudi ambazo hata hivyo zimeyeyuka sasa.
Kwa mujibu wa vyanzo vyetu, baada ya askari huyo kutishia kuacha
kazi, aliyekuwa IGP, Said Mwema, alimtuma kamishna msaidizi wa makao
makuu, Shumbusi, aliyefika Tarime na kuonana na Samwel.
Gazeti hili lilidokezwa kuwa Samwel alimweleza Mshumbusi kuwa anataka
alipwe gharama zake za matibabu na endapo jeshi halina fedha kama
alivyoelezwa, basi apewe likizo ya kujitibia mwenyewe.
“Sikupewa fedha hiyo ya matibabu, badala yake nilipewa likizo ya
miezi mitatu na baada ya kurejea kazini kama wiki nne zilizopita,
nilipangwa kufanya kazi ofisi ya OC CID.
“Pale niliwekwa kama kujifunza kazi maana mkono wangu huu kwa sasa
siwezi kufanya kazi yoyote ngumu,” alithibitisha Samwel baada ya
kuulizwa juzi.
Alisema hivi karibuni alifika kamishna msaidizi mwingine wa makao
makuu, Gerald, na kukutana na askari wote wanne walioathirika katika
tukio hilo ili kuzungumza nao kuhusu fidia zao.
Kwa mujibu wa chanzo chetu, askari hao walihoji ni kwanini wanaambiwa
kuwa wanaweza kulipwa fidia ndogo kuliko madhara waliyopata, na kuliko
gharama walizotumia kujitibia ilhali waliumia wakiwa kazini.
Kwamba walielezwa kuwa wasingeweza kulipwa fedha hizo kwa vile wana
bima ya afya, jambo walilodai ni kinyume na Police Regulation Act ya
2010 kwani bima ya afya haigharamii nauli, chakula wala malazi.
Akizungumza na gazeti hili, Samwel alikiri kufanya kikao na kiongozi
huyo wa makao makuu akiwa pamoja na Kamanda Kamugisha, akisema kuwa
alishangaa kuona kesho yake akiletewa fomu ya uhamisho.
Januari 17, mwaka huu, Samwel alipokea movement order iliyosomeka;
Umeamriwa kuondoka hapa kikosini kwenda Ofisi ya Kamanda (M) Tarime
Rorya. Kwa maelekezo zaidi piga timamu kwa Staff Officer kwa maelekezo
ya kutekeleza amri ya uhamisho kwenda Mwanza. Simu kumb TRR/AD.21/189
yahusika.”
Baada ya kupewa fomu hiyo, alikwenda kuhoji anakwendaje Mwanza bila
kupewa fedha za uhamisho na kujikimu kwa familia yake, lakini akajibiwa
na Kamishna Sweetbert Henjewele kuwa suala la familia wao haliwahusu.
Januari 20, mwaka huu, aliletewa movement order nyingine ikisomeka;
“Umeamriwa kuondoka hapa terehe 20/1/2014 kwenda Mwanza kwa ajili ya
kutekeleza amri ya uhamisho wa Inspekta Jenerali wa Polisi. Ufikapo huko
utaripoti kwa RPC Mwanza kwa maelezo zaidi. Simu PHQ/AD.21/VOLXXI/267
ya tarehe 16/07/2013 yahusika”.
Samwel alisema: “Mimi nimekataa kuichukua hiyo fomu kwa sababu sina
nauli ya kwenda Mwanza na isitoshe sijajua fanilia yangu inabakije hapa
kama nalazimishwa kwenda tu huko tena kwa vitisho vya kuadhibiwa
kijeshi.”
Mwandishi liliwasiliana na Kamanda Kamugisha ili kufahamu ni
kwanini askari huyo hapewi haki yake, ambapo alisema hana taarifa ya
suala hilo.
Alipoulizwa kuwa anamchukia Samwel kwa sababu alivujisha suala hilo
kwenye vyombo vya habari, alisema: “Unajua kuna vitu vya kuandika, mimi
sina taarifa na hilo.
