Wednesday, 11 December 2013

PINDA AZIDI KUANDAMWA NA WABUNGE

Filled under:



Mzimu wa kung’olewa unazidi kumwandama Waziri Mkuu, Mizengo Pinda huku Mbunge wa Muhambwe, Felix Mkosamali (NCCR), akitaka Bunge lipige kura ya kutokuwa na imani naye.
Akizungumza bungeni mjini Dodoma jana, mbunge huyo alienda mbali zaidi na kuomba Naibu Spika, Job Ndugai kuwaongoza 

wabunge kupiga kura hiyo ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu.
Pia alitaka kung’olewa kwa Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Hawa Ghasia akisema haiwezekani aendelee kuwepo wakati fedha za wafadhili zinaliwa bila yeye kuchukua hatua.

Mkosamali anakuwa mbunge wa tatu kupendekeza kung’olewa kwa waziri mkuu, akitanguliwa na Mbunge wa Mwibara, alphaxard Lugola (CCM) na Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila (NCCR).

Mkosamali alisema ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) zinaonyesha hakuna ufuatiliaji wa fedha zinazoidhinishwa na Bunge na kupelekwa katika Halmashauri nchini.

Alisema taarifa zinaonyesha asilimia 20 ya bajeti ya Serikali huingia mifukoni mwa watu na kuongeza kuwa hata Bunge likapitisha bajeti ya Trilioni 40 bado asilimia 20 zitakwenda mifukoni mwa watu.
Mkosamali alisema katika semina mbalimbali wabunge walielezwa kuwa taarifa za CAG zinazofichua ufisadi wa kutisha pamoja na taarifa za Kamati za Bunge zimekuwa hazifanyiwi kazi na Serikali.

Mbunge huyo aliwasihi wabunge wenzake kuchukua hatua na 
kuhakikisha kuwa kabla ya kumalizika kwa mkutano wa 14 wa Bunge unaoendelea mjini Dodoma mawaziri kadhaa wawe wameng’oka.

Akinukuu Ibara ya 52 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977, Mkosamali alisema, Waziri Mkuu ndiye atakuwa na madaraka ya juu katika udhibiti na usimamizi wa Serikali.

Aliongeza kusema “Kwa nini tusipige kura ya kumwondoa?... Mheshimiwa Naibu Spika wewe kama kiongozi wetu ndio unapaswa kutuongoza kupiga kura ya kuwaondoa hawa watu.”
Mkosamali alisema wabunge wanatoa mapendekezo hayo kwa vile wameshindwa kufanya kazi ambayo walipatiwa na kusisitiza kuwa wameshawapima na kubaini kuwa hawawezi kazi tena.

“Hatuna chuki na mtu….Hata tukiwaambia tunajua hamtafanya tumeshawapima tunajua hamtaweza sasa tunawashauri nini tena?” alihoji Mkosamali wakati akijenga msingi wa hoja yake hiyo.

0 comments:

Post a Comment