Wednesday, 15 January 2014

CCM NA CHADEMA WATUNISHIANA MISULI KWENYE UFUNGUZI WA MRADI WA MAJI

Filled under:



Chama cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) katika Manispaa ya Moshi, vimeingia tena katika vita ya kuwania madaraka na kusababisha viongozi wa juu wa vyama hivyo, kutunishiana misuli mbele ya Waziri wa Maji, Profesa Jumanne Maghembe,wakituhumiana kuugeuza mradi wa maji wa Kiboriloni, kete ya kisiasa kuelekea uchaguzi mdogo wa udiwani katika Kata hiyo.

Mradi huo wa maji Kiboriloni ulipangwa kutekelezwa kwa awamu tatu na awamu ya kwanza ilihusisha ujenzi wa bomba kubwa umbali wa kilomita moja kutoka mto Rau hadi KDC, wakati awamu ya pili ilihusisha ujenzi wa umbali wa kilimota 1.2 kutoka KDC hadi Kiboriloni na
awamu ya tatu ni uchimbaji wa kisima kikubwa eneo la KDC.

Aliyetibua mkakati huo na kusababisha viongozi kuumana kwa kurushiana vijembe hadharani ni mbunge wa Moshi Mjini (Chadema), Philemon
Ndesamburo aliyekuwa ameongozana na makada wa chama hicho wakiwamo wabunge wawili, Lucy Owenya na Suzan Lyimo, baada ya kusimama na kumsihi Waziri Maghembe kuwaonya watendaji wasisababishe wanasiasa kugombana kwa sababu ya shughuli za maendeleo.

Kata ya Kiboriloni iliachwa wazi mwishoni mwa mwaka jana baada ya Diwani wake, Vincent Rimoy (Chadema) ambaye pia alikuwa Naibu Meya wa
Manispaa ya Moshi kufariki dunia.

“Mimi kama mbunge wa Moshi Mjini na mkazi wa eneo hili la Kiboriloni nimekuja hapa bila hata ya kualikwa lakini pia mradi huu unazinduliwa kwa sababu tuna uchaguzi mdogo wa udiwani kwenye kata hii mwezi ujao…Mheshimiwa Waziri (Maghembe) watendaji wasitugombanishe wanasiasa kwa ajili ya shughuli za maendeleo, nitaomba uchukue hatua na nitakukumbusha hata tukiwa kwenye vikao vyetu kule Dodoma,” alisisitiza.

Baada ya Ndesamburo kumaliza kuzungumza, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Moshi Mjini, Elizabeth Minde, alisimama na yeye katika jukwaa hilo akawaambia wakazi wa Kiboriloni kwamba kinachofanyika ni utekelezaji wa ilani ya Chama cha Mapinduzi kwa kuwa kiliahidi maji safi na salama kwa wananchi wake.

“Suala la uzinduzi wa leo halihusiani na uchaguzi mdogo wa udiwani Kata ya Kiboriloni na kwanza hiki alichokisema mbunge wetu (Ndesamburo), wala hatujui huo uchaguzi utafanyika lini maana hata tarehe haijatangazwa. Kinachofanyika ni utekelezaji wa ilani ya CCM kwa sababu tulipeleka kwa wananchi mwaka 2010 na wao Chadema walipeleka ya kwao sisi tukashinda kuunda serikali kwa hiyo ndio maana tunatekeleza tulichoahidi,” alisema Minde.

Meya wa Manispaa ya Moshi, Japhari Michael, alisema kilichotokea ni kitu kibaya katika siasa kwa sababu miradi ya maendeleo inataka kuwagawa
wananchi badala ya kuwapa faraja ya kufikia malengo yao katika mipango ya kichumi na hasa huduma za jamii.

Hata hivyo, Waziri Maghembe alisema hakuna
ubishi kwamba mradi huo unatokana na utelelezaji wa ilani ya CCM na kwamba kikubwa wananchi wamepata huduma ya maji safi na salama na kwamba suala la uchaguzi mdogo ni jambo jingine.

0 comments:

Post a Comment