“Huyo askari msaidieni asije akavunja sheria kwa kuleta masuala ya
jeshi kwenu. Ukitaka kujua taarifa zake muulize mwajiri wake.”
tunayo nakala ya barua UPEL.TRR ® Polisi (W) zote ®
vikosi vyote TRR/A.24/5/Nyamongo/232, iliyosainiwa na SSP Sebastian
Zacharia, ikiwaweka tayari askari hao kwa safari ya kwenda mgodini
wakati huo.
Kwa mujibu wa nyaraka, viongozi wa kikosi hicho cha askari 31
walikuwa ni SGT Tabu, WP Vailet, PC Mauki, G9455 PC Hosea na D.2766 PC
Andrew waliokuwa wakitumia gari ya polisi PT 1685.
Samwel alidai kuwa wakiwa kazini mgodini walishambuliwa kwa mawe na
watu wasiojulikana na kuwasababishia majeraha sehemu mbalimbali za
mwilli.
Alisema kutokana na tukio hilo, walifungua kesi M/NY/3032/10/2012
Oktoba 23, 2012, kuhusu shambulio hilo ambalo lilimjeruhi mkono wa
kulia.
PC Samwel alisema kuwa alipewa barua na uongozi wa mgodi ili aweze kwenda hospitali ya Bugando.
Kwa mujibu wa Dk. Gerald Lenjima wa mgodi wa dhahabu wa Barrick
uliopo Nyamongo, askari huyo alikuwa ameumia sana kiganja cha mkono wa
kulia, na hivyo angehitaji uangalizi wa karibu wa madaktari bingwa.
Lakini mnadhimu wa jeshi hilo mkoani Mara alikataa ushauri wa daktari
na kuamrisha apelekwe hospitali ya Shirati iliyopo mkoani humo.
Alisema kuwa baada ya kubaini kuwa mkono wake unaharibika, alienda
kumwona Kamanda Kamugisha kuomba fedha za matibabu na nauli ili aweze
kwenda Bugando kama alivyoandikiwa na daktari.
Daktari bingwa wa Bugando alielekeza kuwa PC Samwel ahudhurie
matibabu ya mkono huo kwa wiki nane mfululizo kwa kuwa mifupa ilikuwa
imevunjika.
Lakini Januari 21, 2012 aliomba ruhusa ili aweze kwenda Bugando kwa
wiki nane na kujibiwa: ‘Umeamriwa kuondoka hapa kesho kwenda Bugando kwa
ajili ya matibabu na umepewa siku tatu urudi hapa mara umalizapo
matibabu.”
Chanzo chetu kilisema kuwa askari waliokuwa katika operesheni hiyo
walikuwa wanalipwa na mgodi huo sh 25,000 kila mtu kwa siku, lakini
Samwel baada ya kuumia aliacha kulipwa.
Samwel alisema kuwa akiwa katika hali hiyo ngumu, mkono wake
ulibadilika rangi na hivyo akalazimika kufika tena ofisini kwa kamanda
wa polisi kuomba ruhusa, fedha za nauli na matibabu aweze kurudi
hospitali, lakini aliambulia matusi ya nguoni.
Kwamba alitishiwa kuwekwa mahabusu ya polisi kama mtuhumiwa kwa
kumsumbua kamanda wa polisi, huku kamanda huyo akisema: “Nimekwambia
jeshi halina fedha za kukutibu, unataka niuze gari ya kamanda ili nikupe
nauli na fedha za kutibiwa?”
Baadaye alipewa ‘movement order’ ya kuruhusiwa kwenda hospitali kwa
gharama zake na aliporudi na kupeleka maombi ya kulipwa fedha alizotumia
kujitibu, alikataliwa akiambiwa hawana fedha.
Samwel aliongeza kuwa alipokwenda kwa kamanda alikamatwa na kuwekwa
mahabusu na kupigwa marufuku ya kumwona bosi wake huyo na kuelezwa kuwa
akirudia mkataba wake utazuiwa ili afukuzwe kazi.
0 comments:
Post a Comment