Friday, 6 December 2013

WAZIRI MKUU AUANIKA MSHAHARA WAKE BUNGENI

Filled under:



Waziri Mkuu, Mizengo Pinda ametangaza mshahara wake bungeni akisema analipwa Sh6 milioni mbali na marupurupu mengine.
Pinda alisema hayo jana katika kipindi cha Maswali ya Papo kwa Hapo kwa Waziri Mkuu baada ya kuombwa na Spika wa Bunge, Anne Makinda kutoa ufafanuzi juu ya utata wa mshahara wake na viongozi wakuu wa nchi, alipokuwa ajibu swali la nyongeza la mbunge wa Mkanyageni (CUF), Habib Mnyaa.

Katika swali hilo,Mnyaa alisema mitandao ya kijamii imekuwa ikisema kwamba mshahara wa Rais ni Sh32 milioni na wa Waziri Mkuu ni Sh26 milioni lakini Bunge halijawahi kuidhinisha mishahara hiyo.

“Sasa kwa kuwa Bunge ndilo linapaswa kupanga je, utakubaliana na mimi kuwa Bunge lako limeporwa haki hii na kupelekwa kwenye Executive (Utawala)?” alihoji Mnyaa. Swali hilo lilionekana kumgusa Spika Makinda ambaye alimtaka Waziri Mkuu atumie nafasi hiyo kujibu kile alichosema ni uongo wa magazeti juu ya mishahara ya viongozi hao.

Hatua ya Makinda imetokana na madai ya Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema), Zitto Kabwe ambaye katika mikutano mbalimbali ya hadhara aliwahi kusema kuwa Waziri Mkuu analipwa mshahara wa Sh26 milioni kwa mwezi huku Rais akilipwa Sh32 milioni.

Akijibu, Pinda Alisema: “Mshahara anaopata Waziri Mkuu ni Sh6 milioni na hiyo ni pamoja na posho ya mke wangu ambayo ni sehemu ya fedha hiyo… Sasa mtu anakuja anasema napata milioni 30!

“Nataka nikuthibitishie, tofauti ya mshahara wangu mimi na Makamu na Rais hauzidi hata milioni moja. Nadhani Mwenyezi Mungu atamwepusha (Zitto) na balaa zinazoweza kumpata kwa kusema uongo.” Alisema ukiondoa mshahara huo, kwa vile yeye ni sehemu ya Bunge, amekuwa akilipwa posho kati ya Sh500,000 na Sh600,000 ya uwajibikaji (responsibility allowance) kwa kuwa Waziri Mkuu.

“Posho nyingine unazopata kama Mbunge na mimi napata ikiwamo Mfuko wa Jimbo. Kinachonisaidia ni mfumo wa Serikali wa kutoa nyumba ya bure na kugharimiwa chakula.”

Alisema alipomsikia Zitto akisema hayo kwa mara ya kwanza hakushtuka hadi alipomsikia akirudia maneno hayo Mpanda.

“Nilishtushwa na madai hayo ya Zitto... naona labda ni njama za kuniharibia tu jina langu ili Watanzania waanze kujiuliza inakuwaje mtoto wa mkulima alipwe fedha nyingi kiasi hicho? Mtoto wa mkulima gani anatapa mshahara mkubwa huo?”, alisema na kuongeza: “Nadhani Mwenyezi Mungu atamwepusha (Zitto) na balaa zinazoweza kumpata kwa kusema uongo”.

Alisema mifumo mizuri iliyowekwa na Serikali kuwahudumia viongozi wakuu wa Serikali akiwamo ni mizuri na ndiyo ambao imewafanya wasijiingize kwenye kwenye tamaa.
Hatua ya Zitto kutangaza mishahara ya viongozi wakuu wa Serikali ilitokana na kupinga adhabu ya kufungiwa kwa magazeti ya kila siku ya Mwananchi na Mtanzania.

0 comments:

Post a Comment