RAIS
Jakaya Kikwete ameshauriwa katika mchakato wa mabadiliko ya Baraza la
Mawaziri kumtaka Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo
kujieleza kwake na umma ili kuwezesha hatua stahiki kuchukuliwa dhidi
yake kutokana na ongezeko la bei ya umeme.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na Waziri
Kivuli wa Nishati na Madini, John Mnyika (CHADEMA), Rais Kikwete
anapaswa kutambua kuwa Waziri Muhongo alisema uongo kwa nyakati
mbalimbali mwaka 2012 na 2013 alipowahakikishia wananchi kuwa bei ya
umeme haitapanda hata baada ya Shirika la Umeme Nchini (TANESCO)
kuwasilisha mapendekezo ya kupandisha bei ya nishati hiyo.
Alisema kinyume na kauli za Prof. Muhongo, Bodi ya Wakurugenzi wa
Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura), katika kikao
cha Desemba 10, mwaka jana, ilitoa maamuzi ya ongezeko la bei za umeme
kwa viwango mbalimbali kwa makundi mbalimbali ya wateja, hatua ambayo
itaongeza mzigo wa gharama za maisha kwa wananchi na itaathiri uchumi wa
nchi.
Wakati Mnyika akisema hayo, wananchi wamependekeza kwamba iwapo
mamlaka husika hazitapunguza kiwango cha ongezeko la bei ya umeme;
maandamano yaandaliwe kuishinikiza serikali kuchukua hatua za haraka za
kunusuru uchumi wa nchi na maisha ya wananchi kutokana na ongezeko hilo.
Mnyika ambaye ni mbunge wa Ubungo, alisema kuwa uamuzi wa kupandisha
nishati hiyo ulifikiwa Oktoba 11, mwaka jana, baada ya TANESCO
kuwasilisha maombi ya kurekebisha bei ya umeme kwa Ewura, iliyopendekeza
kuongeza bei kwa asilimia 67.87 kuanzia Oktoba 1, mwaka jana, asilimia
12.74 kuanzia Januari 1, mwaka huu na asilimia 9.17 kuanzia Januari 1,
mwaka 2015.
“Vilevile TANESCO waliomba kuidhinishwa kwa kanuni ya kurekebisha bei
ya umeme kulingana na mabadiliko ya bei za mafuta, mfumko wa bei na
mabadiliko ya thamani ya shilingi ya Kitanzania hatua ambazo nazo zina
athari katika uchumi na maisha ya wananchi,” alisema.
Kuhusu wananchi kuandamana, alisema kuwa kutokana na ongezeko hilo
aliomba kufikishiwa maoni ya wadau katika kipindi cha wiki moja juu ya
athari za ongezeko hilo na hatua ambazo wananchi wanapendekeza
zichukuliwe kurekebisha hali hiyo.
“Kabla ya kipindi hicho kumalizika tayari nimepokea maoni ya wananchi
kutoka katika mikoa mbalimbali nchini. Hakuna mwananchi yeyote mpaka
hivi sasa kati ya waliotuma maoni kwa njia ya barua pepe aliyeunga mkono
ongezeko hilo la bei ya umeme,” alisema.
Mbunge huyo alisema kuwa wananchi hao wameelezea athari ambazo
wameanza kuzipata huku wakipendekeza hatua ambazo zinapaswa kuchukuliwa
kunusuru uchumi wa nchi na ongezeko la gharama za maisha linalotokana na
ongezeko la bei ya umeme.
Alisema kuwa wananchi wamependekeza kwamba badala ya mamlaka
kukimbilia kupandisha bei ya umeme ni muhimu kuchukua hatua za kupunguza
mzigo mkubwa wa gharama za uzalishaji, usafirishaji na usambazaji wa
umeme pamoja na uendeshaji wa sekta ya nishati.
0 comments:
Post a Comment