Mkurugenzi wa zamani wa Utawala na Utumishi (DPA), Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Amatus Liyumba anayekabiliwa na kesi ya kukutwa na simu gerezani, ameiomba mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imfutie shtaka hilo na kumuachia huru kwa madai kuwa kesi hiyo ilipangwa kwa ajili ya kumkomoa.
Liyumba aliyaeleza hayo jana wakati akijitete mbele ya Hakimu Mkazi, Augustina Mmbando anayetarajia kutoa hukumu ya kesi hiyo, Januari 15, mwaka na kuzitaka pande zote mbili kuwasilisha majumuisho yao ya mwisho kama mshtakiwa ana hatia ama la, Desemba 30, mwaka huu .
“Kesi hii imepangwa kwa ajili ya kunikomoa, wakati natumikia kifungo sijawahi kuvunja sheria, kupewa adhabu wala kuonywa kwa kosa lolote, simu yenye namba 0653004662 siijui nimeiona hapa na kama imesajiliwa ni lazima mhusika atajulikana.” alieleza Liyumba.
Alidai kuwa, Julai 2011 alikuwa mfungwa akitumikia kifungo cha miaka miwili na unapofikishwa huko ni lazima upekuliwe mara tatu kwa kuvuliwa nguo zote.
Kutokana na utaratibu wa ulinzi gerezani, siyo rahisi kwa mfungwa ama mahabusu kuingia na simu
Julai 27, 2011 mchana nikiwa kwenye selo yangu na mtu mmoja ambaye ni mahabusu, tukisoma magazeti ghafla askari wawili akiwamo shahidi wa pili wa upande wa mashtaka, waliingia na kuniambia kuwa hii simu umeipataje wakati wakiwa wameishika mkononi.
Aliongeza kuwa tukio hilo kwake lilikuwa ni mshtuko na aliona ni kitu kilichopangwa na kwamba, wakati huo ilikuwa bado mwezi mmoja na nusu amalize kutumikia kifungo chake.
“Naamini walikuwa wananingojea, nilitafakari mlolongo wa matukio yanayonikuta, nilishtakiwa kwa kuambiwa nimesababisha harasa ya Sh261 bilioni shtaka ambalo liliondolewa na kupewa la kutumia madaraka vibaya, madaraka ambayo sina wala sijapewa huu ni uonevu.” alisema Liyumba.
Alibainisha kuwa wakati akiwa gerezani muda mfupi kabla ya kutoka watu wa Takukuru walimfuata na wakitaka kuandaa kesi dhidi yake, lakini aliwapinga kwa madai ya kutaka kuwasiliana na mwanasheria wake.
Alidai kuwa watu hao walimfuata tena na kwamba baada ya dulu hilo, akaona tukio hili la Julai 27,2011 la kubambikiwa kesi ya kukutwa na simu gerezani.
Alisisitiza kuwa simu na namba ya 0653004662 haifahamu, kama imesajiliwa mhusika atajulikana na iwapo atakuja mtaalamu ataeleza angalau ilipigwa kwa nani.
Liyumba anadaiwa kukutwa na simu ya mkononi akiwa gerezani Ukonga, Dar es Salaam, wakati akitumikia kifungo cha miaka miwili.
0 comments:
Post a Comment